ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 11, 2018

MKURABITA Yawajengea Uwezo Wajasiriamali 1000 Singida ili Waweze Kurasimisha Biashara Zao

  Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri akizungumzia faida za kurasimisha Biashara kwa wajasiriamali wa mjini Singida wakati akifungua mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini humo (hawapo pichani) yaliyolenga kuwajengea uwezo ili warasimishe Biashara zao, Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kushirikina na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
 Sehemu ya Washiriki wa Mafunzo yakuwajengea uwezo wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini Singida wakifuatilia hotuba ya Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri wakati wa hafla yakufungua mafunzo hayo mjini humo Novemba 10, 2018.
 Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Alhaji Gwae Mbua akisisitiza jambo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini Singida (hawapo pichani) wakati wa hafla ya kufungua mafunzo kwa wajasiriamali hao mjini humo mapema Novemba 10, 2018. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri na Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Urasimishaji kutoka MKURABITA Bw. Japhet Werema.
 Kaimu Mkurugenzi wa Urasimishaji kutoka MKURABITA Bw. Japhet Werema (katikati) akisisitiza jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri (kulia) mara baada ya hafla ya kufungua mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini humo yaliyolenga kuwajengea uwezo ili warasimishe Biashara zao, Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kushirikina na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
 Meya ya Halmashauri ya Manispaa ya Singida Alhaji Gwae Mbua (kushoto) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri  katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mwenge ya Mjini Singida wakati wa hafla ya kufungua mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini humo yaliyolenga kuwajengea uwezo ili warasimishe Biashara zao, Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kushirikina na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya watoa mada katika mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini humo yaliyolenga kuwajengea uwezo ili warasimishe Biashara zao, Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kushirikina na Halmashauri ya Manispaa ya Singida. 
 Mkuu wa Wilaya ya Singida Bw. Pascas Muragiri (katikati walioketi) akiwa kwenye picha ya pamoja na sehemu ya washiriki na watoa mada wa mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 wa mjini humo yaliyolenga kuwajengea uwezo ili warasimishe Biashara zao, Mafunzo hayo yanaendeshwa na Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) kwa kushirikina na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
(Picha zote na MAELEZO- Singida)


Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) unaendesha mafunzo yakuwajengea uwezo wajasiriamali 1000 wa Mkoani Singida ikiwa ni hatua mojawapo yakuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa uchumi kwa kufanya biashara katika mfumo rasmi.
Akizungumza mjini Singida wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo  leo mjini humo, Mkuu wa Wilaya hiyo Bw.Pascas Muragiri amesema kuwa  mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambapo Serikali inasisitiza wajasiriamali kufanya biashara katika mfumo rasmi ili waweze kukuza biashara zao na kuongeza tija.
“Mafunzo haya ni nyenzo muhimu kwa wajasiriamali wetu hapa Singida kwani yatawawezesha kuwa na uwezo wa kutambua na kuzingatia taratibu zote zinazosimamia biashara hali inayotoa fursa kwao kurasimisha biashara zao.” Alisisitiza Muragiri.
Akifafanua amesema kuwa katika mafunzo hayo wajasiriamali hao watajifunza namna ya kutunza hesabu, Urasimishaji, taratibu za kupata leseni za biashara,umuhimu wa kutunza kumbukumbu za biashara na umuhimu wa bima ya afya.
Aliongeza kuwa wajasiriamali hao wanajukumu la kuzingatia yale watakayojifunza wakati wa mafunzo hayo na hivyo kuendana na dhamira ya Serikali kuwawezesha kukuza uwezo wa kufanya biashara baada ya kurasimisha biashara zao hali itakayowawezesha kupata mikopo katika taasisi za fedha ili kukuza mitaji yao na pia kuwezesha kukua kwa biashara katika mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia faida za mafunzo hayo amesema kuwa ni pamoja na kuwafanya wajasiriamali hao kutambulika, kuondoa usumbufu uliokuwepo awali, kuondoa urasimu kutokana na kuwepo kwa kituo kimoja cha huduma katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida kitakachojumuisha taasisi zote zinazohudumia wajasiriamali .
Alieleza kuwa kuwepo kwa Kituo hicho kutasaidia kuondoa ucheleweshaji wa huduma kwa wajasiriamali ambapo aliwataka watendaji wa Serikali kuepuka vitendo vya urasimu ili kuendana na dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwainua wajasiriamali hasa wanyonge. 
Mada mbalimbali zinatolewa na wataalam kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, MKURABITA, BRELA, TRA, Benki za CRDB na NMB, NSSF, SIDO, TCCIA ambapo Mragiri aliwataka wajasiriamali hao kutekeleza kwa vitendo yale watakayojifunza ili waweze kurasimisha  biashara zao. 
“MKURABITA kwa kushirikiana na Manispaa ya Singida  wanaanzisha  kituo kimoja cha Urasimishaji na uendeshaji biashara  katika Manispaa hii, ili kufanya mchakato mzima wa kufanya urasimishaji wa biashara kuwa wa haraka, rahisi na wa gharama nafuu kwa mfanyabiashara.” Alisisitiza Muragiri.
 Kituo hiki kitahudumia wafanyabiashara wote wa Wilaya ya Singida, Huduma zitakazotolewa katika Kituo hiki ni pamoja na kupata taarifa mbalimbali kuhusu uendeshaji wa biashara rasmi, kusajili biashara, upatikanaji wa leseni za biashara, taarifa za kodi, huduma za kibenki, huduma za kuanzisha na kuendesha viwanda, bima, mafao na mtandao wa masoko. 
Kwa upande wake ,  Kaimu Mkurugenzi wa Urasimishaji kutoka MKURABITA  Bw. Japhet Werema amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wajasiriamali hao kupata faida nyingi ikiwemo kuingia katika mfumo rasmi na hivyo kukuza mitaji yao na kupanua wigo wa kufanya biashara.
Alibainisha kuwa kutokana na mafunzo hayo wajasiriamali wamekuwa na mwamako wa kuanzisha makampuni na pia kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuanzisha viwanda katika maeneo yao akitolea mfano Mkoa wa Njombe ambao wajasiriamali wake wameshanufaika na mafunzo hayo na kuonesha mwamko wa kukuza biashara zao.
Akizungumzia  baadhi ya  Manispaa ambazo tayari zina vituo hivyo amesema kuwa ni pamoja na; Njombe, Bariadi, Morogoro na kwa sasa Manispaa ya Singida itakuwa na kituo kama hicho baada ya kukamilika kwa mafunzo kwa wajasiriamali wake.
Naye Meya wa Manispaa ya Singida  Alhaji Gwae Mbua amesema kuwa wametenga maeneo kwa ajili ya wajasiriamali wa Manispaa hiyo ili kuendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuwawezesha wajasiriamali.
Aliongeza kuwa maeneo yaliyotengwa yanakidhi mahitaji ya wajasiriamali wanaotaka kuanzisha biashara za aina mbalimbali kulingana na mahitaji yao.
Mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya 1000 yanafanyika Mjini Singida yakilenga kuwajengea uwezo ili waweze kurasimisha biashara zao na hivyo kukuza uchumi na kuchangia katika ujenzi wa Uchumi wa Taifa na pia kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwawezesha kukuza na kutoa mchango katika uchumi.

No comments: