ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 28, 2019

Lissu atumia mawakili kudai mshahara wake

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amemwandikia barua katibu wa Bunge, akimtaka kumlipa mshahara na posho zake za kuanzia Januari, ndani ya siku 14 vinginevyo atakimbilia mahakamani. Hata hivyo, katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ameliambia Mwananchi jana kuwa “barua sijaipata na wala sifahamu lolote.”

Lissu alieleza uamuzi huo baada ya kuulizwa na Mwananchi lililotaka kujua wito alioutoa Machi 14 kwa Spika na katibu wa Bunge akiwataka kumrejeshea stahiki zake kama umetekelezwa. Mbunge huyo amekuwa nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi katika makazi yake Area D mjini Dodoma. Mpaka sasa yupo nchini Ubelgiji akiendelea na matibabu.

Akielezea suala la barua yake kwenda kwa katibu wa Bunge, alisema, “mawakili wangu walimwandikia barua katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai ya kumtaka kulipa mshahara na posho zangu za kibunge za tangu Januari, 2019.” “Aidha, barua hiyo ilimtaka kutokuingilia au kuzuia tena malipo ya mshahara na posho hizo kwa namna nyingine yoyote.
“Mawakili wangu walimpa siku 14 kutekeleza madai, vinginevyo tutafungua madai Mahakama Kuu kudai haki yangu.”

Alisema barua hiyo iliyoandikwa Machi 18 na mawakili wa Chadema wakiongozwa na John Mallya ilitumwa kwa katibu wa Bunge kwa njia ya rejesta (EMS). “Bado tunasubiri majibu ya katibu wa Bunge na wakati huohuo mawakili wangu wanahesabu siku 14,” alisema Mallya alipoulizwa na Mwananchi alisema, “siku 14 hizo zinaanza kuhesabika tangu siku alipoipokea barua hiyo.”

Alisema waliituma kwa njia mbili, moja ikitumwa ofisi ndogo za Bunge Dar es Salaam kwa njia ya kitabu cha hati ya kupokea kwa kutia saini (dispatch) na nyingine kwa EMS.
“Hii ya dispatch imefika, lakini hii ya EMS leo jioni (jana) tutakutana katika kikao ambacho tutajua kama imefika au la.”

Akifafanua, Lissu alisema, “Bunge halina mamlaka yoyote ya kisheria kuzuia au kukata au kupunguza mshahara wa mbunge na posho zinazotokana na ubunge, isipokuwa tu kama mbunge husika amesimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa azimio la Bunge kutokana na kukiuka maadili ya kibunge.” “Na hilo haliwezi kufanyika bila kwanza Spika wa Bunge kuielekeza Kamati ya Maadili na Mamlaka ya Bunge kushughulikia suala hilo kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.”

Alisema ni lazima mbunge husika apatiwe wito wa maandishi kuhudhuria kikao cha kamati ya maadili ili aweze kujitetea. “Hakuna lolote kati ya masharti haya lililotekelezwa. amezuia mshahara na posho zangu kienyeji enyeji tu, kana kwamba ni mali yao binafsi. Haya ndio masuala tutakayoenda nayo Mahakama Kuu kuyaombea tamko la kisheria la Mahakama hiyo,” alisema.

Mwananchi lilipotaka kujua maendeleo ya afya yake baada ya kufanyiwa upasuaji wa 24 wa mwisho, Lissu alisema, “Kazi kubwa iliyobakia ni mazoezi ya kukunja goti la kulia na kunyoosha mkono wa kushoto. Naendelea vizuri na mazoezi hayo.”

MWANANCHI

No comments: