Mhe. Abdullah ametoa agizo hilo hivi karibuni wakati akifungua rasmi Kongamano la Maadhimisho ya Miaka 40 ya SADC lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na kuwashirikisha wanafunzi na wadau kutoka sekta mbalimbali.
Mhe. Abdullah amesema kuwa, Lugha ya Kiswahili ambayo ilipitishwa kuwa miongoni mwa Lugha nne rasmi zinazotumika SADC ni rasilimali mojawapo inayoweza kuchangia uchumi wa nchi endapo Serikali, Taasisi, Mashirika na Wadau mbalimbali watashirikiana kikamilifu ili kuifanya lugha hiyo kuwa bidhaa inayouzika katika nchi za SADC.
“Kwa kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha mama, lugha ya taifa na rasmi kwenye Taifa letu ni vizuri Kongamano hili likachambua kwa kina jinsi ambavyo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla inaweza kunufaika na Lugha hii kupitia Jumuiya. Pia tuchekeche kwa undani na kupendekeza kile ambacho Serikali inaweza kufanya kwa kushirikiana na wadau husika ili kuona Kiswahili kinakuwa ni bidhaa inayouzika kwa nchi za SADC” alisema Mhe. Abdullah
Aliongeza kusema kuwa kwa sasa wapo vijana wengi wahitimu wa ngazi mbalimbali wa mafunzo ya ualimu wa Kiswahili na hawana ajira, hivyo alisema vijana hao wanaweza kutumia fursa hiyo na kwenda kufundisha Kiswahili kama lugha ya pili katika nchi za SADC.
Kadhalika Mhe. Abdulah alitumia fursa hiyo kulikumbusha Baraza la Kiswahili la Zanzibar kuzingatia maelekezo yaliyotolewa kwao wakati wa Kongamano la Kiswahili lililofanyika mwaka 2020 ya kujiimarisha ili kuona Kiswahili kinastawi na kuuzika nje ya nchi kwa faida ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Mbali na Lugha ya Kiswahili, Mhe. Abdullah aliwataka washiriki wa Kongamano hilo pia kujadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kunufaika na Sekta ya Uchumi wa Bluu ambayo ni miongoni mwa sekta za kipaumbele za Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar.
“Napenda kuwakumbusha kwamba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya uchumi wa bluu inayoelekeza matumizi mazuri na endelevu ya rasilimali Bahari ili kuwawezesha wananchi kuondokana na umaskini. Hivyo basi ni muhimu kuonesha namna ambavyo Zanzibar inaweza kutekeleza kipaumbele hicho na kuimarisha sekta ya uchumi wa bluu kupitia SADC” alisisitiza Mhe. Abdullah.
Pia alisisiza umuhimu wa kutumia maadhimisho hayo kuuelewesha umma wa Watanzania kuhusu Jumuiya hiyo katika ustawi na maendeleo ya kiuchumi na kutoa wito kwa watanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye SADC.
Awali akizungumza wakati wa Kongamano hilo ambalo liliandaliwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na SUZA, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Simai Mohammed Said alisema kuwa kuwa upo umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano katika sekta ya elimu na nchi za SADC ili wananchi wa Tanzania wanufaike na fursa za elimu ikiwemo vyuo vya elimu ya juu vinavyopatikana kwenye nchi hizo.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha SUZA, Dkt. Zakia Mohammed Abubakar alisema kuwa Jumuiya ya SADC inazo fursa nyingi za kitaaluma na kitaalam ambazo zitasaidia Chuo hicho kujenga mashirikiano na vyuo ambavyo vipo katika nchi wanachama kwa manufaa ya watanzania.
Naye Mwakilishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambaye ni Balozi Mteule na Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar, Bw. Masoud Abdallah Balozi aliwashukuru wadau mbalimbali walioshiriki Kongamano hilo na kuwaomba kuendelea kushirikiana na Wizara ili kwa pamoja waweze kunufaika na Jumuiya ya SADC.
Wakati wa Kongamano hilo, mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa ikiwemo “Historia ya SADC” iliyowasilishwa na Waziri Wa Fedha Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Mohammed Ramia Abdiwawa mada isemayo “Fursa zilizopo SADC kwa Zanzibar” ambayo iliwasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrick Ramadhan Soraga na mada kuhusu “Mafanikio na Changamoto katika SADC iliyowasilishwa na Mhadhiri Mwandamizi wa SUZA, Dkt. Abdallah Rashid Mkumbukwa.
No comments:
Post a Comment