SALVATORY NTANDU
Masunga Nindwa (36)mkazi wa Lunzwe mkoani Geita na Peter Matiko mkazi wa nyakato mkoani Mwanza wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya bangi kilogramu 20 na mirungi kilogramu 25.
Akizungumza waandishi wa habari Kamanda wa jeshi la polisi mkoani humo (ACP) Debora Magiligimba alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa katika matukio mawili tofauti baada ya kufanyika kwa msako mkali wa jeshi hilo ambao umefanikisha kukamatwa kwa dawa hizo.
Katika tukio la kwanza Masunga Nindwa alikamatwa na jeshi la polisi wilayani kahama mei 21 mwaka huu katika nyumba ya kulala wageni ya kalunde iliyopo katika mtaa wa nyasubi akiwa na debe mbili za bangi zenye uzito wa kilogramu 20 huku akijua wazi kuwa kufanya hivyo ni kosa la jinai.
Kamanda Magiligimba alisema kuwa katika tukio la pili mei 21 mwaka huu majira ya asubuhi katika kata ya Ibinzamata Peter Matiko alikamawa na jeshi hilo akiwa na mirungi kilogramu 25 iliyokuwa imewekwa kwenye mabegi aliyokuwa anaisafirisha kwenda mkoani Singida.
“Jeshi la polisi lilipata taarifa za kiintelijensia kutoka kwa wasamaria wema na kuanza kuafuatilia na kisha kufanikiwa kuwakamata na dawa hizo za kulevya,mtuhumiwa wa mirugi alikiri kutumia na kuuza dawa hizo upelelezi ukikamilika tutawafiksha mahakamani,”alisema Magiligimba.
Sambamba na hilo Magiligimba alisema kuwa jeshi hilo pia linamshikilia Elida Zakaria (19)mkazi wa kagongwa kwa tuhuma za kukutwa na kete 111 za dawa za kulevya aina ya bangi zilizokuwa zimefungwa kwenye magazeti nyumbani kwa Lucia Luhende ambaye ndiye mmiliki wa dawa hizo
“Tunatarajia kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote upelelezi ukikamilika na tunatoa rai kwa wananchi kuwafichua watu wanaouza na kusafirisha dawa za kulevya ambazo zimekuwa zileta athari kwenye jamii”,alisema Magiligimba.
No comments:
Post a Comment