Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adam Mgoyi akisisitiza kuhusu wananchi
kutumia hati za kimila za kumiliki ardhi kujiletea maendeleo ikiwemo
kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha wakati wa hafla ya
kuwakabidhi wananchi wa Kijiji cha Magubike Wilayani Kilosa hati hizo
zilizotolewa baada ya maeneo yao kurasimishwa kwa kupimwa .
Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge
Tanzania ( MKURABITA) Bi. Serapia Mgembe akisisitiza umuhimu wa hati za
kimila za kumiliki ardhi katika kuchochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa
wananchi wakati wa hafla ya kutolewa kwa hati hizo kwa wananchi wa
Kijiji cha Magubike Wilayani kilosa ambapo Mpango huo kwa kushirikiana
na Halmashuri ya Wilaya hiyo wamefanikisha upimaji wa ardhi katika
Vijiji 37.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adam Mgoyi akimkabidhi mmoja wa wananchi wa Kijiji cha Magubike hati kimila ya kumiliki ardhi .
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adam Mgoyi akisalimiana na viongozi wa
Kijiji cha Magubike kabla ya kuanza kwa hafla ya kutoa hati za kimila
kwa wananchi wa Kijiji hicho.
Mkurugenzi wa Urasimishaji
kutoka MKURABITA Bw. Japhet Werema akisisitiza umuhimu wa mpango wa
kurasimisha ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Magubike Wilayani Kilosa
wakati wa hafla ya kutoa hati za kimila za kumiliki ardhi kwa wananchi
wa Kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Bw. Adam Mgoyi (katikati) akiwa kwenye picha ya
pamoja na wananchi walipata hati za kimila katika Kijiji cha Magubike
Wilayani Kilosa pamoja na Watendaji wa Halmashuri na wale wa
MKURABITA.
Mratibu wa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za
Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Bi. Serapia Mgembe akifurahia ngoma za
asili pamoja na kikundi cha ngoma hizo katika Kijiji cha Magubike
Wilayani Kilosa wakati wa hafla ya kukabidhi hati kwa wananchi wa Kijiji
hicho.
Kikundi cha ngoma za asili cha Kijiji cha Magubike kikionesha umahiri
wake katika kucheza ngoma hizo wakati wa hafla ya kukabidhi hati za
kimila za kumiliki ardhi kwa wananchi wa Kijiji hicho.
Sehemu ya wananchi wakifuatilia hafla hiyo ya kutolewa kwa hati za
kimila za kumiliki ardhi katika Kijiji cha Magubike Wilayani Kilosa.
Mratibu wa Mratibu wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania(MKURABITA) Bi. Serapia Mgembe akiwasikiliza baadhi ya wananchi mara baada ya hafla ya kutoa hati za kimila za kumiliki ardhi kwa wananchi wa Kijiji cha Magubike.
(Picha zote na Frank Mvungi- MAELEZO, Magubike- Kilosa)
Frank Mvungi- MAELEZO, Morogoro
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro Bw. Adam Mgoyi amewata wananchi kutumia fursa zinazotokana na urasimishaji ardhi uliowezesha kutolewa kwa hati zaidi ya 300 za kimila za kumiliki ardhi kwa wakazi wa Kata ya Magubike Wilayani humo jana.
Akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji hicho waliojitokeza katika hafla ya kutolewa kwa hati hizo amesema kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuleta ukombozi wa kiuchumi kwa wananchi wake kupitia mpango wa matumizi bora ya adhi uliotekelezwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) na Halmashuri ya Wilaya hiyo.
“Tumieni hati hizi kutatua changamoto za kiuchumi kwani zinawawezesha kupata mitaji kutoka katika taasisi za fedha zilizopo ambazo zimeonesha nia yakuwawezesha wananchi na nyingine zimeanza kutoa mikopo kwa wananchi wetu wenye hati za kimila” Alisisitiza Mgoyi.
Akifafanua amesema kuwa hati hizo zitasaidia kuondoa migogoro ya ardhi, kuongeza thamani ya ardhi na kuwapa wananchi uwezo wa kujiendeleza kiuchumi ambapo tangu MKURABITA ianze zoezi la urasimishaji ardhi Wilayani humo wananchi wengi wamenufaika na mikopo iliyowawezesha kuwa na kilimo chenya tija.
Aliongeza kuwa Vijiji 37 vimenufaika na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Wilaya ya Kilosa ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“ Halmashuri ya Wilaya inao wajibu wa kutenga sehemu ya mapato yake ya ndani kuwawezesha wananchi katika upimaji wa ardhi na kuleta mpango bora wa matumizi ya Ardhi” Alisisitiza Mgoyi.
Pia kwa kuzingatia umuhimu wa kurasimisha ardhi Mgoya alibainisha kuwa mpango huo unasaidia kubainisha maeneo ya ufugaji na yale ya kilimo katika Wilaya hiyo.
Kwa upande wake Mratibu wa MKURABITA Bi. Serapia Mgembe amesema kuwa wananchi wa Wilaya hiyo ambao maeneo yao yamerasimishwa na kupimwa watumie fursa hiyo kushiriki katika kujiletea maendeleo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa.
Aliongeza kuwa Serikali inafanya jitihada kubwa kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na maisha bora hivyo jukumu lao ni kuunga mkono kwa kutumia fursa zinazoletwa na Serikali kupitia mpango wa matumizi bora ya Ardhi uliwawezesha kupimwa na hatimaye kuwapatia hati za kimila za kumiliki maeneo hayo.
Mpango wa Kurasimisha Biashara na Rasilimali za Wanyonge Tanzania umetajwa kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Kilosa na hivyo kuleta ustawi wa wananchi kiuchumi baada ya kupata hati za kimila za kumiliki maeneo yao yakiwemo mashamba na Viwanja.
No comments:
Post a Comment