TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania kupokea Watalii 10,000 kutoka Shanghai mwaka 2019
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) imesaini makubaliano na kampuni ya Touchroad International Group ya China kwa ajili ya kusafirisha watalii 10,000 kutoka jiji la Shanghai kutembelea Tanzania mwaka 2019 kwa kutumia ndege Maalum (chartered flights).
Makubaliano hayo yalisainiwa sambamba na mikutano ya kutangaza utalii katika soko la China- Tourism Roadshow katika miji mitano ya China iliyoanza katika jiji la Shanghai tarehe 12 Novemba 2018.
Mikutano hiyo ni matokeo ya jitihada za Ubalozi wa Tanzania nchini China kwa kushirikiana na TTB ambapo katika mkutano wa kwanza uliofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Aloyce Nzuki, washiriki mbalimbali zaidi ya 200 walijitokeza wakiwemo makampuni ya utalii (tour operators), mawakala wa usafirishaji (travel agents), mashirika ya ndege (airlines), na vyombo vya habari.
Katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii, Bi. Devotha Mdachi alitoa mada maalum kuhusu vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania pamoja na fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii.
Aidha, makampuni ya utalii kutoka Tanzania yalipata fursa ya kuelezea packages zao za utalii mahsusi kwa soko la China.
Kadhalika, Shirika la Ndege la Tanzania lilitumia fursa hiyo kutangaza juu ya mpango wake wa kuanza safari za moja kwa moja kutoka Tanzania hadi China katika mji wa Guangzhou mwezi Februari 2019.
Mikutano ya kutangaza utalii itaendelea kufanyika katika miji mingine ikiwa ni pamoja na Guangzhou tarehe 14 Novemba 2018, Hong Kong tarehe 16 Novemba 2018, Chengdu tarehe 19 Novemba 2018 na Beijing tarehe 20 Novemba 2018
-Mwisho-
Imetolewa na: Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dodoma, 13 Novemba 2018
Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki akitoa neno la ukaribisho katika mkutano wa kutangaza vivutio vya utalii uliofanyika Shaghai, China tarehe 12 Novemba 2018. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bi. Devotha Mdachi, Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo na viongozi wa kampuni ya Touchroad International Group wakiwa katika furaha baada ya kukamilika uwekaji saini wa makubaliano ambapo kampuni hiyo italeta watalii 10,000 nchini Tanzania mwaka 2019. Wajumbe wameshika shuka la kimasai ambalo linaonesha utamaduni wa kabila hilo maarufu kutoka Tanzania. Baadhi ya Washiriki wakiwemo viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii, TTB na Balozi wa Tanzania nchini China wakiwa katika mkutano huo. |
No comments:
Post a Comment