Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni, akiongea na wakimbizi walioko katika Kambi ya Nduta mkoani Kigoma, ambapo amewahamiza kuendelea kujiandikisha katika orodha ya wanaotaka kurejea nchini Burundi.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu,KigomaSerikali ya Tanzania na Burundi zimewahakikishia kurejea kwa amani na utulivu katika nchi zao wakimbizi na waomba hifadhi walioko katika makambi mbalimbali nchini huku serikali ya Tanzania ikiweka wazi haijalazimisha zoezi la urejeaji makwao kwa wakimbizi hao.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa ziara yake katika kambi ya Nduta iliyoko wilayani Kibondo mkoani Kigoma ikiwa na ukubwa wa kilometa za mraba 36 na ikihifadhi wakimbizi 62,127,waomba hifadhi 11,841 huku wenye hadhi nyingine wakifikia 1,168.
“Novemba 29, mwaka jana pande tatu ikiwemo Serikali ya Tanzania,Serikali ya Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) walishawekeana saini mkataba wa urejeshwaji wa wakimbizi wanaotaka kurejea kwao kwa hiari yao wenyewe,pande hizo zilikaa vikao kadhaa ikiwemo kutembelea nchi husika na walijiridhisha kurejea kwa amani na utulivu kabla ya kusaini mkataba huo,nawasihi sasa mjitahidi kujiandikisha ili muweze kwenda kuijenga nchi yenu,Burundi inawahitaji zaidi” alisema Masauni
“Amani imerejea katika maeneo yenu na sasa hivi ni kipindi cha uchaguzi jiandikisheni ili muweze kurejea kwenye nchi yenu muende mkatumie haki yenu ya kidemokrasia ya kuchagua viongozi.
Awali akisoma taarifa ya urejeaji wa hiari wa wakimbizi na waomba hifadhi,Mratibu wa Wakimbizi Kanda ya Kigoma,Athman Igwe alisema suluhisho la kudumu la wakimbizi ni kuwarejesha katika nchi ya asili kwa hiari,kuwahamishia nchi ya tatu na kupewa uraia katika nchi ya kimbilio huku akiweka wazi idadi ya waliorejea na walioomba kurejea.
“Mheshimiwa Naibu Waziri idadi ya wakimbizi na waomba hifadhi waliorejea tangu kuanza kwa zoezi hilo mwaka 2017 ni familia 27,459 zenye watu 80,072 huku kwa mwaka huu jumla ya familia 715 zenye wakimbizi 1,247 wakirejea kwao na sasa tuna maombi ya familia 31,723 zenye jumla ya wakimbizi 93,503 walioomba kurejea lakini tuna familia 3,163 zenye wakimbizi 10,883 wamebadilisha nia ya kurejea nchini kwao” alisema Mratibu Igwe
“Lakini katika mpango wa kuwahamishia wakimbizi nchi ya tatu kupitia Shirika IOM,Mei 2007 hadi kufikia Februari mwaka huu jumla ya wakimbizi 36,127 walihamishiwa nchi ya tatu na hivi karibuni tayari wakimbizi 200 walienda nchi za Marekani na Australia.
Akizungumzia suala la wahamiaji haramu katika kambi za wakimbizi Mratibu wa Kanda ya Kigoma,Athman Igwe, alisema jumla ya wahamiaji haramu 1,094 walichukuliwa hatua huku hali ya ulinzi na usalama ikiimarika na kuripotiwa kutokuwepo kwa tukio lolote ambalo lingeashiria usalama wa makambi yote katika mkoa wa Kigoma ambao kwa ujumla wake unahifadhi jumla ya wakimbizi 266,482.
Ni takribani miezi kadhaa sasa imepita tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. John Magufuli kwenye ziara yake katika mkoa wa Katavi kuagiza pande zote zinahusika na wakimbizi wakutane ili kuweza kujadili suala la warundi wanaojiandikisha kwa hiari kurudi nchini kwao,akiwaambia umefika wakati sasa wakurudi katika nchi zao kwenda kuzijenga huku akiwaonya wakimbizi wanaoshiriki katika matukio ya uhalifu hapa nchini.
No comments:
Post a Comment