ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 28, 2019

Wapinzani wakutana Dar, Zitto atoa neno

Viongozi wa vyama vya upinzani jana Jumatano Machi 27, 2019 jioni walikutaka jijini Dar es Salaam, na baadaye kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alidokeza waliyojadili.
Kikao hicho kilifanyika saa chache baada ya polisi kuzuia mkutano wa ACT uliokuwa ufanyike ukumbi wa PR Temeke kwa kile kilichoelezwa kuwa wamepata taarifa kuwa kuna wanachama wa CUF ambao walitaka kufanya vurugu.
“Tumefanya kikao cha ndani, ni kikao cha kawaida cha vyama 10. Ni kikao cha mahusiano kuhusu masuala mbalimbali,” alisema Zitto.
“Kikao hiki ni cha mwendelezo wa kile ambacho vyama vilikutana kujadili muswada (wa Sheria ya Vyama vya Siasa) ambao sasa umesainiwa kuwa sheria.”
Baadhi ya viongozi walioshiriki mkutano huo ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, naibu katibu mkuu wa chama hicho, Salum Mwalimu; katibu mkuu, Dk Vicent Mashinji, Maalim Seif Sharif Hamad na Zitto.
“Ni kikao cha kawaida hatukuita wanahabari ni mwendelezo wa vikao vyetu vya kawaida,” amesema Zitto bila kuweka wazi masuala waliyoyajadili.

No comments: