“Ndiyo ulikuwa mkataba wetu na si kwa maneno, lakini uliwekwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 75 mpaka 77 eneo kubwa limezungumzwa uchumi wa gesi na imeandikwa mafuta na gesi,” alisema.
Alisema kura nyingi alizozipata Rais Magufuli ni kwa sababu ya makubaliano hayo yaliyopo kwenye ilani hiyo kwamba atakwenda kuyaendeleza kwa kujenga miundombinu ya kuendeleza uchumi wa gesi Lindi na Mtwara.
“La pili ilikuwa kuwaandaa wananchi wanufaike na kufaidika na gesi na mafuta Lindi na Mtwara na lipo jambo mahsusi la ujenzi wa LNG plant (mtambo wa kuchakata gesi) kwa mikoa ya Lindi, hili limo kwenye ilani ya uchaguzi,” alisema.
Nape alisema anasikitika alipoangalia hotuba ya Waziri Mkuu kuanzia ukurasa wa kwanza hadi wa mwisho hakuna neno gesi.
Alisema hata kwenye shughuli zinazoendana na gesi huko ni kama vile zimeanza kufungwa na nyingine zimesimama.
“Swali langu la kwanza, hivi ni bahati mbaya kwamba hotuba ya Waziri Mkuu imeshindwa kuliona jambo hili kuwa ni kubwa na ikaamua kuliacha au Serikali imeamua kuachana nalo?” alihoji Nape aliyewahi kuwa waziri katika Serikali ya Awamu ya Tano.
Alisema anaona jitihada zinaanza kwenda kwenye umeme wa Stiegler’s Gorge jambo lisilo na ubaya lakini ilani ya CCM ilizungumza nishati ya gesi.
Alisema kwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa anatoka Lindi waliamini wapo salama. “Sasa ni bahati mbaya sana kwamba humu ndani hakuna kabisa, maana yake ni kwamba hili jambo pengine limeanza kuachwa sasa twende kwenye Stiegler’s lakini je, hatusaliti ilani ya uchaguzi ya CCM?”
Nape alisema baada ya harakati za gesi na mafuta Kusini, watu walianza kuwekeza Lindi na Mtwara na uchumi ukaanza kukua, lakini sasa wanaondoka na uchumi unadorora. Alimtaka Waziri Mkuu asikubali suala la gesi lifie mikononi mwake.
Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja akizungumzia gesi alisema, “Nimekuwa nikisikia Serikali ikisema mpango uliopo ni tukifika mwaka 2020 tuwe na megawati 5,000 na mwaka 2025 tuwe megawati 10,000.” Waziri huyo wa zamani wa nishati na madini alisema vyanzo vilivyopo vya maji ikiwamo Stiegler’s Gorge havizidi megawati 5,000 hivyo kuhoji mwaka 2021 kwenda 2025 kama hakutafanyika mipango ya kuendeleza gesi ni vipi zitapatikana.
Alisema kwa sababu bomba la gesi linatumika kwa asilimia sita tu kwa taarifa ambazo zimekuwa zikisikika na kubakia asilimia 94, ni vyema wakaendeleza miradi ya gesi.
Alisema sekta binafsi ipewe kipaumbele isaidiane na Serikali katika kuendeleza miradi hiyo.
Hata hivyo, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde alisema, “Ndugu yangu Nape amesimama akasema Waziri Mkuu anatoka Kusini na ni aibu kukosa maendeleo, najiuliza tuna waziri mkuu wa Kusini, tuna Rais wa Kanda ya Ziwa, tuna Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jamani!”
Alitaka wasiwafanye viongozi wao wakawa wa kanda kwani watakuwa hawatendi haki, “Hivi na sisi ambao Spika unatoka Dodoma mbona unawapa wao kusema, kwa nini usituruhusu sisi wa Dodoma tuseme sana ili shida zetu zisikike. Hili jambo lazima tujue viongozi wakishakuwa wa kitaifa wanaongoza Taifa na si sehemu walipotoka,” alisema.
Alitaka wabunge kutowagawa viongozi kwa sehemu wanapotoka na kwamba wanataka maendeleo na nchi ni kubwa Serikali haiwezi kupeleka maendeleo kila mahali.
Mbali ya Lusinde, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma alimpa taarifa Nape kuwa hata mbunge aliyemuachia jimbo (Bernard Membe) hakupeleka maendeleo jimboni kwake ingawa alikuwa waziri wa mambo ya nje na kwamba wafadhili wote aliokuwa akizungumza nao hakuwapeleka Mtama, bali Geita.
Sukari na dawa za kulevya
Hoja nyingine iliibuliwa na Mbunge wa Welezo (CCM), Saada Mkuya Salum ambaye alisema bila wabunge kutoka Zanzibar, Bunge haliwezi kuitwa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Zanzibar kuna sheria zake. sheria zipo na changamoto zipo kila sehemu. Bunge lililopita naambiwa kuna mheshimiwa mmoja aliwahi kusema Zanzibar haijawahi kukamata hata kilo moja ya cocaine,” alisema Saada.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Halima Bulembo alimpa taarifa Saada kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ukimwi, Oscar Mukasa ndiye aliyezungumza kuhusu suala la wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Alisema mwenyekiti huyo alisema dawa hizo zimedhibitiwa Tanzania Bara lakini Zanzibar bado.
Mbunge wa Konde (CUF), Khatibu Said Haji alimpa taarifa Saada kuwa kuna kontena la dawa za kulevya lilikamatwa Zanzibar na kesi hadi sasa iko mahakamani.
Awali, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Kemilembe Lwotta alisema kamati ilibainisha kuwa kazi kubwa imefanyika Bara lakini wafanyabiashara wengi wamehamia Zanzibar.
Wapinzani watoka ukumbini, moshi wavunja kikao
Katika hatua nyingine, wabunge wa CUF walitoka ndani ya ukumbi jana baada ya Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu kuzuia mjadala wa Muungano. Kabla ya kuzuia, mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Mariam Msabaha alisema Serikali ya Muungano inaiminya Zanzibar na kushindwa kujitangaza kimataifa.
Mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka alisema wabunge wa CCM wanaiumiza Zanzibar na nia yao si njema kuhusu muungano.
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais, Kangi Lugola aliomba mwongozo na kutaka atajwe mbunge anayepinga muungano. Mwongozo huo ulisababisha kelele wabunge wa upinzani wakimtaja Ally Keissy wa Nkasi Kaskazini.
Katika hatua nyingine kikao cha Bunge kiliahirishwa kabla ya muda jana baada ya kutokea moshi ndani ya ukumbi ukielezwa kusababishwa na simu iliyoungua.
Zungu aliahirisha shughuli za Bunge akisema moshi uliotokea wakati Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige akichangia ungeweza kuathiri afya za wabunge.
Kikosi cha zimamoto na maofisa wengine waliitwa wakati wabunge wakitoka ndani ya ukumbi.
Nyongeza na Habel Chidawali
No comments:
Post a Comment