KATIBU Mkuu wa Wizara ya Katiba
na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, ametoa
ahadi ya kuchangia shilingi milioni
tano ukiwa ni mchango wake wa kusaidia kukamilisha Zahanati ya Jeshi la Polisi Wilayani Mpanda, Mkoani Katavi.
Ametoa mchango huo baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Benjamin E.
Kuzuga kuelezea kwamba, Jeshi la Polisi Mkoani humo
limekamilisha ujenzi wa Zahanati yake,
lakini bado haijaanza kutoa huduma kutoka na
ukosefu wa vifaa tiba, madawa na
samani.
Aidha Kamanda Kuzunga alieleza kwamba kama Zahanati hiyo ingeanza kutoa huduma basi pia kituo cha mkono kwa mkono ( one stop center)
ambacho pamoja na mambo mengine
kingeweza kutoa huduma na faragha
kwa akina mama na watoto wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hayo yamejili wakati wa kikao kilichofanyika mwishoni mwa
wiki wilayani Mpanda , Mkoani Katavi
kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria , Katibu Mkuu wa
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na baadhi ya Maafisa
na Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Katavi. Kikao hicho kilichofanyika katika Bwalo la Polisi
kilikuwa ni cha kubadilishana mawazo
kuhusu hali ya utoaji wa Hakijinai kwa
upande wa Jeshi la Polisi.
“Changamoto moja kubwa ni ya kutokuwa na kituo cha mkono kwa mkono ( one stop center)
kutoka na kutokuanza kufanya kazi kwa Zahanati yetu ambayo ujenzi wake
umetokana na michango ya askari na
maafisa na kuchangiwa pia na Mkuu wa
Jeshi la Polisi ( IGP) na baadhi
ya wadau wengine, hata hivyo jengo
limeshindwa kuanza kazi kutokana na kutokuwa na vifaa tiba, madawa na samani”
akasema ACP Kuzunga.
Amebainisha kwamba ujenzi wa Zahanati umegharimu takribani shilingi
Milion 70. Na kwamba zinahitajika shilingi milioni 24 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba na mambo mengine na
tayari wameshanunua baadhi ya vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 3.
“Katika hili la Zahanati, kwanza
niwapongeze kwa juhudi zenu hizi, basi mimi
nitachangia shilingi Milioni Tano
ili zisaidie mambo fulani fulani
kwasababu jambo mmlilolibuni ni
jema” akaahidi Katibu Mkuu Profesa Mchome.
Katibu Mkuu Profesa Sifuni
Mchombe akiambatana na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na
Watoto, walipata fursa ya kuitembelea Zahanati hiyo wakiongowa na Kamanda wa
Polisi ambaye aliwaeleza kwamba,Zahanati hiyo
ina vyumba vya madaktari vitatu, chumba cha maabara, chumba cha
kuhifadhia dawa na chumba wa akina Mama
na chumba cha watoto.
Kuhusu upatikanaji wa madaktari, Kamanda ACP Benjamin Kuzuga amesema
Mganga Mkuu wa Mkoa pia ameahidi
kuangalia uwezekano wa kusaida katika eneo hilo.
Wakati Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Profesa
Mchombe akiahidi kutoa milioni Tano, kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. John Kingu ameahidi kuisaidia zahanati hiyo
gari pamoja na vifaa vingine ili
hatimaye zahanati iweze kuanza kazi
haraka iwezekanavyo.
Awali Katika kikao hicho cha Makatibu Wakuu na Maafisa na Askari wa Jeshi
la Polisi ,RPC pia alielezea ukosefu wa majengo
ya Kituo vya Polisi karibu katika wilaya zote za mkoa huo pamoja na ukosefu wa
nyumba za askari .
Akasema hata Ofisi yake ipo
katika Jengo ambalo ni Kituo cha Polisi
cha Wilaya ya Mpanda.
“Waheshimiwa Makatibu Wakuu, kwa
kuwa Mkoa huu ni mpya, tunashida sana ya
Majengo ya Vituo vya Polisi , hata askari wetu wanaishi uraiani ama katika
nyumba za kupanga au walizojenga wenyewe. Kiutendaji wa majukumu yetu hali hii
si salama sana, kwa sababu ikitokea dharura tu
itakuwa shida sana kukutana na kukusanyika mara
moja. Na ndiyo maana kiutaratibu askari wanatakiwa kuishi kambini ili
kukitokea dharura yoyote inakuwa rahisi
kuwasiliana”
Aidha RPC Kuzuga pia ameeleza kwamba hali hiyo ya kutokuwa na
Vituo vya Polisi kumepelekea kutokuwapo kwa vyumba maalumu vyenye mazingira
mazuri ya kusikiliza na kuchukua maelezo ya wahanga waliohujumiwa kijinsia na kwamba katika
baadhi ya maeneo imebidi askari na
wahanga hao kukaa chini ya miti ili
kuchukua maelezo yao au kuwapatia huduma
nyingine stahiki.
Wakati huo huo Katibu Mkuu
Profesa Mchome, amesema Jeshi la Polisi
ni sehemu ya mnyororo wa mchakato wa kuijenga Tanzania iliyobora na wananchi wake
kutekeleza majukumu yao bila hofu na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi
na maendeleo ya taifa lao.
Na kwa
sababu hiyo, amelitaka Jeshi la Polisi
Mkoani Katavi, kama chombo cha utoaji wa
HakiJinai kutekeleza majukumu yake kwa weledi, kwa kuzingatia kanuni, sheria na
taratibu ambazo Jeshi hilo limejiwekea
pamoja na Sheria za Utumishi wa Umma.
Akasema Jeshi la Polisi pamoja na changamoto
mbalimbali bado limeweza kutekeleza
majukumu yake ya utoaji Hakijinai, na akalitaka kutumia sheria ya ufifishaji wa
makosa hasa yale makosa madogomadogo ambayo yanaweza kuishia au kumalizwa katika Kituo cha Polisi na hivyo kujipunguzia wenyewe mzingo wa mafaili ya
upelelezi lakini kuvisaidia pia vyombo
vingine vya utoaji hakijinai mzigo wa
kuendesha mashataka na kesi na mlundikiano wa wafungwa na mahabusu.
Amebainisha kwamba, katika
mnyororo wa utoaji Hakijinai, Serikali
ya awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
imeelekeza mambo ya kutekeleza na Jeshi la Polisi kama sehemu ya Serikali
mnaowajibu pia wa kuyatekeleza.
Akayataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na kutenda haki kwa kila kosa
na kwa weledi, uadilifu, kujiamini
kuwajibika na kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu na kumaliza
baadhi ya mashauri kwa njia ya upatanishi na utoaji wa adhabu mbadala badala ya
kukimbilia mahakamani pasipo ulazima wa kufanya hivyo, mahakama iwe chombo cha
mwisho kabisa.
“Ujumbe
wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hasani kuhusu eneo la utoaji haki katika maeneo
mbalimbali ni kutenda haki, tusimbambikie watu kesi, anataka haki itendeke kwa
wakati na kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu, Jeshi la Polisi ni sehemu ya
mnyororo wa utoaji wa haki lakini pia mnao mchango mkubwa sana katika kuijenga
nchi yetu kiuchumi” akasisitiza Katibu
Mkuu Mchome.
Akalipongeza pia Jeshi hilo la
Polisi kwa kazi nzuri inayofanya kupitia
Dawati la Jinsia, Dawati ambalo
limekuwa kimbilio na faraja wahanga wa matukio mbalimbali hasa ya
udhalilishaji wa kijinsia wanaotafuta haki zao.
Makatibu Wakuu wa Wizara ya
Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wapo katika Ziara ya Kikazi
ya Kawaida ambayo imewafikisha katika
Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na katika
mikoa hiyo yote Makatibu Wakuu hao wamekuwa na vikao mbalimbali na Wadau
wa Mnyororo wa Utoaji Hakijinai na
Watumishi wa Serikali.
No comments:
Post a Comment