ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 19, 2018

WANAHISA CRDB WATAKIWA KUNUNUA HISA KWA WING


PICHANI: Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles Kimei akizungumza kwenye semina ya Wanahisa wa benki hiyo. Semina hiyo imefanyika leo Mei 18, 2018 kwenye Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha ikiwa ni utangulizi wa Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB kesho Mei 19, 2018. (Picha Zote na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Mtoa mada kwenye semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB Dkt. Blandina Kilama iliyofanyika leo Mei 18, 2018 Ukumbi wa AICC jijini Arusha. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).


Wanahisa wa Benki ya CRDB wakisikiliza watoa mada (hawapo pichani) kwenye semina iliyofanyika leo Mei 18, 2018 kwenye Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha, ikiwa ni utangulizi wa Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB kesho Mei 19, 2018. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).
Mtoa mada kwenye semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB Grace Joachim. Semina hiyo imefanyika leo Mei 18, 2018 kwenye Ukumbi wa Simba (AICC) jijini Arusha ikiwa ni utangulizi wa Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa Benki ya CRDB kesho Mei 19, 2018. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog. Arusha

WANAHISA wa Benki ya CRDB wameshauriwa kununua hisa kwa wingi ili kuweza kujiletea maendeleo, kwani ununuaji wa hisa hasa wakati kampuni husika imepata mgogoro wa muda mfupi bei yake inashuka.

Hayo yalisemwa leo Mei 18, 2018 na mtoa mada Dkt. Blandina Kilama kwenye Semina ya Wanahisa wa Benki ya CRDB iliyofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC) jijini Arusha.

Dkt. Kilama alisema wanahisa hao wanatakiwa kununua hisa bei zikiwa ndogo na kuuza hisa hizo bei ikiwa kubwa, lakini pia wanatakiwa kununua hisa muda mfupi kabla ya gawio, kwani uhitaji wa hisa hupanda.

"Nunua hisa bei inapokuwa ndogo, uza hisa bei inapokuwa kubwa. Uza hisa kabla ya gawio, kwani uhitaji wa hisa husika hupanda. Na pia nunua hisa muda baada ya dirisha la gawio kufungwa, uhitaji wa hisa husika hushuka. Pia nunua wakati kampuni imepata mgogoro au changamoto ya muda mfupi, kwani bei hushuka, na nunua hisa iwapo thamani inapanda

"Tunawekeza tukiwa na matarajio ya kupata faida katika uwekezaji wetu. Hili laweza kuwa lengo la muda mfupi au mrefu. Changanya hisa za muda mfupi na mrefu, kampuni ambayo inatoa gawio ama ongezeko la thamani, changanya hisa za huduma na viwanda, mfano usafiri na kuchakata vyakula, changanya makampuni mapya na makongwe, kampuni yenye kukua kama ya nishati ama kampuni ambayo imekuwepo muda mrefu" alisema Dkt. Kilama.

Dkt. Kilama amesema watu wengi hawana mpango mkakati wa kimaendeleo, na wenye mkakati huo hawajauandika, hivyo ili mtu kuendelea anahitaji kuweka mkakati ulioandikwa, utamuwezesha kuwa na kumbukumbu, lakini pia kumuwezesha kufanikiwa.

"Tengeneza mpango mkakati binafsi na uutathmini kila wakati. Katika kutekeleza mpango wako wa mwaka, tenga fedha za kutosha kwa ajili ya hisa kila mwezi. Pia katika kutekeleza mpango wako wa kila mwaka, tenga muda wa kutosha kwa ajili ya kutathmini hisa kila mwezi" alisema Dkt. Kilama.

Dkt. Kilama amewataka wanahisa hao kutumia Soko la Hisa kama njia ya kujiongezea mtaji wa awali, kutekeleza maamuzi yako na kuyasimamia na kuona mtu anafanikiwa. Kesho Mei 19, 2018, Mkutano Mkuu wa 23 wa Wanahisa wa CRDB ndiyo utafanyika, ambapo mambo mbalimbali ya benki hiyo yatazungumziwa.

2018-04-21 21:05 GMT+03:00 Imma Mbuguni : HABARI WADAU, POKEA CODES KWA MATUMIZI TAFADHALI ASANTE
PICHANI: Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala (fulana nyekundu) akiwa na uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) pamoja na baadhi ya washiriki wa mbio za Ngorongoro Marathon zilizofanyika leo Aprili 21, 2018. Wengine ni Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Profesa Abiud Kaswamila (namba 002), Mhifadhi Mkuu wa NCAA Dkt. Fred Manongi (namba 003) na Meneja Mahusiano wa NCAA Joyce Mgaya (kulia waliosimama). (Picha na Yusuph Mussa Immamatukio Blog).

Na Yusuph Mussa, Karatu
Immamatukio Blog

WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala ametuma salamu kwa majangilli wanaojihusisha na uwindaji haramu wa wanyama kwenye Hifadhi za Taifa ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA).

Amesema Serikali na wadau wengine wamejipanga kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa kwa kudhibiti ujangili wa wanyama na viumbe hai vyote vinavyotokana na maliasili yetu ya asili kwenye hifadhi za Taifa.

Dkt. Kigwangala alituma salamu hizo kupitia Mbio za Ngorongoro Marathon zilizofanyika leo Aprili 21, 2018 kwa kuanzia Lango Kuu la kuingilia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na kuishia Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu mkoani Arusha.

Pamoja na kuwa mgeni rasmi kwenye mbio hizo, Dkt. Kigwangala pia alikimbia kilomita 21 kuanzia saa 3.30 asubuhi na kumaliza saa 6.20 mchana, na kusema hiyo ni ishara tosha ya kujipanga na kukabiliana na majangili. Dkt. Kigwangala alisema kwa kumaliza mbio hizo, sio tu anawatishia majangili kuwa yupo vizuri kukabiliana nao, bali anataka askari wote wa wanyama pole wawe wakakamavu na asimuone askari yeyote mwenye kitambi.

"Moja ya malengo ya mbio za Ngorongoro Marathon kwa mwaka huu ni kupambana na ujangili na majangili. Na sikumaliza mbio hizi za kilomita 21 kwa bahati mbaya, bali ni kuwadhihirishia majangili na watu wote wenye nia mbaya na rasilimali zetu kuwa nipo fiti.

"Lakini sio kwa majangili, hata kwa askari wetu, nataka kuwaeleza kuwa kuanzia sasa sitaki kuona askari anakuwa na kitambi. Hatuwezi kupambana na majangili kama askari wetu wana vitambi na wapo legelege... Na nataka kuwaeleza askari kama wanataka twende nao pamoja kwenye hili basi wajipange" alisema Kigwangala.

Dkt. Kigwangala alisema nia nyingine ya NCAA kudhamini mbio hizo ni kutangaza shughuli za utalii ndani na nje ya nchi, kwani anaamini kupitia waandishi wa habari na washiriki wa mashindano hayo kutokea ndani na nje ya nchi, itawezesha kuongeza watalii na hifadhi hiyo kujulikana zaidi.

Naye Rais wa Chama cha Riadha nchini (RT) Anthony Mtaka, alisema moja ya mambo yanayotushinda nchini ni kujitangaza, lakini hapo hapo kushindwa kupenda vya kwetu, kwani pamoja na kuwa Mlima Kilimanjaro upo Tanzania, lakini matangazo yake mengi yapo Kenya.

Mtaka ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu alisema amefurahishwa na uongozi wa NCAA kudhamini mashindano hayo, kwani yatawezesha Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufahamika duniani kote.

"Kwenye Serikali ukiwa na mtu kama Dkt. Fred Manongi (Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) mambo yatakwenda vizuri. Tumempa taarifa wiki mbili kabla ya mashindano kumuomba atudhamini, lakini akawa amekubali na mambo yamekwenda vizuri.

"Hiki cha kukubali kudhamini mashindano haya ni kikubwa sana. Sasa anatufanya Watanzania tuanze kujitangaza na kupenda vya kwetu. Hili tatizo la kushindwa kujitangaza ni kubwa ndiyo maana kila siku kuna malalamiko kuwa Kenya wanajitangaza Mlima Kilimanjaro ni wa kwao. Sisi sasa tujitoe na kuonesha rasilimali hizi za utalii ni za kwetu" alisema Mtaka.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala akionesha medali yake kwa waandishi wa habari mara baada ya kumaliza mbio za Ngorongoro Marathon (kilomita 21). Alimaliza mbio hizo saa 6.20 mchana. Mbio hizo zilizoanza leo Aprili 21, 2018 saa 3.30 asubuhi kwenye lango kuu la kuingia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), zimehitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu. NCAA ndiyo wadhamini wakuu wa mbio hizo. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala akihutubia wananchi wa Wilaya ya Karatu mkoani Arusha mara baada ya kumalizika mbio za Ngorongoro Marathon leo Aprili 21, 2018 na kuhitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu. Wa pili kulia ni Rais wa Chama cha Riadha (RT) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka na kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya NCAA Profesa Abiud Kaswamila. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).
Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Dkt. Fred Manongi (kulia), Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karatu Jubilate Mnyenye (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Arusha Cecilia Pareso (katikati) wakimsikiliza Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangala (hayupo pichani) kwenye kilele cha mbio za Ngorongoro Marathon zilizohitimishwa kwenye Uwanja wa Mazingira Bora mjini Karatu leo Aprili 21, 2018. (Picha na Yusuph Mussa, Immamatukio Blog).

2018-03-04 17:22 GMT+03:00 Imma Mbuguni : HABARI WADAU, POKEA CODES TAFADHALI, Mbunge wa Korogwe Mjini Mary Chatanda (wa tatu kulia) akisikiliza taarifa inayosomwa na Mkuu wa Shule ya Sekondari Joel Bendera Nasson Msemwa (wa pili kushoto). Hapo ndipo Chatanda aliliamsha 'dude' kutaka kujua kwa nini sh. milioni 150 zimeshindwa kukamilisha mabweni mawili.

Yussuph Mussa, Korogwe
IMMAMATUKIO BLOG

Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga Mary Chatanda amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Korogwe Jumanne Shauri kupeleka wakaguzi kwenye Shule ya Sekondari Joel Bendera iliyopo Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi.

Ni kutaka kubaini ukweli kuhusu matumizi ya fedha baada ya sh. milioni 150 zilizopelekwa shuleni hapo kumalizika, kabla ya ujenzi wa mabweni mawili kumalizika, huku tena zikihitajika sh. milioni 17 kumalizia ujenzi huo.

Chatanda alibaini hilo baada ya Machi 3, 2018 kufanya ziara kata ya Kwamsisi, na kusomewa taarifa na Mkuu wa Shule hiyo Nasson Msemwa kudai sh. milioni 150 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kujenga mabweni hayo ikiwa ni pamoja na kuweka samani, fedha zake zimekwisha.

"Mheshimiwa Mbunge, Serikali ilituletea sh. milioni 230, ambapo sh. milioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili ya wasichana na wavulana na sh. milioni 80 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mapya manne. Fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ambapo tupo kwenye hatua za mwisho zimekwisha. Na ili tukamilishe mabweni hayo kunahitajika sh. milioni 17.

"Kwa upande wa ujenzi wa madarasa manne, bado tunakwenda vizuri, kwani pamoja na ujenzi kuwa kwenye hatua za mwisho, bado tuna sh. milioni 28" alisema Msemwa.

Chatanda alisema kwa uzoefu wake, tangu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, na sasa Mkuu wa Wilaya ya Geita Mhandisi Robert Gabriel, wamekuwa wakijenga namna hiyo kazi inakamilka na fedha inabaki, iweje kwao imekwisha kabla ya kazi kumalizika.

"Sisi tuna uzoefu, kwa pesa hizi mlizoletewa na Serikali, mnapowashirikisha wananchi kuchimba msingi, kuleta mchanga na kokote, huku mkitumia mafundi wa kawaida, fedha hizi zingetosha na kubaki. Hili sikubaliani nalo, na ninamtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kuleta wakaguzi ili kubaini ukweli wa matumizi wa hizi fedha.

"Mnataka tuonekane kazi hii ya kufanya vizuri kujenga madarasa na mabweni na kudhibiti matumizi ilikuwa inafanywa na mtu mmoja Robert Gabriel (sasa Mkuu wa Mkoa wa Geita. Nina hakika Bodi ya Shule haikuwashirikisha wananchi ndiyo maana mabweni hayakuisha, lakini kama hamkushirikisha wananchi na viongozi wa vijiji na kata, ambao ndiyo wenye shule yao, maana yake kuna chembechembe za ubadhirifu" alidai Chatanda.

Diwani wa Kata ya Kwamsisi Nassor Mohamed alisema Bodi ya Shule awali wakati wanaanza ujenzi wa shule hiyo kwa njia ya msalagambo chini ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Mhandisi Gabriel, walishirikisha watu wote, lakini baada ya Serikali kuingiza sh. milioni 230 kwenye akaunti ya shule, mambo yalibadilika.

"Mwanzo walitushirikisha, lakini fedha zilipoingia Bodi ya Shule ilikuwa inafanya kazi peke yake bila kushirikisha viongozi wa vijiji wala kata, muulize Mkuu wa Shule huyu hapa, alikuwa mbogo pindi ninapomuulizia mambo yanayohusu fedha ama maendeleo ya ujenzi" alisema Mohamed.

Akijibu tuhuma hizo, Msemwa alisema hakuna fedha imeliwa, bali mabweni hayo ni makubwa tofauti na Shule ya Sekondari Mnyuzi, kwani kila moja linachukua wanafunzi 40, lakini yupo tayari kukaguliwa.

Kaimu Mkurugenzi wa Mji Korogwe Dkt. Elizabeth Nyema, ambaye alikuwa ameambatana na Chatanda kwenye ziara hiyo, alisema amepokea maagizo hayo na watayafanyia kazi.
Madarasa mapya manne ya Shule ya Sekondari Joel Bendera, Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi, Halmashauri ya Mji Korogwe. Madarasa hayo ambayo yapo kwenye hatua za mwisho kukamilika, Serikali ilitenga sh. milioni 80 kujenga madarasa hayo. (Picha na Yusuph Mussa).
Moja ya mabweni yaliyopo Shule ya Sekondari Joel Bendera Kijiji cha Kwakombo, Kata ya Kwamsisi, Halmashauri ya Mji Korogwe. Mabweni mawili yaliyojengwa shule hiyo, kila moja litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kwa wakati mmoja.

PICHA ZOTE NA YUSSUPH MUSSA

No comments: