ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, January 8, 2019

PTF YAPONGEZWA KWA KUTEKELEZA SERA YA UCHUMI WA VIWANDA

 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) wakati wa ziara ya kikazi alipowatembelea ofisini kwao jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kufahamu majukumu ya mfuko na kuhimiza uwajibikaji, ambapo pia alipata fursa ya kujionea wanufaika wa mikopo inayotolewa na mfuko huo.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akikabidhiwa nyaraka mbalimbali na Mkurugenzi wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) Bi. Haigath Kitala mara baada ya mkurugenzi huyo kuwasilisha taarifa ya utekelezaji  wakati wa ziara ya kikazi ya Dkt. Mwanjelwa katika ofisi za PTF jijini Dar es Salaam,  ziara ilikuwa na lengo la kufahamu majukumu ya mfuko na kuhimiza uwajibikaji.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akisikiliza maelezo ya Bi. Rose Kalulika kuhusu bidhaa zinazozalishwa  na kikundi cha akina mama cha UWAZI SHALOOM  wakati wa ziara ya  kikazi katika ofisi za PTF jijini Dar es Salaam,  ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanufaika hao wa mikopo inayotolewa na PTF.
 Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akishuhudia bidhaa zinazotengenezwa na  kikundi cha Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi  Tanzania (FUWAVITA), kikundi cha UWAZI  SHALOOM cha akina mama wasindikaji, Kikundi cha MAKINI FOOD SUPPLIES cha akina mama wasindikaji na kikundi cha MAB cha vijana  wakati wa ziara yake ya  kikazi katika ofisi za PTF jijini Dar es Salaam,  ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanufaika hao wa mikopo inayotolewa na PTF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwasisitiza watumishi wa PTF kutoa huduma nzuri  kwa walengwa wa mikopo inayotolewa  na PTF wakati wa ziara ya  kikazi katika ofisi za PTF jijini Dar es Salaam,  ambapo alipata fursa ya kuzungumza na wanufaika hao wa mikopo inayotolewa na PTF.

Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) umepongezwa kwa utekelezaji mzuri wa Sera ya Uchumi wa Viwanda inayohimizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa mikopo kwa makundi maalumu ya watu wenye ulemavu, akina mama na vijana wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati wa ziara ya kikazi ya kuwatembelea watumishi wa Mfuko wa Rais wa Kujitegemea  kwa lengo la kufahamu majukumu ya mfuko huo na kuhimiza uwajibikaji, ambapo alipata fursa ya kujionea wanufaika wa mikopo inayotolewa na mfuko huo.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa, makundi yaliyopatiwa mikopo ambayo ni kundi maalumu la walemavu la Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi Tanzania (FUWAVITA), kikundi cha UWAZI  SHALOOM cha akina mama wasindikaji, Kikundi cha MAKINI FOOD SUPPLIES cha akina mama wasindikaji na kikundi cha MAB cha vijana ni mfano mzuri wa kuigwa kwa kutekeleza sera ya Uchumi wa viwanda kwa vitendo kwani wanazalisha bidhaa zenye ubora ambazo ni mvinyo, viungo vya mchuzi, viungo vya chai, siagi ya karanga, mango pickle na mabeji ya wanafunzi wa shule za awali, za msingi na vyuo.

Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, PTF imejitofautisha na taasisi nyingine za kifedha kwani  inajali makundi maalumu yote kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu na yenye riba ndogo zaidi bila ubaguzi wowote.
Kwa upande wake, mwakilishi wa kikundi cha Furaha ya Wanawake Wajasiriamali Viziwi  Tanzania (FUWAVITA), Bi. Aneth Gerana amesema wanaishukuru PTF kwa kuwapatia mikopo kwani imekuwa ikiwanufaisha sana ikizingatiwa kwenye mabenki hawadhaminiki hivyo PTF imekuwa mkombozi kwao.
Bi. Gerana amesisitiza kuwa, kupitia mkopo wa fedha wa PTF wao kama walemavu wameweza kuuthibitishia umma kuwa, wanaweza kwa kuzalisha mvinyo wenye ubora na kuongeza kuwa wana hakika ya kuifikia ndoto ya kuwa na kiwanda cha mvinyo kikubwa Afrika ya Mashariki ili kuunga mkono kwa vitendo sera ya uchumi wa viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Bi. Gerana, ameiomba PTF kuwapatia mafunzo ya kompyuta wao kama kundi maalumu la walemavu ili mafunzo hayo yaweze kuwasaidia kutafuta masoko kwa njia ya mtandao,  ombi ambalo lilitiliwa mkazo na Mhe. Dkt. Mwanjelwa kwa kuitaka PTF kuwapatia mikopo ya vifaa itakayowawezesha kununua kompyuta zitakazowarahisishia  utafutaji wa masoko kwa njia ya mtandao. 
Naye, Mwakilishi wa kikundi cha MAB cha vijana wanaotengeneza mabegi, Bw. Amon Philemon amesema mkopo wa PTF umewawezesha kuwa wajasiriamali wa  kutengeneza mabegi ya wanafunzi wa kuanzia shule za awali hadi vyuo vya elimu ya juu.
Bw. Philemon ameainisha kuwa, katika mabegi wanayoyatengeneza wanaweka picha za wanafunzi husika, majina yao na logo,  lengo likiwa ni  kudhibiti wizi mashuleni na vyuoni, hivyo Dkt. Mwanjelwa amekipongeza kikundi hicho kwa ubunifu huo.
Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) ni Taasisi ya Kifedha inayotoa mikopo ya fedha na vifaa nchini kwa makundi ya akina mama wajasiriamali wazalishaji, kundi maalumu la watu wenye ulemavu na vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi lengwa kabla ya kutoa mikopo kwa wanufaika hao wa PTF. 

No comments: