ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 5, 2020

Johnson Aelezea alivyopona corona



LONDON, UINGEREZA, Mtanzania

WAZIRI Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson ameweka wazi kwamba mipango ya dharura ilikuwa imefanywa wakati alipokuwa mgonjwa sana hospitali akiugua ugonjwa wa virusi vya corona.

Katika mahojiano na gazeti la the Sun jana Jumapili, Johnson alisema aliwekewa lita nyingi za oksijeni ili kumwezesha kuwa hai.

Alisema uwepo wake katika hospitali ya St Thomas huko London ulimwacha akiwa na hamu ya kutaka wengine wasitaabike kama ilivyotokea kwake na kuhakikisha Uingereza inarejea katika hali yake ya kawaida.

Awali, mchumba wake, Carrie Symonds, alisema mtoto wao wa kiume amepewa jina la Wilfred Lawrie Nicholas Johnson.

Majina hayo yakiwa yametokana na babu yao na madaktari wawili waliomtibu waziri mkuu Johnson alipokuwa hospitali kwasababu ya virusi vya corona, Symonds aliandika kwenye akaunti yake ya Instagram.

Kijana wao alizaliwa Jumatano, wiki kadhaa baada ya Johnson kutoka hospitali alipokuwa anatibiwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

Katika mahojiano yake kwenye gazeti hilo, Johnson alielezea alivyounganishwa kwenye nyaya kadhaa kufuatilia hali yake na kubainika kwamba “viashiria vilkuwa vinaenda katika upande usio sahihi”.

“Ulikuwa wakati mgumu sana, hilo siwezi kupinga,” alinukuliwa akisema, akiongeza kwamba kila wakati alikuwa anajiuliza: “Nitawezaje kuepuka hili?”

Johnson alibainika kuwa na virusi vya corona Machi 26 na kulazwa hospitali siku 10 baadae. Siku iliyofuata, alipelekwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.

“Ilikuwa vigumu kuamini kwamba ndani ya siku chache tu, hali ya afya ilikuwa imezorota kiasi kile. Madaktari walikuwa wamefanya maandalizi yote kuhusu kile kitakachofanyika iwapo hali itaendelea kuwa mbaya,” Johnson aliliambia gazeti la the Sun Jumapili.

Kupona kwake, anasema kulitookana na huduma bora aliopata.

Johnson alisema alijihisi mwenye bahati hasa ikizingatiwa kwamba wengi bado wanataabika, na kuongeza: “na iwapo utaniuliza mimi, ‘Je nimepata msukumo wa kuhakikisha wengine hawapitii tabu hii? ‘ Ndio, bila shaka uo ndio ikweli. “Lakini pia nimepata msukumo wa kutaka kuhakikisha nchi yetu inarejea katika hali yake ya kawaida, kuwa imara tena na nina uhakika tutafika tu,” alisema.

Idadi kamili ya waliokufa kwa magonjwa yenye kuhusishwa na virusi vya corona nchini Uingereza hadi kufikia sasa ni 28,131, ikiwa ni ongezeko la watu 621 kutokea Ijumaa.

Hata hivyo, Naibu Ofisa wa Matibabu Uingereza Dk. Jenny Harries alisema idadi ya wagonjwa wanaotibiwa hospitali kwasababu ya virusi hivyo imepungua kwa asilimia 13 katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

No comments: