Tuesday, April 14, 2020

Epuka sana majaribio penzini, ni hatari!


MUNGU ni mwema sana. Kwa Wakristo na wasiokuwa Wakristo wanaendelea kusherehekea Sikukuu ya Kufufuka Yesu Kristo. Ni vizuri watu wote mkaisherehekea siku hii kwa amani na upendo. Wakati Yesu Kristo anawaaga wanafunzi wake saa chache kabla kuteswa, kufa na kufufuka, aliwapa amri kuu ya upendo, Yohana: 15:7-9.

“Kama vile Baba alivyonipenda, ndivyo nimewapenda ninyi; kaeni katika upendo wangu. Mkishika amri zangu, mtakaa katika upendo wangu, kama vile ambavyo nimeshika amri za Baba na kukaa katika upendo wake. “Nimewaambia mambo haya ili shangwe yangu iwe ndani yenu na shangwe yenu ijae. Hii ndiyo amri yangu, kwamba mpendane kama vile nilivyowapenda.”

Ni vizuri tukaishi katika pendo la kweli. Tukaacha kudanganyana. Kwa wapendanao, kufufuka kwa Yesu Kristo kuwe mwanzo mpya wa kutafakari safari yenu. Mmetoka wapi? Mnaenda wapi, kikwazo chenu hasa ni nini katika kufikia hatua ya ndoa?

Kama mmeshafunga ndoa, mnaiboreshaje ndoa yenu iwe mpya na yenye furaha zaidi. Mnaishi katika mapenzi ya Mwenyezi Mungu? Hii ni changamoto ninawapa na kila mmoja wetu anapaswa kujitafakari na kuchukua hatua ili kuboresha uhusiano wake.

Msiishi kwa mazoea, badilikeni ili muweze kuyaelekea mafanikio maishani mwenu. Hata Wayahudi, kabla ya kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo walikuwa na Pasaka yao, lakini mara baada ya Yesu kuja, alipokufa na kufufuka aliiacha Pasaka mpya ambayo mpaka sasa Wakristo wanaisherehekea.

Kama mada inavyojieleza hapo juu, kuna baadhi ya watu wao miaka yote wapo kwenye majaribio tu ya mapenzi. Hawataki kuamua. Wao siku zote macho yao hayakubaliani na yanachokiona. Huku anataka na kule anataka.

Watu wa aina hii ni wale wasiokuwa na msimamo. Ndiyo maana wao kila siku wanajaribujaribu tu. Hawaridhiki. Mtu anamuangalia huyu, anamtoa kasoro anatafuta mwingine anaona naye ana tatizo, basi yeye anakuwa mtu wa kujaribujaribu tu.

Ndugu zangu, madhara ya kujaribujaribu haya ni mengi ikiwemo suala la kupoteza muda. Ni vizuri sana ukauheshimu muda kwa kuwa na msimamo kwenye maisha yako. Uangalie mahali, pachunguze na ukiona ni salama, basi kuwa na msimamo.

Hakuna mwanadamu aliye mkamilifu. Maisha ya uhusiano ni kusaidiana. Kufanyana bora kila siku. Mwenzako anakujenga na wewe wakati huohuo unamjenga. Mwisho wa siku wote wawili mnakuwa bora.

Ukiwa mtu wa kuyumbayumba, utajipotezea muda hata wa kufanya mambo ya kimaendeleo. Maendeleo mazuri yana maana zaidi pale utakapokuwa na mke au mume wako pamoja na watoto. Unapochelewa, unajichelewesha pia kuitengeneza familia bora.

Ukishaona upo mahali sahihi, acha kuyumbayumba. Acha kutangatanga, tulia. Huna sababu ya kufanya majaribio mara kwa huyu, mara kwa yule. Kuna baadhi ya udhaifu wa mwenzako unatakiwa kuubeba ili maisha yaende.

Mheshimu uliye naye, tengenezeni maisha yenu. Ninyi ndiyo mnaweza kufika pale mnapotaka kufika kwenye maisha yenu. Wekeni mipango, angalieni njia za kupita, hakika mkifanya kwa moyo na bidii na mkimtanguliza Mungu, mtafanikiwa. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri. Unaweza kunifuata kwenye kurasa zangu za mitandao ya kijamii; Instagram na Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale

GPL

No comments: