Dar es Salaam. Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema hivi sasa tumetoka katika maambukizi ya mlipuko wa ugonjwa virusi ya corona yanayoletwa kutoka nje na imeingia kwenye maambukizi ya ndani kwa ndani.
Ummy ameeleza hayo leo Alhamisi Aprili 9, 2020 wakati akifungua mkutano wa viongozi wa madhehebu ya dini ulioandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision uliolenga kuelimisha jamii dhidi ya ugonjwa corona.
Amesema hadi sasa kuna idadi ya wagonjwa 25 na taarifa nyingine ataitoa mchana baada ya kupata maelezo watalaamu waliopo maabara.
"Ugonjwa tumeletewa kutoka nje, hivi sasa takwimu za jana, juzi na wiki iliyopita tumeanza kuambukizana wenyewe kwa wenyewe. Ili viongozi wangu wa dini naomba niliweke wazi its no longer imported cases, tumeanza local transmission.
"Ndani ya siku chache tutaingia katika community transmission. Maana yake tutapata mgonjwa ambaye hajui ugonjwa ameupata wapi? Sasa hivi amekuja mtu anamuambikiza fulani ndio maana tunafanya contact (muingiliano) kujua.
Amefafanua kuwa hatua ya maambukizi katika jamii ni ngumu aliyeambukizwa amepewa na nani na kwamba ndani ya siku chache inawezekana tukaingia katika hatua hiyo.
"Lazima niwaambia ukweli nisiwafiche soon (karibuni), tutaingia kwenye community transmission. Bado tunatakiwa kuchukua tahadhari na kuongeza juhudi za kukabiliana na ugonjwa huu," amesema Ummy.
Waziri huyo amesema ni wajibu wa kila kiongozi wa dini kuhakikisha wanaendesha ibada katika utaratibu na mazingira yasiyo hatarishi ili kujikinga dhidi ya virusi vya corona, akisema makongamano ya dini sio muhimu kwa wakati huu.
"Nimpongeza mkuu wa mkoa wa Pwani (Everist Ndikilo) kwa kuzuia kongamano la dini lililopangwa kufanywa na madhehebu ya kidini na kuhusishwa watu 3,000 wanaotoka nchi nzima," amesema Ummy.
Ummy amewataka viongozi hao wa madhehebu ya dini kuendelea kufanya ibada katika mazingira ya usalama kati yao na waumini sambamba na kuwahamasisha waumini kuepukana na vitendo vya kushikana na kukumbatiana.
"Tunaomba pia ibada ifanyike muda mfupi, pia wekeni utaratibu wa kupunguza msongamano wa waumini wakati wa kuingia na kutoka katika nyumba za ibada," amesema Ummy.
Awali mkurugenzi wa World Vision Tanzania, Gilbert Kamanga amesema shirika hilo lipo bega kwa bega kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa virusi vya corona.
Amewataka viongozi wa dini kutoa ujumbe sahihi kuhusu corona akisema ni miongoni mwa watu wanaoaminika katika jamii pamoja na kufuata yale yanayoelekezwa na Serikali kuhusu ugonjwa huo.
"Tushikane mkono pamoja tupambane na ugonjwa huu wa corona. World Vision ipo tayari kushirikiana na Serikali katika mapambano haya na kuweka mikakati," amesema Kamanga.
No comments:
Post a Comment