Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akiwasha Mtambo maalum unaoruhusu kuwaka kwa umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, baada ya kuzima ule uliokuwa ukiwasha umeme wa mafuta ya dizeli, Aprili 8 mwaka huu.
Sehemu ya umati wa wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (waliokaa-katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa serikali, vyama vya siasa, TANESCO na REA baada ya hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka (wa pili-kushoto) akimweleza jambo Mbunge wa Ngara, Alex Gashaza (kulia), wakati wakimsubiri Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani kuwasili kwa ajili ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu. Wengine pichani ni viongozi mbalimbali kutoka wizarani, TANESCO na REA.
Na Veronica Simba - Ngara
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amefungua matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu hivyo kuwezesha Wilaya hiyo kuachana na matumizi ya umeme wa mafuta.
Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi huo, Waziri Kalemani alisema kuwa yeye pamoja na watendaji wote wa Wizara na Taasisi zake hususan TANESCO na REA, wamedhamiria kutekeleza kwa vitendo, azma ya Rais John Magufuli ya kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa uhakika nchini kote ili kuchochea uchumi wa viwanda.
“Serikali imekusudia kujenga uchumi wa viwanda na kuipeleka nchi kwenye uchumi wa kati. Hayo yote yanahitaji nishati ya uhakika, na ndicho tunachotekeleza.”
Alisema kuwa, mpango wa serikali ni kuiunganisha nchi nzima katika umeme wa Gridi ya Taifa ili wananchi wote wanufaike kwa kupata umeme wa aina moja.
Akifafanua Zaidi, Waziri kalemani alisema kuwa uunganishaji umeme wa Gridi ya Taifa umeshafanyika kutoka Mbagala Dar es Salaam kupitia Mkuranga, Kibiti, Ikwiriri, Utete, SomangaFungu hadi Lindi.
“Kwa sasa tunaendelea kuunganisha Lindi mpaka Mtwara ambapo kufikia mwisho wa mwezi huu, watanzania watakuwa wanatumia umeme wa Gridi ya Taifa kutoka pembe ya Kusini mwa nchi Mtwara hadi pembe nyingine ya nchi iliyopo Magharibi ambayo ni Ngara Kagera,” alisema.
Aidha, aliongeza kuwa, kazi iliyobaki ni kuunganisha upande mwingine wa nchi ambao unaanzia Mbeya kupitia Sumbawanga, Kigoma, Mpanda, Nyakanazi hadi Geita na Bulyanhulu. Alisema kazi hiyo inatarajiwa kukamilika ifikapo 2020/21.
Alitoa rai kwa wawekezaji wakubwa na wadogo kutumia nishati ya umeme katika kujenga uchumi wao binafsi na wa Taifa kwa ujumla.
Awali, akiwasilisha taarifa ya TANESCO Mkoa wa Kagera kwa Waziri Kalemani; Meneja wa shirika husika mkoani humo, Mhandisi Francis Maze, alisema kuwa mitambo ya kufua umeme wa mafuta ya dizeli ambayo ilikuwa inatumika awali wilayani Ngara, imekuwa ikiigharimu serikali takribani shilingi bilioni 2 kwa mwaka ukilinganisha na mapato ya shirika hilo ya shilingi milioni 540 tu kwa mwaka.
Aidha, alifafanua unafuu wa gharama ambazo TANESCO itapata kutokana na Mradi wa kuiunganisha Ngara katika Gridi ya Taifa ambapo alisema; Wilaya ya Ngara sasa itapata unafuu wa asilimia 73.4 katika gharama za kupata Uniti moja ya umeme.
“Wastani wa gharama ya kufua Uniti moja ya umeme kwa mitambo ya dizeli ni shilingi 578, ambayo ni kubwa sana ukilinganisha na gharama ya shilingi 154 kwa Uniti moja kwa umeme wa Gridi ya Taifa; ambayo ni sawa na asilimia 26.6 tu ya gharama ya umeme wa mitambo ya dizeli,” alifafanua.
Akizungumzia madhumuni ya mradi husika, Mhandisi Maze alisema ni pamoja na kuiwezesha Wilaya ya Ngara kuwa na umeme wa uhakika utakaowezesha kukua kwa uchumi kwa kasi, kupunguza gharama ya matumizi ya mafuta katika kufua umeme pamoja na kuandaa maunganisho ya Wilaya ya Ngara na Kituo kipya cha kupooza umeme wa Gridi kinachojengwa Nyakanazi wilayani Biharamulo.
Alitaja madhumuni mengine kuwa ni kuvipatia umeme vijiji 10 vinavyopitiwa na Mradi huo pamoja na kuwa chachu ya kutimiza sera ya serikali ya kila Wilaya kuwa na viwanda.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka, pamoja na kuipongeza Serikali, aliwashukuru wananchi wa Ngara na viongozi wao kwa kuunga mkono utekelezaji wa Mradi husika.
“Nafahamu hizi njia zimepita katika mashamba ya baadhi ya watu lakini mmeuthamini Mradi huu na hatujapata migogoro yoyote, hivyo tunawashukuru sana.”
Kwa upande wao, wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mtenjele na Mbunge wa Wilaya hiyo Alex Gashaza, waliipongeza Serikali kwa jitihada za dhati katika kuwaletea wananchi maendeleo kupitia upatikanaji wa umeme wa uhakika na wa gharama nafuu.
Viongozi wote waliwataka wananchi kuilinda miundombinu hiyo muhimu inayojengwa na serikali kwa gharama kubwa ili iendelee kuwanufaisha kwa muda mrefu na kuepusha hasara kwa Taifa.
Hafla ya ufunguzi huo ilihudhuriwa pia na viongozi wa vyama vya siasa, mwakilishi wa Kamishna wa Nishati Mhandisi Salum Inegeja, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Vestina Rwelengela pamoja na wananchi. Jumla ya wateja 482 watanufaika na mradi husika.
No comments:
Post a Comment