ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 11, 2018

Mikataba ya wakandarasi wa umeme vijijini kupitiwa na wanasheria wa Serikali

 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati), akimsikiliza Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Haji Janabi wakati wa kikao kazi na watendaji wa REA na TANESCO na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka REA, TANESCO na Wizara ya Nishati. Wengine katika picha ni Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka (wa pili kulia) na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga  (wa kwanza kulia).
 
Baadhi ya watendaji wa REA na TANESCO na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka REA, TANESCO na Wizara ya Nishati wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani)  wakati wa kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameeleza kuwa, Wanasheria wa Wizara ya Nishati, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wataanza kupitia mikataba ya wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini ili kuchukua hatua za kuwawajibisha wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo kwa kusuasua.

Aliyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao chake na Mameneja wa TANESCO wa Kanda, Mikoa, Wilaya na wasimamizi wa miradi ya usambazaji umeme vijijini kutoka Wizara ya Nishati, REA na TANESCO.

“ Yako baadhi ya maeneo ambayo Wakandarasi hawafanyi vizuri kama vile Mtwara, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Shinyanga, Singida, Tabora (Kaliua, Uyui, Urambo), Dodoma na Tanga (Wilaya ya Korogwe, Mkinga na Pangani), ambao utekelezaji wao katika mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa kwanza, wako chini ya asilimia 20,” alisema Mgalu.

Naibu Waziri alitoa agizo kuwa, wakandarasi katika maeneo hayo wahakikishe kuwa, wanafanya kazi kwa kasi na ufanisi ikiwemo kuweka magenge mengi ya kazi, uwepo vifaa na wasimamizi wa miradi wa kutosha ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria na Serikali na pia kutorudisha nyuma juhudi za Serikali za kusambaza umeme vijijini.

Kuhusu hali ya usambazaji umeme vijijini, Mgalu alisema kuwa, kuanzia Januari mwaka 2017 hadi sasa jumla ya vijiji 1,098 vimesambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme wa Awamu ya Tatu Mzunguko wa Kwanza, Mradi wa Makambako-Songea, Mradi wa Backbone na miradi ya umeme iliyo nje ya gridi.

Hivyo kwa ujumla alisema kuwa, hadi sasa jumla ya vijiji 5,493 vimesambaziwa umeme nchini na vijiji vilivyosalia ni 6,775 ambavyo vinaendelea kusambaziwa umeme kupitia REA III mzunguko wa kwanza na wa pili.

Aidha, Naibu Waziri wa Nishati, aliwakumbusha wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha kuwa miradi husika inaleta tija kwa jamii kwa kuunganisha nishati hiyo katika sehemu mbalimbali zinazotoa huduma za kijamii kama vituo vya afya na katika shughuli zinazokuza uchumi wa wananchi kama vile mashine za kusaga na kukoboa nafaka au sehemu za biashara.

Vilevile, Naibu Waziri wa Nishati aliwakumbusha wakandarasi na wasimamizi wa miradi  ya umeme vijijini kuhusu kutekeleza agizo la Serikali la kuwasha umeme katika vijiji vitatu  kila Wiki na kununua vifaa vya umeme vinavyozalishwa hapa nchini.

Hata hivyo, alisema kuwa viwanda vinavyozalisha vifaa hivyo chini ya ubora unaotakiwa vitaanza kuchukuliwa hatua kwani vinachelewesha kazi ya usambazaji umeme nchini.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati katika kikao hicho, Haji Janabi alitoa pongezi kwa Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Nishati kwa kusimamia ipasavyo utekelezaji wa  miradi mbalimbali ya umeme na kuwa na ari ya kufanya kazi, usiku na mchana.

Aidha alitoa wito kwa watendaji wa Wizara ya Nishati na Taasisi kufanya kazi kwa bidii kama ilivyo kwa viongozi hao wa Wizara na kuwa wabunifu. Alisema kuwa,  baada ya kikao kazi hicho, Wizara na Taasisi zitatekeleza ipasavyo maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri na kusimamia miradi ya usambazaji umeme vijijini.


Kikao hicho kilihudhuriwa na Kamishna Msaidizi wa Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dkt Tito Mwinuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.

No comments: