ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 5, 2020

HAKI ZA WAFANYAKAZI WA NDANI

Image result for mfanyakazi wa ndani\
Na Zain Hamza

Ni watu huru, sio watumwa!

Sheria ya haki za wafanyakazi ya Marekani ya mwaka 1938, (Fair labor Standards Act) imetaja haki za wafanyakazi wa ndani. Haki hizo ni pamoja na mishahara, masaa ya kufanya kazi, bima na kodi.

Mfanyakazi wa ndani ni lazima alipwe mshahara usio chini ya kima chini kwa kila saa analokuwa kazini. Ikitokea amefanya kazi zaidi ya masaa 40 kwa wiki basi ni lazima alipwe ovataimu. Ni malipo ya mara moja na nusu ya mshahara wa kawaida.

Kwa wafanyakazi wanaoishi na kulala wanapofanya kazi, hawa hawalazimiki kulipwa ovataimu. Masaa wanayolala na kupumzika hayalipwi. Vilevile wanaruhusiwa kutoka nje ya nyumba kwenye wakati wao wa mapumziko. Lakini kwa masaa wanayofanya kazi ni lazima walipwe.

Sheria inamtaka kila anayeajiri mfanyakazi wa ndani kuripoti jina la mfanyakazi, umri wake, namba yake ya utambuliasho (SSN) kwa Tanzania ni kitambulisho cha taifa, anuani yake, masaa anayofanya kazi kila wiki, na mshahara wake. Rekodi hii pia ionyeshe muajiri anamchaji kiasi gani mfanyakazi wake kwa chakula na malazi. Na pia ionyeshe malipo ya ziada inapotokea mfanyakazi amefanya kazi masaa zaidi ya 40 kwa wiki. Rekodi hizi zinatakiwa kuhifadhiwa kwa muda usiopungua miaka mitatu.

Kuna baadhi ya majimbo yanataka muajiri amkatie bima mfanyakazi wa ndani hasa kwa kumlinda iwapo ataumia akiwa kazini. Kulingana na mshahara wa mfanyakazi, muajiri anaweza kuwajibika kukusanya kodi na kuiepeleka mamlaka ya kodi (IRS)

Sasa basi, kama upo Marekani unafanya kazi za ndani, zijue haki zako, usiendelee kudhulumiwa. Tamu zaidi ni kuwa ukimshtaki muajiri anaekudhulumu, una uwezekano wa kupata fidia ya mamilioni. Inategemea na utajiri wa muajiri wako na kesi yenyewe.

Kama upo Marekani unadhulumu waafrika wenzio, hasa wale wasio na vibali vya kufanya kazi Marekani (huwezi kumpata mzungu) lijue janga unalojitafutia. Haya ndio mambo Trump hayataki. Unaweza kwenda jela na baadae kurudishwa kwenu. Na sio vigumu sana kukamatwa. Mfanyakazi wako akiugua, akifariki, akipata tatizo lolote la kiserikali au polisi, akikushtaki au akipata watu wa kumfundisha kukushtaki, vyovyote itakavyokuwa ukikamatwa ujue hii ni kesi.

Kwa Tanzania sijui sheria imekaaje. Ni vyema wahusika wakaliangalia hili jambo kwa makini. Kuna wabunge, wakuu wa mikoa, mameya, mabalozi, ili mradi vyeo vingi. Watu wanapiga sana siasa wanasahau kero halisi za jamii. Na ukifuatilia hao hao viongozi na vibosile ndio wana mahousigeli sita sita. Watoto wanatolewa vijijini wakiwa umri wa kwenda shule halafu wanapelekwa mijini kufanyishwa kazi. Watoto wanateswa, wananyonywa kiuchumi, wengine wanabakwa na hawana msaada wowote. Sharti moja la kuwa mfanyakazi wa ndani ni kutimiza umri halali unaouruhusiwa kwa mtu kufanya kazi.

Sasa hivi Tanzania kuna kitambulisho cha taifa, ni wakati muafaka kwa wizara ya kazi kufuatilia wafanyakazi wote ili kuhakikisha wanatendewa haki. Hii ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa ndani.

Ni sheria hizi ngumu ndio zinazoleta maendeleo kwa wenzetu. Watu wakikosa wa kuwatuma kazi ambazo hawawezi kuzifanya au hawana muda wa kuzifanya ndio wanagundua mashine. Kuna za kufulia, za kuoshea vyombo, za kufagilia na kadhalika. Kuna mpaka mafagio ya umeme yanayofagia yenyewe. Upo kazini unalituma linafagia sakafu yote na likimaliza linajizima. Sio ujanja kuwa na mahousigeli wengi usiowalipa kihalali. Huna tofauti yeyote na mtemi wa kikonongo aliyekuwa na watumwa mwaka 1887. Kwa wenzetu mfanyakazi wa ndani anamudu kuwa na nyumba yake mwenyewe na familia yake.

Kazi gani tena nyingine wanafanya mahousigeli? Kupika! Uvivu wa kupika na kukosa muda wa kupika ni chachu ya maendeleo kwa wenzetu. Ajira nyingi hupatikana kwenye mahoteli, mikahawa na watu wanaopeleka vyakula majumbani kwa watu. Hata UBER wameanzisha huduma ya kupelekea watu vyakula majumbani kwao.

Kazi za bustani na kukata majani ambazo hufanywa na watumishi, kwa wenzetu ni biashara kubwa zinazofanywa na makampuni (landscaping).

Kulea watoto pia ni eneo jingine linalotoa ajira kwa wenzetu. Kinamama wenye watoto wakienda kazini huacha watoto wao kwenye vituo vya kulea watoto (day care). Huko huwafanya watoto waanze shule mapema. Kwa Tanzania watoto huanza shule na miaka saba. Mtoto wa kimarekani wa miaka saba alishajua kusoma na kuandika siku nyingi sana. Ukizubaa anasoma text zako. Ukiuliza jiji la Dar lina day care ngapi inaweza kuwa mtihani. Uliza lina mahousigeli wangapi.

Ni vitu vya namna hii ndio vinavyotofautisha nchi zilizoendelea na nchi zinazojiita changa ingawaje kiumri zimezeeka.

No comments: