By THOMAS NG’ITU NA BETHA ISMAILMwanaspoti
BAADA ya Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), kuipa ubingwa klabu ya Gor Mahia kutokana na kuufuta msimu kwa sababu ya corona, Simba imewataka viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kukaa na kuzungumzia mustakabali wa ligi.
Lakini wanachama wao kwenye matawi ya Arusha, wakisapotiwa na wenzao wa Yanga wamependekeza biashara iishe kwavile kila kitu kipo wazi.
“Siwezi kusema lolote kwa sababu wapo kimya kwa muda mrefu, nadhani wanatakiwa kuitisha kikao na Bodi ya Ligi na viongozi wa klabu kwa pamoja,” alisema Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa.
“Kikao ndio kitakachoamua kila kitu, na hakika hakitaweza kumbeba yoyote yule, bali ni uamuzi wa kwenye kikao,” alisema Senzo.
Uongozi wa wanachama wa matawi ya Yanga mkoa wa Arusha wao wamesema kuwa uamuzi wowote utakaofikiwa na TFF hauwezi kivyovyote kuwapatia nafasi ya ubingwa hivyo wameamua kujiweka kando na ubishi huo lakini wakasisitiza; “Simba wapewe nafasi, sio kombe.”
Katibu wa matawi ya Yanga mkoa wa Arusha, Bahati Lumato alisema; “Kikubwa kanuni na busara zitumike tu katika uamuzi utakaopitishwa ikiwamo kuwaita viongozi wa klabu timu husika kuamua hatma ya ligi yetu.”
“Sisi kama Yanga hasa mimi binafsi nitakubali tu uamuzi wowote wa Simba kutangazwa bingwa na kutuwakilisha kwa alama alizonazo au kumaliza ligi maana kwa matokeo ya michezo 26 tulizokwisha kucheza tumeshapoteza uelekeo,” alisema huku akisapotiwa na wanachama wenzie wa Arachuga.
Lumato alisema kuwa Simba hawana haki ya kupatiwa kombe kwa vile hawajalitetea uwanjani kwa mujibu wa kanuni bali kutokana na dharura iliyojitokeza anaweza kupewa tu nafasi ya kuwakilisha nchi kimataifa
Katibu wa matawi ya Simba mkoa wa Arusha, Thabit Ustadhi alisema; “TFF wanavyozidi kuchelewesha mambo ndio yanafelisha baadhi ya mipango maana kivyovyote lazima Tanzania iwe na mwakilishi katika michuano ya kimataifa na kanuni inamtaka bingwa wa nchi husika ndio awakilishe hivyo tayari Simba anazo asilimia zaidi ya 90 kupata nafasi hiyo sasa kwanini uamuzi usifikiwe?”
Alisema wao hata wakipangiwa wamalize ligi bado wanayo nafasi ya kutetea ubingwa wao.
Simba ndio wanaongoza Ligi wakiwa na pointi 71 katika michezo 28 waliyocheza huku nafasi ya pili ikishikiliwa na Azam FC wenye pointi 54 katika michezo 28 waliyocheza.
Yanga wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi 51 katika michezo 27.
Gor Mahia nchini Kenya wao wamepewa ubingwa huo wakiwa wanaongoza ligi kwa pointi 54 baada ya mechi 23, nafasi ya pili ikishikiliwa na Kakamega Homeboys wenye pointi 47 baada ya kucheza michezo 22. Tusker ya 3 kwa pointi 46 katika michezo 22.
No comments:
Post a Comment