ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 18, 2019

THIBATI YA MAABARA YA GST

Image result for THIBATI YA MAABARA YA GST
TAARIFA KWA UMMA

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) inapenda kuwajulisha wadau wake na Umma kwa ujumla kuwa maabara ya GST imepata ITHIBATI (ACCREDITATION) kutoka Shirika la Kimataifa linaloshughulika na utoaji wa Ithibati katika Maabara zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi zilizopo Kusini mwa Afrika (SADCAS). Ithibati hii imetolewa kwenye eneo la uchunguzi wa kemia katika sampuli za madini. (Scope: Chemical analysis to ISO/IEC 17025:2017-Minerals) na kupewa namba ya usajili ya kipekee TEST-5 0043.

Maabara ya GST imekuwa ya kwanza ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kupata Ithibati ya toleo jipya la Mwaka 2017 ambalo linatakiwa kufuatwa na maabara zote za uchunguzi (Testing laboratories). Aidha, upatikanaji wake ulitokana na tathimini iliyofanywa na wakaguzi kutoka SADCAS na kuidhinishwa na kikao cha Kamati Maalum ya Ithibati kilichofanyika tarehe 15 Octoba, 2019 jijini Gaborone, Botswana baada ya kukidhi vigezo vyote vya kitaalamu vinavyozingatiwa na shirika hilo la kimataifa.

Kupatikana kwa Ithibati hii ni sehemu ya mikakati ya Wizara ya Madini kupitia GST ya kuendelea kuboresha huduma za uchunguzi wa sampuli za miamba na madini. Maboresho haya yanalenga kuendelea kutoa majibu sahihi na ya uhakika kupitia wataalam wenye uzoefu mkubwa na mashine zenye viwango vya kimataifa.

Majibu ya uchunguzi wa maabara kutoka GST yanatambulika kimataifa, hivyo GST inawakaribisha wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa kuendelea kufanya uchunguzi wa sampuli za miamba na madini kupitia Maabara ya GST kwa ajili ya kuongeza tija kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Imetolewa tarehe 17 Oktoba, 2019 na:


KAIMU MTANDEJI MKUU

No comments: