ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 26, 2020

Salamba mambo yamekwama Kuwait

By OLIPA ASSA

KILIO cha straika wa zamani wa Lipuli na Simba, Adam Salamba cha kutaka kurejea Tanzania katika kipindi hiki cha janga la corona, kilianza kuonyesha dalili nzuri kwa uongozi wa klabu yake ya Al Jahra ya Kuwait kumruhusu kutimka, lakini kuzuiwa kutua kwa ndege nchini kumemtibulia.

Mabosi wa klabu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza ya Kuwait ilikaa na wachezaji wote wa kigeni na kuwaruhusu kuondoka kipindi hiki Ligi ikiwa imesimama kutokana na janga la corona na Salamba akawa na matumaini makubwa ya kurejea Tanzania, lakini mambo yamekwama.

Awali, Salamba aliiambia Mwanaspoti, wachezaji saba wa kigeni waliitwa na viongozi na kuambiwa watarejeshwa katika nchi zao kwa kuwa hawajui mwisho wa janga hili ni lini.

Alidokeza tayari wachezaji kutoka Japan wamesharudishwa kwao kwa kutumia ndege za serikali, hivyo anasubiri ya namna yeye atakavyosaidiwa kurejea Tanzania, lakini wakati akifuatilia ubalozi wa Tanzania nchini humo ili kujua anaondokaje akakutaka na kikwazo kilichomtuliza.

“Tumebakia wachezaji kama watatu akiwamo Mnigeria na Mcameroon, ngoja tuone nasi tutasaidiwaje ili turejee nyumbani kwetu, hapo angalau nitapumua nitakapoikanyanga ardhi ya Tanzania,” alisema juzi wakati akieleza furaha yake ya kutaka kurejea nyumbani.

Hata hivyo, jana ndoto ya kurejea nyumbani kwa straika huyo chipukizi imeyeyuka kama mshumaa, baada ya kufahamishwa ndege zote za kutoka nje ya nchi haziruhusu kutua Tanzania.

Salamba aliliambia Mwanaspoti kuwa haelewi afanye nini kutokana na kufahamishwa kuwa ndege zote za kutoka nje zimepigwa marufuku kutua nchini kwa sababu ya virusi vya corona.

Alisema hana amani na amejawa hofu baada ya wenzake kutoka nchi nyingine kuondoka naye kuendelea kubaki nchini humo akiomba Mungu janga hilo lipite.

Alisema baada ya kuruhusiwa alimpigia simu Balozi wa Tanzania nchini Kuwait kumuuliza kama inawezekana kurudi Tanzania na kudai alijibiwa ndege haziruhusiwi kuingia nchini.

“Yaani sijui hata nifanyaje, ili niweze kurejea nyumbani kwani wenzetu wa nchi nyingine walishaondoka, hivyo najiona mkiwa kushinda ndani peke yangu,” alisema straika huyo aliyeifungia mabao 10 Lipuli msimu wa 2017-2018 na kusajiliwa Msimbazi alikodumu msimu mmoja kabla ya msimu huu kutimkia Umangani.

Kuhusu mshahara, Salamba amethibitisha wanaendelea kulipwa kama kawaida na wataendelea kulipwa bila kukatwa na hata senti, ila shida yake ni kubaki mpweke wakati wenzake wameondoka kurejea makwao.

“Kwa upande wa mshahara hatujayumbishwa, tutaendelea kuwekewa kama kawaida, ila shida ni hofu niliyonayo juu ya upweke,” amesema Salamba aliyekuwa gumzo Mei mwaka jana baada ya kumuomba kiatu nyota wa Sevilla, Ever Banega, timu hiyo ya Hispania ilipokuwa kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na kushinda kwa mabao 5-4 dhidi ya Simba.

“Ugonjwa huu umeleta changamoto ya aina yake kwa sababu kila jambo limesimama, watu wanapigania usalama wa afya zao,” alisema.

Awali, Salamba alikuwa akilalama anajisikia uchungu kuwa maili nyingi mbali na nyumbani wakati janga la corona likishika kasi na kufyeka roho za maelfu ya watu duniani kote.

Rekodi zinaonyesha kwa Kuwait mpaka jana mchana taifa hilo lilikuwa na visa 2,614 za walioambukizwa virusi cha corona, huku kukiwa na vifo vya watu watano na wengine 613 wakipona kutokana ugonjwa huo uliogundulika mwishoni mwa mwaka jana mjini Wuhan, China.

No comments: