ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 9, 2020

Klabu zachekelea ofa ya Fifa

By Oliver Albert
UAMUZI wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuruhusu wachezaji ambao mikataba yao imeisha ama iliyopo ukingoni wakati huu ligi zikiwa zimesimamishwa kupisha janga ja virusi vya corona, kuruhusiwa kuzitumikia klabu zao hadi misimu itakapomalizika imepokelewa kwa furaha.
Viongozi mbalimbali wa klabu nchini hasa zilizopo Ligi Kuu Bara wamedai wamefurahishwa na maamuzi hayo kwani awali walikuwa na presha kubwa, kwa vile baadhi ya mikataba na wachezaji wao ilikuwa ikiwaacha njia panda kama wataendelea kuwatumia ama la, ila kwa sasa kwao freshi.
Fifa ilitoa agizo hilo kwa nchi wanachama kwa nia ya kuziepushia klabu hasara ya kukimbiwa na wachezaji wao wakati ligi mbalimbali zikiwa hazijamaliza msimu na nyingine zikitajwa huenda zikasogezwa mpaka Juni ama Julai kulingana na tishio la corona litakavyokuwa limepoa.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kupitia Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidao alikiri wameyapata maagizo hayo na watayasimamia kwa ukamilifu mpaka pale msimu wa 2019-2020 utakapomalizika.
Katibu wa Prisons, Ajabu Kifukwe amesema uamuzi huo utawasaidia pande zote mbili, viongozi wa klabu na wachezaji wenyewe.
"Unajua wakati mwingine inahitajika busara tu, kwani mchezaji anaweza akawa anamaliza mkataba kabla ya msimu kumalizika na akasaini timu nyingine, lakini kule hawezi kwenda kucheza mpaka msimu umalizike," amesema na kuongeza;
"Hivyo uamuzi huu ni mzuri kwani kwanza utalinda kiwango cha mchezaji kuliko akakae benchi huko alikosaini kabla ya msimu kumalizika, hivyo ni bora aendelee kucheza timu yake ya zamani hadi mwisho wa msimu ndipo aondoke kwa amani pia kwa upande wa klabu itapunguza presha ya usajili."
Naye Katibu wa Namungo Fc, Ally Selemani alisema wamepokea vizuri uamuzi huo kwani jambo hilo tayari lilishaanza kuleta shida wakati huu ligi ikiwa imesimama.
Klabu ambayo imechekelea zaidi maamuzi hayo ya FIFA ni Ndanda, ambayo kupitia viongozi wake walidokeza asilimia 70 ya wachezaji wao walikuwa wameshamaliza mikataba nao, kitu ambacho kama kusingetolewa 'ofa' hiyo ingeweza kuwaumiza wakimalizia mechi zao zilizosalia.
Viongozi wa Simba na Yanga ambao walikuwa na presha ya kuwakosa baadhi ya nyota wao waliobakisha mikataba na bado hawajasainishwa upya kama Papy Tshishimbi, Deo Kanda, Mzamiru Yasin, Shiza Kichuya, Tariq Seif kwa sasa ni kama wanapumua kwa agizo hilo la FIFA.

No comments: