Afisa Tarafa ya Itiso Remidius Emmanuel akizungumza wakati anafungua Semina Maalum kwa waandikishaji wa Wapiga kura katika Tarafa ya Itiso, Semina hiyo imefanyika Makao Makuu ya Tarafa hiyo.
Afisa TAKUKURU Wilaya ya Chamwino Bi.Idda Siriwa akitoa Elimu ya kupambana na Rushwa katika Semina maalum kwa waandikishaji wa wapiga kura katika Tarafa ya Itiso
Mmoja wa wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Wilaya, Raymond Mwachango akiwasilisha mada katika Semina maalum kwa waandikishaji wa wapiga kura katika Tarafa ya Itiso.
Baadhi ya waandikishaji wa wapiga kura katika Tarafa ya Itiso wakifuatilia semina hiyo iliyoandaliwa ili kuwaongezea ujuzi kwenye kazi yao
ZIKIWA zimesalia wiki chache kufika Uchaguzi wa serikali za mitaa, Afisa Tarafa Itiso Remidius Emmanuel amewataka waandikishaji wote wa wapiga kura katika Tarafa hiyo kuzingatia nidhamu,Weledi na Uzalendo kwa kipindi chote cha zoezi hilo linalotarajia kuanza rasmi tarehe Oktoba 8 hadi 14 Oktoba 2019.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Semina maalumu iliyolenga kutoa Elimu kwa waandikishaji wa wapiga kura tarafani Itiso na kufanyika makao makuu ya tarafa hiyo ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uchaguzi wa serikali za Mitaa kwa mwaka 2019.
Katika Ujumbe wake kwa waandikishaji hao Remidius amewataka kutambua dhamana kubwa waliyopewa katika kufanikisha zoezi hilo muhimu la kitaifa kupitia Tarafa ya Itiso.
"Ninasisitiza sana mzingatie yale yote mtakayoelekezwa katika jukumu hili zito, nina hakika hamtaniangusha, nina imani na uwezo wenu mkubwa,lakini haya yote yatawezekana ikiwa mtamtanguliza mungu pamoja na kufanya kazi hii kwa weledi,nidhamu na uaminifu mkubwa,"amesema Emmanuel
Hata hivyo, kiongozi huyo amewashukuru na kuwapongeza wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo ngazi ya vijiji,Kata na Wilaya kwa namna walivyojipanga vyema katika kufanikisha zoezi la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019.
"Kazi hii inahitaji sana uzalendo, ninatoa onyo kwa wale wote watakaojaribu kukwamisha zoezi hili, tunazo kanuni, miongozo muhimu pamoja na ratiba ya matukio yote ya uchaguzi, sisi tuhakikishe tunazingatia haya na sio kuwa sehemu ya kufifisha ufanisi wa shughuli za uchaguzi katika maeneo yetu,"
"Lazima mkumbuke kwamba kazi hii mnayoifanya ndio itakayowawezesha kutoa haki ya msingi kwa wananchi wetu kuwachagua viongozi wao katika ngazi za Vitongoji, Mitaa na Vijiji, kwa hiyo kazi mliyonayo ni muhimu katika maslahi mapana ya Taifa letu," ameongezea Emmanuel.
Kwa upande wake Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Wilaya ya Chamwino Idda Siriwa ametoa elimu ya kuzuia,kupambana na kutokomeza rushwa kwa waandikishaji hao pamoja na Wasimamizi wasaidizi ngazi ya vijiji na Kata na kuwasisitiza kutojihusisha kabisa na vitendo vya kutoa au kupokea rushwa.
Idda amesema ikiwa watabaini uwepo wa matukio hayo watoe taarifa kwa kupiga namba 113 kwa mitandao yote ya simu au kutuma Ujumbe mfupi au kubonyeza *113# kisha kubonyeza OK na kufuata maelekezo ambapo watapata maelezo na kutoa tuhuma au malalamiko husika.
Aidha Afisa huyo ametoa namba ya simu ya mkononi ya Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Chamwino kama njia ya ziada ya kufikisha malalamiko yoyote ya Rushwa kutoka Tarafa ya Itiso na Wilaya hiyo kwa ujumla.
Zoezi hilo la Elimu kwa Waandikishaji wa wapiga kura lilifanyika kwa mujibu wa ratiba ya matukio ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa iliyoelekeza Elimu hiyo kutolewa kwa wahusika kati ya tarehe 4-6 Oktoba,2019 na Msimamizi wa uchaguzi pamoja na wasaidizi wake ngazi ya Wilaya.
Baadhi ya Waandikishaji walioshiriki Semina hiyo wameahidi kuzingatia yote waliyojifunza na kwamba wanatambua uzito wa kazi hiyo waliyonayo kwa kipindi chote watakachoshiriki katika zoezi hilo na kuwa sehemu ya kufanikisha zoezi hilo la uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mwaka 2019 kupitia Tarafa ya Itiso.
No comments:
Post a Comment