ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 26, 2020

Waliokutwa na kilo 270 za dawa za kulevya kizimbani

KULWA MZEE – DAR ES SALAAM

RAIA wa Nigeria, David Chukwu (38) na Watanzania wawili wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kukutwa na kilo zaidi ya 270 za dawa za kulevya aina ya heroine.

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Godfrey Isaya na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, Veronica Matikila, Wakili wa Serikali, Batilda Mushi.

Wakili Batilda aliwataja washtakiwa kuwa ni raia wa Nigeria, Chukwu Mkazi wa Masaki,

Isso Lupembe (49) Mkazi wa Mbezi na

Allistair Mbele (38).

Alidai watuhumiwa walikamatwa Aprili 15, 2020, wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zinazokadiriwa kuwa ni zaidi ya kilo 270.

Katika tarehe hiyo washtakiwa wanadaiwa walikutwa maeneo ya Mbezi kibanda cha mkaa wakisafirisha kilo 268.50 dawa za kulevya aina ya heroine.

Shtaka la pili lilisomwa na Wakili Wankyo ambaye alidai washtakiwa wanadaiwa kutakatisha fedha.

Inadaiwa Januari Mosi 2016 na Aprili 15,2020, walijihusisha miamala ya fedha Dola za Marekani 61,500 na 17,835,000 huku wakijua ni zao tangulizi la biashara ya dawa za kulevya.

Upande huo wa Jamhuri ulidai upelelezi haujakamilika na kwamba washtakiwa wanakabilika na makosa ambayo hayana dhamana.

“Tumepima afya za washtakiwa virusi vya corona na majibu yao ni ‘negative’ kuonyesha kwamba tuko makini,” alidai.

Hakimu Isaya alisema wamefanya vizuri kuwapima na aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 8,2020 itakapotajwa tena.

MTANZANIA

No comments: