ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 1, 2020

Mwili waopolewa Ziwa Victoria


Na Nyemo Malecela-Kagera

MWILI wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na miaka 30 hadi 35, umekutwa na Padri Deritius Rweumbiza wa Kanisa Katoliki la Bunena lililopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera ukielea kwenye maji ya Ziwa Victoria.

Kamanda wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto mkoani Kagera, Hamisi Dawa amesema padri huyo aliuona mwili huo ukielea kwenye maji wakati akiwa katika matembezi yake kwenye fukwe za ziwa hilo zilizopo karibu na makazi ya mapadri.

“Baada ya Padri Deritius kutupatia taarifa saa nne na dakika mbili tuliweza kuuopoa mwili huo ukiwa umevimba sana, hivyo haijulikani lini ulizama maji,” alisema Kamanda Dawa.

Alisema bado haijulikani kama mtu huyo wakati anakutwa na mauti alikuwa muogeleaji au alipata ajali, kwani kwa jinsi Ziwa Victoria lilivyojaa maji yaliyofunika fukwe, uwezekano wa kusababisha maafa ni mkubwa.

“Lakini pia bado haijulikani marehemu alitokea wapi, hivyo mwili wake umepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera ukisubiria kutambuliwa,” alisema Kamanda Dawa.

Wakati huo huo, Kamanda Dawa alisema idadi ya matukio kwa mwaka huu imepungua ukilinganisha na mwaka uliopita.

“Kwa mwaka jana Mkoa wa Kagera ulikuwa na matukio 76 ambapo ya maokozi yalikuwa 22 ya moto yalikuwa 54. Mwaka huu tangu uanze, matukio ya moto ni 40 na ya maokozi ni 10, hivyo tumepunguza matukio 26.

“Kufuatia kuendelea kuwepo kwa matukio hayo, tunawashauri wavuvi kabla hawajaingia ziwani kwa ajili ya shughuli zao wanatakiwa kuwasiliana na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) ili kujua hali ikoje ziwani,” alisema Kamanda Dawa.

Alisema hata Jeshi la Uokoaji na Zimamoto wamekuwa wakiwatumia TMA kuwapa taarifa ya mwelekeo wa hali ya hewa, hivyo hata wavuvi wanatakiwa kuwatumia ili kuepuka matukio ya kupotea ziwani kutokana na kukumbwa na dhoruba au kuzama.

“Ili kuhakikisha tunafanya kazi vizuri, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli ametupatia Sh milioni 1.467 ambazo nimezikabidhi kwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto Taifa ili kuunga mkono jitihada za wananchi walioanza kujitolea kujenga kituo cha Zimamoto wilayani humo.

“Hadi sasa tayari ujenzi uliofanyika ni zaidi ya Sh milioni 20 na baada ya ujenzi huo kukamilika, tunatarajia kupeleka gari la Zimamoto katika kituo hicho ambalo tunatarajia kulifanyia ukarabati maana lilipata itilafu kidogo,” alisema Kamanda Dawa.

No comments: