WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Mkoa wa Mara na Watendaji
katika Sekta ya Utalii wabadilike na waweke mkakati wa kuitangaza mbuga
ya Serengeti ili kuweza kuvutia zaidi watalii na kuitambulisha mbuga
hiyo kuwa iko mkoa humo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan inaboresha mazingira ya
uwekezaji na biashara ili kuvutia uwekezaji utakaoinua uchumi wa nchi na
watu na mwongozo huo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Serikali ya
kuvutia uwekezaji na kuimarisha biashara.
Waziri Mkuu ametoa
agizo hilo leo wakati akizindua Mwongozo wa
Uwekezaji wa Mkoa wa Mara katika Ukumbi wa Bishop Rudin uliopo katika
viwanja vya Mwembeni mjini Musoma. Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwaagiza viongozi wa mkoa huo wahakikishe watendaji, wataalamu na
wananchi wanakuwa nyenzo ya kurahisisha kazi ya kuvutia uwekezaji.
“Mheshimiwa
Mkuu wa Mkoa hakikisha watendaji wote wa mkoa wanausoma na kuuelewa
ipasavyo mwongozo huu. Hakikisha watendaji wako wanatekeleza majukumu
yao kwa weledi, uadilifu na uaminifu ili kufikia malengo
yaliyokusudiwa”.
Waziri Mkuu amesema mkoa huo una fursa nyingi za
uwekezaji ambazo endapo zitatumika vema, zinaweza kuipaisha nchi
kimaendeleo. “…Nitoe wito kwa uongozi mzima wa mkoa uhakikishe unaratibu
vilivyo shughuli za uzalishaji hasa wa malighafi, bidhaa na huduma
mbalimbali kwa ajili ya wananchi na mahitaji ya viwanda vya ndani.
Amesema
miongoni mwa maeneo ambayo mkoa wa Mara unaweza kunufaika zaidi kwenye
uwekezaji kutokana na fursa zilizopo ni kilimo, mifugo na uvuvi.
Serikali ilitoa maelekezo yenye lengo la kuboresha sekta ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi kwa ili kuzalisha malighafi za kutosha zitakazotumika
kwenye viwanda.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya
Uwekezaji ishirikiane na mkoa ili kuwezesha Kituo cha Uwekezaji cha
Kanda (TIC) kilichopo mkoani Mwanza kuanzisha Kituo cha Kutolea Huduma
kwa Pamoja (One Stop Centre) ambacho kinapaswa kuwa na rasilimali za
kutosha, vifaa na wataalam wote muhimu.
“Watu wote muhimu
wanaopaswa kutoa huduma katika kituo wawepo, wakiwemo wataalamu wa
Ardhi, Biashara, Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA), Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Shirika la Viwanda
Vidogo (SIDO), Wakala wa Vipimo, NEMC, Bodi ya Nyama, Bodi ya Maziwa”.
Pia
Waziri Mkuu ameziagiza idara zote za kisekta katika ngazi ya mikoa na
wilaya, zishirikiane katika kubuni njia rahisi zitakazosaidia kuondoa
urasimu na kurahisisha uwekezaji katika maeneo yao ili kuongeza ajira na
vyanzo vya mapato ya Serikali.
“…Viongozi na watendaji wa sekta
ya umma, fanyeni vikao na sekta binafsi kupitia Mabaraza ya Biashara ili
kujadili na kutatua kero za kibiashara na uwekezaji zinazowakabili kwa
wakati”.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka mamlaka husika
zihakikishe zinaweka mipango ya urasimishaji sekta isiyo rasmi,
kurasimisha namba msimbo, kuwapatia wafanyabiashara ndogo ndogo maeneo
ya kufanyia biashara na kuongeza kasi ya upimaji ardhi na kasi ya
utekelezaji wa anuani za makazi na postikodi kwenye Mamlaka za Serikali
za Mitaa ili kuchochea fursa za kibiashara.
No comments:
Post a Comment