ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 8, 2019

NAIBU WAZIRI MABULA AWAONYA WATENDAJI WA SEKTA YA ARDHI BIHARAMULO

 Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akikagua jalada la ardhi katika ofisi ya masijala ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera alipofanya ziara ya kushtukiza katika halmashauri hiyo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye halmashauri hizo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri Sospiter Mwishamba na kushoto ni Mpimaji Ardhi Vedastus Masige
 Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akimsikiliza Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera Novatus Babu alipofanya ziara ya kushtukiza katika halmashauri hiyo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye halmashauri hizo.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akiwasili Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera alipofanya ziara ya kushtukiza katika halamashauri hiyo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye halmashauri hizo.

Na Munir Shemweta, Biharamulo 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera kujipanga na kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza migogoro ya ardhi na wasipotekeleza majukumu yao vizuri atawawajibisha. 

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya Biharamulo katika ofisi za halmashauri hiyo mkoani Kagera,  Dk. Mabula alisema pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi katika halmashauri hiyo lakini watumishi wa sekta hiyo wanapaswa kujipanga na kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kupunguza migogoro ya ardhi na wakati huo kuwawezesha serikali kukusanya mapato kupitia sekta ya ardhi. 

"Kama kazi haziendi migogoro ya ardhi haiwezi kuisha na ninyi hapa mna viwanja vichache lakini mmeshindwa kuviingiza katika mfumo hivyo mkimaliza kuviingiza viwanja hivyo hapo mnaweza kurekebisha takwimu" alisema Dk Mabula. 

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaziangalia idara za ardhi katika halmashauri zao kwa kuwa hakuna miradi inayokamilika bila kuhusisha ardhi hivyo sekta hiyo ni muhimu na inapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. 

Ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kupitia idara ya ardhi kuhakikisha inatoa ilani za madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi mia tano katika kilindi cha wiki moja na kueleza kuwa watakaoshindwa kulipa basi wafikishwe katika mabaraza ya ardhi. Hata hivyo,  Dk Mabula ameshangazwa na halmashauri hiyo kushindwa kutoa hati za madai wakati ina wadaiwa wa kodi ya ardhi wapatao 2000. 

Akigeukia suala la utoaji hati za ardhi ,  Dk Mabula ameshangazwa na kasi ndogo ya utoaji hati ambapo katika kipindi cha ropo ya pili ya mwaka 2018/2019 idara hiyo imeweza kuandaa hati 31 kati ya 200 huku baadhi ya hati zikiwa katika ofisi ya  Kaimu Mkuu wa Idara ya ardhi tangu mwezi Novemba 2018 bila kusainiwa wakati hati zinaweza kutolewa ndani ya mwezi mmoja. 

Aidha, Dk Mabula ameitaka halmashauri ya Biharamulo kutambua mali zake na kuhakikisha maeneo yake yanakuwa na hati za ardhi sambamba na kulipa kodi ya pango la ardhi.  Kwa mujibu wa Dk Mabula maeneo mengi ya halmashauri yanekuwa na mgogoro kutokana na kukosa hati na wakati huo kushindwa kulipa kodi ya ardhi. 

Mapema Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi ambaye ni Afisa Ardhi Mteule  katika halmashauri ya wilaya ya Biharamulo Novatus Babu alimueleza Naibu Waziri Mabula kuwa halmashauri hiyo imepima jumla ya viwanja 3, 101 katika maeneo ya Biharamulo Mjini,  Nyakanazi,  Runazi,  Lusahunga na Nyakahura na jumla ya viwanja 2, 191 vimeingizwa katika mfumo huku viwanja 200 vikiwa havijaingizwa. 

Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu huyo wa Idara halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo katika kilindi cha robo ya pili 2018/2019 imeweza kukusanya kiasi cha shilingi 38, 022, 624 kati ya milioni 150 ilizopangiwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019. 

No comments: