ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA
POLAND NCHINI 11-13 APRILI 2018
Waziri wa Mambo ya Nje wa
Jamhuri ya Poland, Mhe. Prof. Jacek Craputowicz atafanya ziara ya kikazi nchini
Tanzania kuanzia tarehe 11 hadi 13 Aprili 2018.
Katika ziara hiyo, Prof. Craputowicz pamoja na mambo mengine, atafanya
mazungumzo na mwenyeji wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) Jijini Dar Es Salaam tarehe 12
Aprili 2018. Viongozi hao watajadili
namna ya kuboresha mahusiano na mashirikiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania
na Poland, hususan katika eneo la uwekezaji na biashara.
Poland ni moja ya nchi zinazounga
mkono Sera ya Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda ifikapo mwaka
2020. Katika kuunga mkono Sera hiyo, Serikali ya Poland imetoa mkopo wa
masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 110 kwa Serikali ya Tanzania.
Kati ya fedha hizo, Dola
za Marekani milioni 55 zimetumika kujenga kiwanda cha kuunganisha matrekta Wilayani
Kibaha, Mkoani Pwani ambacho kimeshaanza kazi na Dola za Marekani milioni 55 ni
kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ya kilimo katika mikoa minane
ya Rukwa, Katavi, Manyara, Ruvuma, Dodoma, Shinyanga, Njombe na Songwe.
Prof.
Craputowicz na mwenyeji wake watashiriki hafla fupi ya uzinduzi rasmi wa ofisi
ya Ubalozi wa nchi hiyo zilizopo nyumba namba 15, mtaa wa Mtwara, Masaki Jijini
Dar es Salaam tarehe 12 Aprili 2018. Poland ilifungua upya Ubalozi wake nchini
mwaka 2017 baada ya kuufunga mwaka 2008 na kabla ya hapo nchi hiyo ilikuwa
inawakilishwa kutokea Nairobi, Kenya.
Baada
ya ufunguzi viongozi hao watafanya mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi
hizo saa tano asubuhi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
10 Aprili, 2018
No comments:
Post a Comment