ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 7, 2020

Watu maarufu waliopoteza maisha, jamii kudhani ni corona

Getrude Lwakatare

Na MWANDISHI WETU, Mtanzania

NDANI ya kipindi cha wiki tatu mfululizo, watu kadhaa maarufu hapa nchini wamepoteza maisha na taarifa zao kusambaa mitandaoni huenda vifo vyao vimesababishwa na maambukizi ya virusi vya corona.

Japo sababu ya vifo vyao kutosemwa ama kuwa ni tofauti na corona kumekuwa na mjadala wa namna vilivyotokea ghafla na kwa kuongozana pia na hatua za tahadhari ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwenye mazishi yao.

Getrude Lwakatare, ambaye alikuwa Mchungaji Mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto, jijini Dar es Salaam, na Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) aliaga dunia Aprili 20 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa familia yake, kifo chake kilisababishwa na shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Siku moja baadaye, Spika wa Bunge Job Ndugai, akatangaza kuwa mazishi yake yatasimamiwa na serikali na kwamba yatahudhuriwa na watu wasiozidi 10.

Japo haikusemwa kuwa ni corona, ila ni utaratibu wa serikali kuongoza mazishi ya watu waliofariki kwa virusi hivyo na kuzuia idadi ya waombolezaji kwa uchache unaowezekana.

Abdulkarim Shah

Siku chache baadae, Aprili 25 aliyewahi kuwa mbunge wa kisiwa cha Mafia Abdulkarim Shah, alifariki dunia katika hospitali moja jijini Dar es Salaam na kuzikwa asubuhi ya siku iliyofuata na watu wachache.

Evod Mmanda

Aprili 27, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda, alifariki dunia. Akithibitisha taarifa za kifo chake Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alisema Mmanda alilazwa hospitali kwa siku mbili kabla kufikwa na mauti na alikuwa akikabiliwa na ‘changamoto za upumuaji.’

Mazishi ya Mmanda yalifanyika siku iliyofuatia yakisimamiwa na serikali huku ndugu zake 10 tu wakiruhusiwa kushiriki.

Tarehe 27 Aprili pia ilishuhudia majaji wawili wastaafu hapa nchini wakifariki, Jaji Ali Haji Pandu ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na mmoja wa waasisi wa chama cha CUF na Jaji Mussa Kwikama ambaye alikuwa kiongozi mwandamizi wa Chama cha ACT Wazalendo.

Siku hiyohiyo, Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro, Isihaka Sengo, alifariki dunia hospitalini. Siku iliyofuata mazishi yake ambayo yalikuwa yamepangwa na familia yalisitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, akisema marehemu alionesha dalili za virusi vya corona na baadae mazishi yake yalisimamiwa na serikali na kuhudhuriwa na ndugu wachache.

Augustino Ramadhani
Aprili 28, Tanzania ilimpoteza Jaji Mkuu wake Mstaafu, Augustino Ramadhani. Taarifa rasmi za Mahakama na Serikali ni kuwa Jaji Ramadhani alikuwa akisumbuliwa na saratani kwa zaidi ya miaka miwili na alipelekwa hospitali siku chache kabla ya kifo chake baada ya kuzidiwa.

Richard Ndassa
Siku moja baadaye, Aprili 29, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa, alifariki dunia baada ya kuugua ghafla, japo ugonjwa uliosababisha umauti wake haukutajwa.

Baada ya kifo chake, hoteli aliyokuwa akikaa mbunge huyo ilinyunyiziwa dawa na hakuna mtu aliyeruhusiwa kuingia kwa muda.

Balozi Augustine Mahiga
Ambassador Augustine Mahiga,

Ijumaa ya Mei Mosi, Watanzania waliamka na taarifa ya tanzia kutoka kwa Rais Dk. John Magufuli, akitangaza kifo cha aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Balozi Augustine Mahiga.

Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa mwanadiplomasia huyo nguli aliugua ghafla alfajiri ya siku hiyo nyumbani kwake mjini Dodoma na alipofikishwa hospitali alikuwa ameshafariki.

Hicho kilikuwa ni kifo cha tatu cha mbunge katika kipindi cha chini ya wiki mbili. Hali hiyo ililazimu chama kikuu cha upinzani nchini – Chadema, chini ya Mwenyekiti wake Freeman Mbowe, kuwataka wabunge wake kutokuhudhuria bungeni na kujitenga karantini kwa siku 14.

Chama hicho pia kimetoa rai kwa Bunge kuahirishwa kwa siku 21, lakini hadi sasa vikao vinaendelea na Rais Dk. Magufuli ameagiza wabunge hao wasiohudhuria vikao kutolipwa posho zao.

Mchungaji Peter Mitimingi
Usiku wa Mei 3, Mchungaji Maarufu wa Kanisa la Ghala la Chakula cha Uzima, Peter Mitimingi, alifariki dunia baada ya kuugua ghafla.

Mitimingi alikuwa maarufu kwa mahubiri yake ya mitandaoni yaliyokuwa yakilenga nyanja mbalimbali za kimaisha kuanzia uhusiano, masomo hadi ujasiriamali. Aliwateka zaidi wakina dada kwa mada zake zinazohusu masuala ya uhusiano.

Kabla ya kifo chake, Mchungaji Mitimingi aliwahi kuweka picha kwenye mtandao wa Instagram akiwa anapata chakula akisema: “ Pale unapokuwa karantini na siku zinakimbia kama umeme. Ngoja nishtue ‘ka appetizer’ haka wakati wananiandalia mlo wenyewe! Maisha ya karantini siku 14,” alisema akamalizia na kicheko.

Masumbuko Lamwai

Usiku wa Mei 4, mwanasheria na mwanasiasa maarufu nchini, Dk. Masumbuko Lamwai, pia alifariki ghafla.

Taarifa zilizothibitishwa na familia yake ni kwamba Dk. Lamwai aliumwa na kuzidiwa ghafla na alipokimbizwa hospitali madaktari walithibitisha kuwa ameshafariki.

Lamwai alikuwa ni miongoni mwa wanasiasa machache wa mwanzo wa upinzani na alishinda ubunge kwa tiketi ya upinzani mwaka 1995. Pia alikuwa wakili maarufu na mhadhiri mwandamizi wa sheria.

Sheikh Suleiman Kilemile

Usiku wa kuamkia jana, Mei 6, Sheikh maarufu hapa nchini, Suleiman Kilemile, alifariki dunia. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu hivi karibuni alirekodiwa akiwataka Waislamu kuchukua tahadhari na kuwataka wenye nacho kutoa sadaka ya sabuni misikitini ili watu wanawe kwa maji na sabuni kama wanavyoshauri wataalamu wa afya.

Sio wote waliokufa ni corona

Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imekuwa ikisisitiza kuwa sio wote wanaofariki dunia katika kipindi hiki, basi vifo vyao vinatokana na maambukizi ya corona.

Rais Dk. Magufuli pia amekuwa akitoa tahadhari kuwa si kweli watu wote wanaofariki katika kipindi hiki ni kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, wapo wanaofariki kutokana na maradhi mengine hivyo hakuna sababu ya watu kutiana hofu.

Rais Dk. Magufuli akilihutubia taifa siku ya Jumapili alisisitiza hilo na kusema haiwezekani wote wanaokufa kuwa na corona na kwani kuna magonjwa mengine pia.

“…japo siyo vizuri kutoa taarifa za watu, lakini Jaji Ramadhani kwa mfano, amesumbuliwa muda mrefu na saratani, hata baba yangu alifariki kwa saratani. Tulihangaika na Jaji Ramadhani India na mwishoni hapa tukampeleka hadi Nairobi, Kenya… haiwezekani kila anayekufa ni corona tu.”

No comments: