Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo, akifungua mafunzo ya utalii kwa vijana zaidi ya 52 wa wilaya hiyo, ikiwa ni mkakati maalumu wa kuandaa vijana na wananchi kufahamu fursa za utalii kwa maendeleo katika wilaya hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dk. Shogo Sedoyeka na Ofisa wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Anna Lawuo.
Na MWANDISHI WETU-PWANI
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, imeamua kuwaandaa vijana zaidi ya 52 kwa kuwapatia mafunzo ya utalii na kutambua fursa zilizopo katika sekta hiyo ikiwa ni mkakatiwa kuinua utalii wilayani humo pamoja na kujiandaa kupokea wageni ambao watakuwa wanapita hapo kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Mafunzo hayo yalifunguliwa jana na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo, ambapo alisema kuwa vijana ndani ya wilaya hiyo kwa sasa wameamka na wapo tayari kuchangamkia fursa mbalimbali za utalii hasa kwa kuzingatia wamebarikiwa kuwa na kila aina ya vivutio vya utalii.
Alisema kuwa hakuna sababu ya vijana kuendelea kubaki nyuma wakati fursa zipo hivyo wahakikishe kwamba kila wanachokiona Wilayani humo ni fursa niwajibu wao Sasa kuchangamkia fursa hizo.
“Wilaya Kisarawe inafursa kubwa ya utalii kwani inavivutio vingi na ukizingatia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa, imepandisha hadhi msitu wa Pugu pamoja na Kazimzumbwi na pia kuna mapango mengi ya utalii hivyo zote hizo ni fursa,” alisema Jokate
Alisema kuwa Kisarawe imekuwa ni chachu ya kuongeza mapato ya halmashauri hiyo ambapo miaka kadhaa ilikuwa inakusanya Sh bilioni moja na kwa sasa yamepanda zaidi na kufikia kukusanya Sh bilioni 2.7 kwa mwaka.
“Kuongezeka kwa utalii kupitia misiru hii ni wazi kwamba mapato yanakwenda kuongezeka na ndiyo maana leo wameona fursa hiyo kuwapa mafunzo vijana kutoka ndani ya kisarawe ili mwisho wasiku waweze kuongoza watalii,” alisema
Mkuu huyo wa wilaya alimpongeza Rais Dk. John Magufuli kwa kuweza kuona umuhimu wa kujenga barabara ya Kisarawe kwenda Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kwa kiwango cha lami jambo ambalo sasa litachochea maendeleo kutokana na shughuli za utalii.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii, Dk. Shogo Sedoyeka alisema kuwa Kisarawe ni eneo zuri na limejaliwa kuwa shughuli nyingi ikiwamo kuwa lango la utalii kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
No comments:
Post a Comment