ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 28, 2019

Rais Magufuli apokea ripoti ya utendaji kazi wa Takukuru

 Kamishna wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Diwani Athmani amesema taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa kiasi cha Sh70.3 bilioni ikilinganishwa na Sh14.6 zilizookolewa mwaka 2016/2017.
Mbali na fedha hizo, amesema taasisi hiyo pia imefungua kesi 495 za rushwa katika kipindi cha mwaka 2017/2018 ikilinganishwa na kesi 435 zilizofunguliwa mahakamani mwaka 2016/2017.

Kamishna Athmani amesema hayo wakati akiwasilisha kwa Rais John Magufuli ripoti ya utendaji kazi wa Takukuru leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika shughuli hiyo, Rais Magufuli pia amemuapisha Kamishna Valentino Longino kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Kamishna Athmani amesema rushwa ni tatizo ambalo halipaswi kufumbiwa macho kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa taifa na jamii.

“Palipo na rushwa hakuna amani, palipo na rushwa hakuna haki na palipo na rushwa hakuna maendeleo,” amesema kiongozi huyo wa Takukuru.
Amesema taasisi hiyo imekamilisha uchunguzi wa majalada 906, kati ya hayo 699 yalihusu hongo, huku mengine 208 yakihusu vipengere vingine vya sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Amesema wataendelea kutekeleza majukumu yao pasipo kumuonea wala kumpendelea mtu yeyote kwani si tu ni kinyume cha sheria bali pia ni dhambi.
Aidha, amewataka Watanzania kusoma alama za nyakati kwa sababu wakati uliopo sio salama tena kwa wala rushwa.

No comments: