ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, July 31, 2021

NAIBU WAZIRI MHANDISI KUNDO AMTUMBUA MENEJA WA TTCL KAGERA, SHIRIKA LA POSTA KAGERA KUCHUNGUZWA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akioneshwa jinsi mfumo wa malalamiko wa huduma kwa mteja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) unavyofanya kazi katika ofisi za Shirika hilo zilizopo Bukoba Mkoa wa Kagera. Anayemuelekeza ni Afisa wa Shirika hilo Theopista Lwakatare
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akizungumza na wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) Wilaya ya Bukoba alipozuru katika ofisi za Shirika hilo kukagua ukarabati uliofanyika wa jengo la Ofisi hizo.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye barakoa nyeusi) akiwa katika moja ya vibao vinavyoonesha majina ya barabara na mitaa ikiwa ni moja ya Miradi inayotekelezwa kupitia Wizara hiyo wa uwekaji na usimikaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi nchini
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye barakoa nyeusi) alipotembelea sehemu ya ukaguzi wa mizigo katika ofisi za TRA katika mpaka wa Mutukula uliopo Wilaya ya Missenyi Mkoani Kagera wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika eneo hilo la mpakani. Wengine ni watendaji alioambatana nao
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye barakoa nyeusi) pamoja na watendaji alioambatana nao wakikagua hali ya upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi na data katika mpaka wa Mutukula wilayani Missenyi
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye barakoa nyeusi) alipotembelea eneo ambalo ujenzi unaoendelea ikiwa ardhi ya eneo husika ni mali ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) kama nyaraka za umiliki wa eneo hilo zinavyoonesha, Mhandisi Kundo ametoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya hiyo kusitisha ujenzi na kufanya ufatiliaji wa mmiliki halali wa eneo hilo na kufikia muafaka
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akimsikiliza Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustine Kamuzora katika kikao cha ndani kabla ya kuanza ziara ya kukagua miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya za Bukoba, Missenyi, Kyerwa, Karagwe na Ngara zilizopo katika Mkoa huo.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye barakoa nyeusi) akiagana na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mkoa wa Kagera (wa pili kulia) Mhe.Moses Machali kabla ya kuendelea na ziara yake katika Wilaya ya Missenyi iliyopo katika Mkoa huo
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye barakoa nyeusi) katika picha ya pamoja na watendaji alioambatana nao katika ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu na data katika mpaka wa Mutukula wilayani Missenyi

Na Faraja Mpina, BUKOBA

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew ametengua uteuzi wa Meneja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wa Mkoa wa Kagera Bi. Irene Shayo kuanzia tarehe 30/07/2021 kwa kile kilichobainika kuwa taratibu za uteuzi wake zilikiukwa na utumishi wake umekuwa wa kusuasua, amekuwa akikwepa ziara za viongozi katika eneo lake pamoja na kupika taarifa za mapato na matumizi

Mhandisi Kundo ameyazungumza hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Kagera ambapo alitembelea ofisi za TTCL na Shirika la Posta Tanzania (TPC) na kuona kuwa Meneja wa TTCL katika Mkoa wa Kagera hatoshi kuwa katika nafasi hiyo ukizingatia Kagera ni mkoa wa kimkakati kwasababu unapakana na nchi takribani nne hivyo Meneja wake anatakiwa kuwa na uwajibikaji wenye ufanisi mkubwa

“Ninaagiza Meneja wa Mkoa wa Kagera aondoshwe mara moja katika Mkoa wa Kagera na kuanzia leo asitambulike kama Meneja wa Mkoa wa Kagera, taratibu zifuatwe na apangiwe kazi zingine kulingana na wasifu wake kitaaluma ili aweze kufanya kazi vizuri kwasababu majukumu ya sasa hana uwezo nayo”, alizungumza Mhandisi Kundo

Ameongeza kuwa wao kama Wizara kupitia kwa Waziri mwenye dhamana Dkt. Faustine Ndugulile wana kasi ya kutaka kuona matokeo ya kile ambacho Serikali imedhamiria kukifanya kwa watanzania katika Sekta ya Mawasiliano

Amesisitiza kuwa ili kufanikisha hilo ni wajibu wao kufanya maamuzi ya kuhakikisha taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo zinaimarisha mifumo ya utendaji kazi katika ngazi za mikoa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi mahitaji ya watanzania

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo alitembelea na kukagua ukarabati wa Ofisi za Shirika la Posta Bukoba zilizogharimu kiasi cha Shilingi Milioni 78,801,000 na kutorudhishwa na kiasi cha fedha kilichotumika kwasababu hakiendani na hali halisi ya ukarabati uliofanywa na kuagiza uchunguzi ufanyike ili kubaini gharama halisi zilizotumika katika ukarabati huo

“Nimetoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Moses Machali aunde kamati itakayohusisha wataalam wa Ujenzi, TAKUKURU na Ofisi ya Usalama wa Taifa (W) ili wakafanye tathmini na kujiridhisha kile ambacho kimefanyika na iwapo ikibainika kuna watu ambao wamefanya ubadhirifu wa fedha za umma watachukuliwa hatua za kisheria

Sambamba na hilo ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa TTCL na PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta kuhakikisha mameneja wao wa Mikoa ambao hawana vigezo na uwezo wa kuongoza Mikoa hasa ile ya kimkakati wanaondolewa na kuwekwa watu wenye uwezo na vigezo vya kuongoza katika Mikoa hiyo

Mhandisi Kundo yupo katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Kagera kwa ajili ya kukagua miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma za mawasiliano ambapo ametembelea katika wilaya ya Muleba, Bukoba na Misenyi na amepanga kuendelea katika Wilaya za Kyerwa, Karagwe na Ngara. Ziara yake katika Mkoa huo ilianza tarehe 29 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2021

No comments: