ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 26, 2019

DKT. KALEMANI AWATAKA MAMENEJA AMBAO HAWAJAUNGANISHIA UMEME WANANCHI KUACHIA MADARAKA

 Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (mwenye shati la bluu), akizungumza na mafundi wanaounganisha umeme katika kijiji cha Osteti wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara, akiwa katika ziara ya kazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme wilayani humo, Aprili 25, 2019.
 Mafundi wakiunganisha umeme katika nyumba ya mmoja wa wakazi wa kijiji cha Osteti wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara. Taswira hii ilichukuliwa Aprili 25, mwaka huu wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kijijini humo kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati), akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani Kiteto, akiwa katika ziara ya kazi wilayani humo, Aprili 25, 2019 kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme na kuzungumza na wananchi.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kabla ya kuwasha rasmi umeme katika kijiji cha Dosidosi wilayani Kiteto, mkoani Manyara akiwa katika ziara ya kazi, Aprili 25, 2019.


Na Veronica Simba – Manyara
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ametoa karipio kwa mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao wamekaidi agizo alilolitoa kuhakikisha wanawaunganishia umeme wananchi waliolipia huduma hiyo kwa wakati na kuwataka wajisalimishe makao makuu ya Shirika hilo Mei 5 mwaka huu, wakiwa na barua za kuachia nyadhifa zao.

Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Dosidosi wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara, jana Aprili 25, akiwa katika ziara ya kazi, Waziri Kalemani alisema hawezi tena kutoa msamaha kwa mameneja ambao hawajawaunganishia umeme wateja kwa wakati kuanzia kipindi cha nyuma hadi kufikia mwezi uliopita (Machi).

“Siwezi kusamehe tena mameneja ambao hawajawaunganishia umeme wateja kwa muda mrefu. Hii ni kwa sababu wamesababisha kuleta kero kwa wateja, usumbufu pamoja na kupotezea mapato Shirika la Umeme,” alisisitiza Waziri.

Katika hatua nyingine, Waziri alikerwa na hali aliyoishuhudia katika kijiji cha Nchinira wilayani humo, ambapo nguzo za umeme zinaonekana kusimikwa kwa muda mrefu pasipo kutundikwa nyaya ili kuwaunganishia wananchi.

Kufuatia hali hiyo, Waziri Kalemani alilazimika kutoa onyo kali kwa mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini wilayani humo pamoja na kumtaka Meneja wa TANESCO wa Wilaya kuwasilisha maelezo makao makuu ya Wizara, Dodoma ni kwanini eneo hilo halijaunganishiwa umeme ilhali nguzo zilishasimikwa kitambo.

“Natoa onyo kwa Mkandarasi. Maeneo yote mliyosimika nguzo; sitaki kuona nguzo zimesimama bila kuwa na nyaya na bila kuwaunganishia umeme wananchi. Ni marufuku. Nguzo zikisimikwa, zitundikiwe nyaya na wananchi waunganishiwe umeme.”

Waziri alielekeza eneo hilo liwe limeunganishiwa umeme ifikapo wiki ijayo.

Aidha, akiwasha umeme katika shule ya sekondari iliyopo Kijiji cha Dodisdosi, Waziri Kalemani alitoa wito kwa walimu na viongozi mbalimbali wa ngazi za vijiji na mitaa nchi nzima, kulipia gharama za uunganishaji umeme ili Taasisi mbalimbali za Umma katika maeneo yao, hususani shule zipatiwe nishati hiyo muhimu.

Alisema siyo vema shule ikakamilika ujenzi na kuanza kutoa huduma kwa takribani miaka miwili au zaidi ikiwa haina umeme kwani inaweza kusababisha uduni wa maendeleo ya elimu katika shule husika.

“Uwepo wa umeme katika shule husaidia kuongeza hali ya ufaulu kwani pamoja na mambo mengine, kwa sababu walimu wataweza kufanya vizuri zaidi maandalizi yao ya kufundisha,” alifafanua.

Waziri aliwaeleza wananchi wa Kiteto kuwa vijiji vyote vya Wilaya hiyo pamoja na vitongoji vyake, ambavyo havijaunganishiwa umeme, vitapata nishati hiyo kwani viko katika orodha ya Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza ambao unatarajiwa kukamilika Juni mwakani.

Hata hivyo, alisema serikali imemuagiza Mkandarasi husika kuhakikisha anakamilisha kazi ya kuviunganishia vijiji vyote umeme kabla ya Septemba mwaka huu ili libaki zoezi la kuunganishia umeme wananchi ambalo nalo litatakiwa kukamilika ndani ya kipindi cha mkataba wake.

Katika ziara hiyo ya kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme wilayani Kiteto, Waziri Kalemani alifuatana na viongozi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Jimbo husika Emmanuel Papian, Kaimu Kamishna wa Nishati Juma mkobya, mameneja wa TANESCO wa Kanda na Wilaya pamoja na wataalamu mbalimbali kutoka wizarani na REA.

No comments: