ASIKWAMBIE mtu, maumivu ya kumpenda mtu halafu yeye akawa hakuelewi huwa yanauma sana. Unateseka kisaikolojia, unafanya kila unalotakiwa kufanya ili aweze kuelewa lakini mwenzako wapi. Ni kama vile unampigia mbuzi gitaa, hachezi yeye anabaki anakutazama tu.
Najua hii inawakuta sana wanaume ambao kiasili ya Mtanzania mara nyingi wao ndio huanza kueleza hisia zao lakini hata wanawake pia huwa inawatokea. Mwanaume anatuma meseji ndefu halafu majibu yanakuja yale mafupimafupi; ok, yeah, pow na mengine mengi yanayofanana na hayo.
Mwanaume anajaribu kujizungumzisha maneno mengi, akitegemea kupata majibu yenye kutia moyo lakini badala yake anaambulia majibu mafupi na yenye kukatisha tamaa hata ya kumzungumzisha kwa mara nyingine.
Umeuvaa ujasiri, umemueleza kwamba unampenda na unamhitaji maishani mwako, lakini yeye hata hana muda na wewe. Anaendelea na maisha yake kama kawaida, wakati wewe ukimfikiria, ukimuwaza usiku kucha mwenzako hata mshipa haumgongi.
Hapo ndipo mapenzi yanapogeuka mateso. Ndugu zangu, inapotokea hivyo jua kuna sababu. Yawezekana akawa unayemhangaikia ana mtu wake. Anamheshimiwa aliyenaye, haoni sababu ya kumuacha yeye na kuwa na wewe.
Yawezekana huyo unayempenda na kumueleza, ametoka kuumizwa na mpenzi wake. Hatamani kuwa na mpenzi kwa wakati huo na ndio maana anakupotezea. Anajua wewe ndio walewale, hataki kuumizwa kichwa chake kukufikiria.
Kuna mwingine anaweza kuwa hana mpenzi, hajatendwa kwa wakati huo lakini hajavutiwa tu na wewe. Waswahili wanakwambia kwa lugha ya ‘damu zenu hazijaendana.’ Mtu wa aina hiyo hata uhangaike vipi, atakutolea nje tu. Hawezi kukupa ushirikiano wowote.
Hoja yangu hapa ni nini? Unapaswa kujua kwamba mahusiano mazuri huwa yanajileta yenyewe. Huwezi kutumia nguvu nyingi sana kulazimisha. Huwa yanatokea kama ajali. Utashangaa tu siku ambayo hujatumia hata nguvu nyingi lakini inatokea tu.
Hukuwa na hata mpango wa kukutana na mtu fulani, mnapokutana mnajikuta tu mkichangamkiana. Mkipeana kampani, mkabadilishana namba za simu na mwisho wa siku mnaanzisha safari ya uhusiano na hata kuweza kuoana.
Siku hiyo hata wewe mwenyewe utashangaa jinsi utakavyoona mambo yanajipa kirahisi wakati kuna mahali ulitumia nguvu nyingi bila mafanikio. Kuna mahali ulipenda, ulitumia nguvu nyingi lakini uliambulia patupu.
Kikubwa unachotakiwa kukifanya pindi unapoona mtu ambaye unapendezwa naye, thubutu tu kumweka karibu. Fanya naye mawasiliano na uweze kumueleza kile kilichopo ndani ya moyo wako. Mueleze kwamba unampenda, unamhitaji katika safari yako.
Tumia kila aina ya ushawishi unaojua kumfanya mtu unayempenda awe wako. Yawezekana akakuonesha majibu ya mkato ya kukatisha tamaa, yawezekana akakujibu majibu ya dharau, lakini wewe usikate tamaa.
Pambana kwa kiasi ambacho kweli aone upo serious unamhitaji. Ikifika mahali ukaona umepambana kiasi cha kutosha, basi achana naye. Epuka kuwa kero kwa yule unayemueleza hisia zako maana kama nilivyosema yawezekana hakuhitaji kutokana na ile sababu ya kutovutiwa na wewe au pengine anaye mtu ambaye anamheshimu.
Heshimu hisia zake na dunia hii haijaisha wachumba, ipo siku utakutana na mwingine ambaye hata hatakuzungusha, hatakusumbua na ukisema mara moja tu anakuwa ameshakuelewa sababu huyo ndiye ambaye mnaendana.
Huyo ndiye ambaye ‘damu’ zenu zinafanana. Huyo ndiyo mwenzi wako wa maisha na mkianzisha maisha ya uhusiano, mtadumu miaka mingi!
Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, Instagram na Facebook natumia jina la Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.
Erick Evarist, GPL
No comments:
Post a Comment