ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, September 29, 2019

DKT. SALIM ATUNUKIWA NISHANI YA JUU YA URAFIKI YA JAMHURI YA WATU WA CHINA

Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mheshimiwa Xi Jinping, leo asubuhi tarehe 29 Septemba 2019 amemtunukia Waziri Mkuu Mstaafu Mheshimiwa. Dk. Salim Ahmed Salim, Nishani ya Juu ya Urafiki ya Jamhuri ya Watu wa China ikiwa ni sehemu ya matukio ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Jamhuri ya Watu wa China iliyofanyika jijini Beijing.  Mheshimiwa Dkt. Salim anakuwa mwafrika wa kwanza kupewa heshima na tuzo hiyo ya juu katika historia ya China.

Nishani hiyo ilipokelewa na Bi. Maryam Salim, Binti ya Dk. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia nchini Albania kwa niaba ya Baba yake kutokana na kushindwa kuhudhuria kwa sababu za kiafya. Katika tukio hilo, Serikali ya Tanzania iliwakilisha na Balozi wa Tanzania nchini China Mheshimiwa Mbelwa Kairuki.

Hafla hiyo kubwa ya kitaifa ya kukabidhi nishani ilihudhuriwa na viongozi waandamizi wa Chama na Serikali ya China akiwemo Makamu wa Rais Mheshimiwa Wang Qishan, Waziri Mkuu Mheshimiwa Li Keqiang, Spika wa Bunge Mheshimiwa Li Zhanshu na Wajumbe wote wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Baraza la Taifa.

Mbali na Dk.Salim,  wengine waliotunukiwa Nishani ya Urafiki ni pamoja na Kiongozi wa Chama cha Kikoministi cha Cuba Jenerali Raul Castro, Dada wa Mfalme wa Thailand Maha Chakri Sirindhorn, Kiongozi wa Jumuiya ya Urafiki ya China na Urusi Ndugu Galina Kulikova, Waziri Mkuu Mstaafu wa Ufaransa Jean-Pierre Raffarin na Bi  Isabel Crook  kutoka Canada.

Vilevile  Rais Xi alitoa Nishani  ya Jamhuri na Nishani ya Heshima ya Taifa kwa raia 36 wa China kwa kutambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa la China kupitia kazi zao katika fani mbalimbali.

Nishani ya Juu ya Urafiki ya Taifa la China imetolewa kwa Dkt. Salim  kutokana na mchango wake wa kuiwezesha Jamhuri ya Watu wa China kuwa Mwanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 1971 alipokuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa.  Aidha, mchango wa Dk. Salim katika kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania wakati aliposhikilia nyadhifa mbalimbali umetajwa kama sababu ya kutunukiwa Nishani hiyo. Vilevile, mchango wa Dk.Salim katika kujenga mahusiano kati ya China na Afrika akiwa na nafasi ya Katibu Mkuu wa OAU umetajwa kuwa sababu nyingine ya kutunukiwa Nishani.

Tukio la Kutoa Nishani limetangazwa moja kwa moja na Televisheni zote za Jamhuri ya Watu wa China na kushuhudiwa na watu zaidi ya Milioni 500.

Kwa mujibu wa maelezo ya Balozi wa Tanzania nchini China Ndugu Mbelwa Kairuki Kupitia tukio la leo, mamilioni ya Wachina hususan vijana wamepata fursa ya kufahamu nafasi na mchango wa Tanzania na Bara la Afrika katika historia ya taifa lao. Aidha, tukio la leo limeifanya Tanzania kufahamika kwa watu wengi zaidi nchini China kupitia tukio mara moja. Hatua hiyo itaamsha udadisi na hamasa miongoni mwa Wachina wengi wa kizazi kipya kutaka kuifahamu zaidi Tanzania. Hali hii yaweza kujitafsiri katika fursa kubwa ya kukua kwa utalii, biashara na wawekezaji ikizingatiwa kuwa  wananchi wa China hutoa mwitikio mkubwa kwa nchi ambazo husemwa vizuri na kuthaminiwa na Serikali yao.

Aidha Balozi Kairuki ameeleza kwamba maadhimisho ya miaka 70 ya Jamhuri ya Watu wa China mwaka huu yanaambatana na maadhimisho ya miaka 55 ya urafiki na udugu kati ya China na Tanzania kufuatia kuanzishwa kwa mahusiano rasmi ya kidiplomasia mwaka 1964. Uhusiano wa China na Tanzania uliotokana na uhusiano mzuri wa waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mao Tsetung. Uhusiano huo umeendelezwa na viongozi wa pande zote mbili ambao umekuwa ukiimarika siku hadi siku. Uhusiano huu umekwenda mbali zaidi ya uhusiano kati ya Serikali na Serikali na kushamiri kwa uhusiano wa watu kwa watu.

Ni kwasababu hiyo, katika maadhimisho ya miaka 70 ya Taifa la China, Jumuiya ya Urafiki wa watu wa China na Tanzania ni miongoni mwa Jumuiya za mataifa 17 yenye urafiki wa majira yote na China walioalikwa  kushiriki kwenye maadhimisho hayo na tarehe 1 Oktoba 2019 watakuwa na gwaride lao maalum. Katika jumuiya hizo 17, Kutoka Barani Afrika ni Tanzania na Zambia ndio watahudhuria.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Bi. Maryam Salim akiwa katika picha na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Xi Jinping na picha ya chini akiwa na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe. Mbelwa Kairuki mara baada ya kupokea nishani.

No comments: