ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 26, 2020

Corona inavyowaweka Waafrika njiapanda

MWANDISHI WETU

WAKATI benki ya dunia ikitahadharisha juu ya uchumi wa bara la Afrika,Kusini mwa jangwa la Sahara kuporomoka kwa kiwango ambacho hakijashuhudiwa tangu miaka 25 iliyopita,kutokana na virusi vya Corona, bara hilo pia limeonywa vifo vya malaria kuongezeka mara mbili zaidi.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema idadi ya vifo vinavyosababishwa na Malaria katika nchi za Afrika zilizoko kusini mwa jangwa la Sahara inaweza kuongezeka hadi kufikia 769,000 mwaka huu, iwapo nguvu zote zitaelekezwa katika mapambano ya virusi vya corona (COVID-19).

Inaelezwa kuwa Afrika inaweza kujikuta njiapanda zaidi kupambana na magonjwa mengine kutokana na kuelemewa na kasi ya maambukizi ya virusi vya corona ambapo hadi sasa imethibitisha kesi zaidi ya 25,000 za virusi hivyo huku vifo vikipindukia 1200.

Kwa sasa serikali kwa kushirikiana na WHO, zimejielekeza zaidi kwenye kupambana na janga la corona.

Mkurugenzi Mkaazi kanda ya Afrika Dk. Matshidiso Moeti mapema wiki hii alitoa wito kwa nchi zote za kiafrika kuhakikisha kwamba juhudi za kupambana na Malaria zinaendelea.

“Uchambuzi wa hivi karibuni ulibaini kwamba vyandarua vilivyowekwa dawa vimeachwa kusambazwa na udhibiti wa kesi umepungua, vifo vya malaria katika nchi za Afrika kusini mwa Sahara vinaweza kuongezeka mara mbili ukilinganisha na mwaka 2018”, amesema Moeti.

“Hii itakuwa idadi kubwa ya vifo kuwahi kushuhudiwa katika ukanda huo tangu mwaka 2000”, ameongeza mkurugenzi huyo.

Pia aligusia juu ya takwimu za mripuko wa kirusi cha Ebola barani Afrika, na kuonyesha kwamba watu walikufa kutokana na maradhi mengine, ikiwemo malaria, kuliko hata Ebola yenyewe, kutokana na ukosefu wa upatikanaji matibabu.

Mwaka 2018, kulikuwa na visa milioni 213 vya malaria na vifo 360,000 vinavyohusiana na ugonjwa huo katika kanda ya Afrika, ikiwa ni asilimia 90 ya kesi zote duniani.

WHO imesema kama lengo la kupunguza kasi ya kuenea kwa virusi vya corona itachangia kupungua kwa upatikanaji wa dawa za kupambana na malaria, vifo vitaongezeka mara mbili.

“Nchi katika ukanda mzima zina nafasi ndogo na fursa ya kupunguza uingiliaji katika udhibiti wa malaria, matibabu na kuokoa maisha katika kipindi hiki cha mripuko wa COVID-19”, ilisema taarifa ya WHO.

Benin, Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, Sierra Leone na Chad zote zilianzisha programu za kupambana na malaria kipindi hiki cha mripuko wa corona.

WHO inasema nchi hizo zinapaswa kuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika.

UCHUMI NA CORONA

Wakati corona ikitishia mapambano ya magonjwa mengine pia inatishia hali ya uchumi.

Mripuko wa virusi hivyo unaozidi kusambaa na utabiri wa benki ya dunia ni kwamba unatarajiwa kuzisukuma nchi za

Afrika, Kusini mwa Jangwa la sahara katika mporomoko wa kiuchumi katika mwaka huu wa 2020 kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25.

Ripoti ya benki ya dunia kuhusu hali ya kiuchumi barani Afrika imesema kwamba uchumi wa bara hilo utashuka asilimia 2.1 na kufikia asilimia 5.1 kutoka kiwango cha ukuaji cha mwaka jana cha asilimia 2.4.

Aidha mripuko huu wa virusi vya Corona utazigharimu nchi za ukanda wa kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika dola bilioni 37 hadi dola bilioni 79 ambayo ni hasara itakayoonekana mwaka huu kufuatia kuvurugwa kwa shughuli nyingi za kibiashara na kiuchumi miongoni mwa sababu nyinginezo.

Makamu mwenyekiti wa benki ya dunia kwa upande wa Afrika, Hafez Ghanem amesema janga la ugonjwa wa Covid-19 linapima uwezo wa mwisho wa jamii na nchi zote ulimwenguni na kuna uwezekano hususani kwa nchi za Afrika kuathirika zaidi.

Benki ya dunia na shirika la fedha la kimataifa IMF zinakwenda mbio kutoa fedha za dharura kwa nchi za Afrika na nyinginezo kukabiliana na virusi vya Corona ili kupunguza athari zitakazosababishwa na hatua za kufungwa kwa shughuli za kimaisha zinazochukuliwa nchi mbali mbali ulimwenguni kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo vya Corona.

Ikumbukwe kwamba janga la virusi vya Corona limesababisha kufutwa kwa safari za kimataifa katika nchi nyingi za bara hilo la Afrika hali ambayo

imeathiri kwa kiwango kikubwa sana sekta mbali mbali kama vile sekta ya utalii, uwekezaji na biashara.

Serikali mbali mbali za bara la Afrika zimetangaza hatua ya kufunga miji au nchi kwa maana ya kwamba hakuna shughuli za kawaida za kimaisha haziruhusiwi tena kufanyika au baadhi ya nchi zimetangaza kuzuia watu kutoka nje, na zile ambazo zimeruhusu raia wake wamekuwa waoga na hata wengine kulazimika kufunga biashara zao.

Kwa mujibu wa WHO licha ya virusi hivyo kuchelewa kuingia barani Afrika sasa inaonekana kuanza kusambaa kwa kasi.

Kutokana na hali hiyo benki ya dunia inasema ukuaji wa pato la ndani utapungua kwa kiwango kikubwa na hasa katika nchi tatu zenye uchumi mkubwa katika bara la Afrika ambazo ni Nigeria,Angola na Afrika Kusini.

Kadhalika nchi zinazouza mafuta pia zitaathirika sana.

MAREKANI TOFAUTI NA AFRIKA


Wakati Afrika ikisubiri ahueni na misaada, Marekani taifa tajiri imechukua hatua ya kupunguza makali yaliyosababishwa na virusi vya corona.

Ikiwa inaongoza kwa maambukizi ya virusi vya corona duniani huku raia wake wakipoteza ajira kwa kiwango kikubwa imeamua kuidhinisha karibu dola nusu bilioni katika mpango mpya wa kuuokoa uchumi.

Wakati ulimwengu ukipambana na kutafuta mbinu za kuuokoa uchumi unaoathirika kwa janga la virusi vya corona Baraza la Wawakilishi Marekani limepitisha mswada mpya wa kichocheo cha uchumi wa dola bilioni 483.

Hatua hiyo imekuja wakati kiwango cha ukosefu wa ajira kutokana virusi vya corona kikipanda na kampuni zikihitaji msaada zaidi.

Muswada huo tayari ulikuwa umeidhinishwa na Baraza la Seneti, na Rais Donald Trump ameashiria kuubariki haraka iwezekanavyo kuwa sheria.

Mpango huo unaongeza kwa ule wa dola trilioni 2.2 ulioidhinishwa mwishoni mwa Machi mwaka huu.

Karibu watu 50,000 wamefariki dunia Marekani kutokana na virusi vya corona, huku idadi ya walioambukizwa ikifikia zaidi ya 866,646.

Spika wa bunge Nancy Pelosi amesema mpango huo ni muhimu kwa kuzilinda familia za Marekani na kuhakikisha kuwa kampuni ndogo ndogo zina rasilimali zinazohitaji.

“Dola bilioni 60 zitatengwa kwa ajili ya wanawake na jamii za walio wachache, maveterani, wamarekani asili, wanaoishi vijijini na watu ambao hawakuwa na fedha kwenye benki lakini wana mahitaji makubwa ya mikopo.

“Bilioni 60 nyingine ni mikopo na ruzuku kwa biashara ndogondogo. Na kisha dola bilioni 100 kwa mahospitali na upimaji.” Unaeleza muswada huo

Bara la Ulaya, ambalo ndilo lililoathirika zaidi na vifo 110,000, viongozi wa Umoja wa Ulaya waliipa Halmashauri Kuu ya umoja huo jukumu la kutayarisha mpango wa kuufufua uchumi kwa ajili ya mporomoko unaotarajiwa, baada ya mazungumzo yaliyosifiwa kupiga hatua moja mbele, japokuwa wengine wameonya kuwa mazungumzo magumu bado yanakuja.

Aidha wameidhinisha mpango wa awali wa kipindi kifupi wa euro bilioni 540 na wakautaka mpango huo kuanza kufanya kazi mwanzoni mwa Juni.

Ugonjwa huo unaonekana kuongezeka barani Ulaya na Marekani, mataifa mengine yangali katika hatua za mapema za vita hivyo ambavyo mpaka sasa vimewauwa Zaidi ya watu 190,000 na kuwaambukiza milioni 2.7 kote duniani.

CHANJO, KIRUSI NA MIALE YA JUA

WHO limeonya kuwa hatua kali zinapaswa kuendelea kutekelezwa hadi pale tiba mwafaka au chanjo vitakapopatikana.

Juhudi zinaendelea kote duniani, huku Chuo Kikuu cha Oxford kikizindua majaribio ya chanjo kwa binaadamu.

Ujerumani imetangaza kuwa majaribio ya aina hiyo yataanza wiki ijayo.

Katika Ikulu ya Marekani, wanasayansi wamesema wamegundua kuwa kirusi hicho kinaharibiwa haraka na miale ya jua, na kutoa matumaini kuwa janga hilo litapungua wakati msimu wa joto ukianza.

Baadhi ya nchi za Ulaya zimeanza kuondoa taratibu vizuizi vya kupambana na virusi vya corona, lakini marufuku dhidi ya mikusanyiko mikubwa imeongezwa.

Migahawa, mabaa na matukio ya michezo bado vimefungwa.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ametangaza kuwa serikali itaanza kuondoa vizuizi vilivyowekwa kuanzia Mei mosi. Ramaphosa

amesema utaratibu huo utafanywa kwa umakini na tahadhari kubwa.

Watu milioni 58 nchini Afrika Kusini wamefungiwa majumbani mwao kwa wiki tano, isipokuwa tu kama unataka kununua chakula au dawa. Nchi hiyo imerekodi visa zaidi ya 3,953 vya maambukizi na vifo zaidi ya 75

Vizuizi vilivyowekwa na serikali mbalimbali vitaathiri ulimwengu wa Kiislamu ambao wiki hii unaanza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

MTANZANIA

No comments: