Advertisements

Sunday, June 20, 2021

Watendaji Ardhi Watakiwa Kuacha Tofauti


 Na Munir Shemweta, WANMM RUVUMA
Watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Ruvuma wametakiwa kushirikiana na kuacha tofauti zao kwenye utendaji kazi ili kuleta ufanisi na tija katika sekta hiyo.

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki na Afisa Utumishi wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Mwajabu Masimba alipozungumza na watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Ruvuma wakati wa kuadhimisha wiki ya utumishi wa umma.

Wizara ya Ardhi inaadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza tarehe 16 Juni 2021 na kufikia kilele tarehe  23 juni 2021 kwa kutembelea ofisi zake zilizoko pembezoni ambapo Wizara hiyo inatembelea ofisi zake za mikoa ya Ruvuma na Mtwara.

Alisema watumishi wa sekta ya ardhi hawatakiwi kutofautiana katika utendaji wowote wa kazi hata kama wako kada tofauti kwa kuwa taofauti yoyote itakayojitokeza haitaleta tija kwenye sekta ya ardhi.

Kwa mujibu wa Bi. Masimba, kufanya kazi maeneo ya pembezo si kama wamewatenga watumishi wa maeneo hayo bali ni sehemu ya majukumu na ndiyo maana Wizara ya Ardhi iliamua kupeleka timu ya maafisa wake ili kujua na kuzipatia ufumbuzi changamoto zao.

‘’Tushirikiane kila moja kwa kazi yake na mkumbuke muda mwingi tunautumia ofisini hivyo ushirikiano mtakaoufanya kwenye utendaji kazi na kuondoa tofauti utaifanya wizara kusonga mbele kwa kuwa taswira nzuri ya ofisi inajengwa na watumishi’’ alisema Masimba.

Naye Afisa Mipango Miji kutoka idara ya Maendeleo ya Mkazi Wizara ya Ardhi Bi. Emmile Mwasoge aliwatia moyo watumishi wa sekta ya ardhi  mkoa wa Ruvuma kuwa wasikate tamaa kutokana na changamoto zilizopo na kuwataka kuwa wavumilivu.

‘’Wapo wananchi wengi wanaotaka ajira hivyo ninyi mliobahatika kupata kazi mvumilie na mchape kazi mambo mazuri yatakuja tu’’ alisema Bi Mwasoge.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Ruvuma Ildefonce Ndemela aliwakumbusha watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa wake kuhakikisha wanatimiza wajibu wao wakati changamoto zao zikifanyiwa kazi.

Awali Watumishi wa sekta ya ardhi mkoa wa Ruvuma walieleza changamoto za kiutendaji na binafsi zinazowakabili katika maeneo yao ambapo baadhi yake ni upungufu wa watumishi na vifaa vya kutendea kazi kama vile magari.

Watumishi ambao Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Ardhi ilisikiliza chanagmoto zao ni kutoka Ofisi za Ardhi mkoa wa Ruvuma zinahusisha Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa, Halmashauri za Mbinga Mji, Mbinga DC, Tunduru, Manispaa ya Songea, Nyasa, Songea DC, Madaba pamoja na Halmashauri ya Namtumbo.

No comments: