ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 16, 2021

Serikali Kusimamia Uanzishwaji Vituo Vya Malezi Vya Kijamii


 Na Mwandishi Wetu Dodoma
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imesema kupitia Halmashauri zote nchini itaendelea kuhamasisha, kuratibu na kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa vituo vya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto  kwa kushirikisha wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.

Hayo yamesemwa jijini hapa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mwanaidi Ali Khamisi wakati akizindua kituo kijamii cha Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kushirikiana na Shirika la BRAC Maendeleo – Tanzania kilichopo katika kijiji cha Chamwino Ikulu Mkoani Dodoma

Naibu Waziri amesema kuwa kwa kushirikiana na wadau wa wa maendeleo Serikali itaendelea kuhamasisha na kuamsha ari ya wananchi ili kushiriki katika ujenzi wa vituo hivyo katika vijiji na mitaa yote nchini ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inapatikana.

 ''Serikali kupitia halmashauri zote nchini zitaendelea kuhamasisha, kuratibu na kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa vituo kwa kushirikisha wazazi, walezi na jamii kwa ujumla.''amesema Naibu Mwanaidi

Kuhusiana na kituo hicho, Naibu Waziri Mwanaidi amesema kuwa kitasaidia  kuwajenga watoto utimilifu wao ikiwa ni pamoja kuwapatia huduma jumuishi za afya, lishe, ulinzi, ujifunzaji na uchangamshi wa awali kabla ya kujiunga na darasa la awali wanapofikia umri wa miaka 5.

"Huduma hizo zinamwezesha mtoto kukua kimwili, kiakili, kisaikolojia na kimaono akiwa angali mtoto hali hiyo itasadia kuwa na Taifa lenye watu walioandaliwa kikamilifu kulitumikia,"alisema Naibu Waziri Mwanaidi

Aidha, amelishukuru Shirika la BRACK Maendeleo-Tanzania kwa kushirikiana na Serikali kujenga vituo 30 vya mfano kikiwemo kituo hivyo ambavyo vipo katika hatua tofauti za ujenzi katika Halmashauri sita.

“Pamoja na faida atakayoipata mtoto moja kwa moja, katika vituo hivyo ni kutoa  fursa kwa wazazi na walezi kupata muda wa kutosha kwa ajili ya kufanya shughuli za maendeleo ya watoto wakiwa vituoni na pia kuwaepusha watoto na hatari mbalimbali,"alisema Naibu Waziri Mwanaidi

Pia, Naibu Waziri Mwanaidi amesema kuwa mtoto asiyepitia katika vituo vya malezi na makuzi ya awali atakuwa tofauti na aliyepitia kwenye vituo kwa kuwa ataimarika katika stadi za kujifunza, ubunifu na uchangamshi kabla ya kujiunga na darasa la awali.

"Watoto wengi hasa wa vijijini ambako hakuna vituo vya malezi wanakosa huduma muhimu za malezi na misingi inayofaa katika maandalizi ya awali ya malezi na makuzi ya mtoto, hivyo kuwafanya baadhi ya wanaomaliza darasa la saba kuwa na uwezo na ubunifu mdogo,"amesema.

"Niwaombe  wadau wote wa maendeleo kushirikiana na serikali katika uanzishaji wa vituo hivyo katika maeneo wanayofanya kazi ili kuhakikisha kila kijiji na mtaa kunakuwa na kituo cha malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kama ilivyoainishwa katika mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025,"amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi Shirika la BRAC Tanzania Susan Bipa, amesema kuwa shirika hilo lilianza kujikita katika sekta ya elimu kwa watoto wadogo kupitia mradi wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya mototo mnamo mwaka 2016 chini ya ufadhili wa Mfuko wa maendeleo wa LEGO.

Amesema Mradi huo unaojulikana kama BRAC PlayLab, umekuwa ukitekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya ambapo vituo 80 vilitumika kutoa mafunzo kwa watoto zaidi ya 3,600 ambao walihitimu miaka miwili ya mafunzo na asilimia 96 ya watoto hao kuweza kuingia katika shule za awali kwenye maeneo husika.

No comments: