Na Eliud Rwechungura
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya kuwezesha vijana kufanya biashara na ujasiriamali ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kutengeneza ajira kwa vijana.
Waziri Prof. Mkumbo aliyasema hayo Julai 18, 2021 katika Maonesho maalum ya Harusi (Adorable Wedding Trade Fair) yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Dar es salaam yenye dhima ya ni kukuza tasnia ya harusi nchini Tanzania na kuwajengea uwezo watoa huduma wanaochipukia kufikia viwango vya kimataifa.
“Moja ya majukumu ambayo tumekabidhiwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ni kutengeneza ajira kwa vijana, Serikali haina uwezo wa kuwaajiri wahitimu wote, ila njia ya kuajiri vijana wengi ni kutengeneza mazingira ili vijana wafanye ujasiriamali, wafanye biashara kubwa na ndogo ndogo” ameeleza Prof. Kitila Mkumbo.
Aidha, Waziri Prof. Mkumbo amepongeza waandaaji wa maonesho hayo ambayo yamesaidia kukuza masoko ya biashara, bidhaa na huduma mbalimbali ambayo ni moja ya Majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara ya kuwezesha biashara ambazo sio rasmi na kuhakikisha zinatambulika rasmi
Maonesho hayo yamewakutanisha wapambaji, wapishi, waandaaji wa keki, watoa huduma za chakula, watoa huduma za honeymoon, wauzaji wa vito vya thamani, wakodishaji wa magari, washereheshaji – ma MC, ma DJ, watoa huduma za kumbi za sherehe, wapiga picha, na kadhalika.
Nae, Anna Lema Mkurugenzi Muandaaji wa Maonesho ya Adorable Wedding Trade Fair ameeleza kuwa Maonesho hayo yamekuwa na manufaa makubwa Sana kwa watoa huduma za Sherehe nchini Tanzania kwa kuweza kuwakutanisha Wafanyabiashara hawa na watoa huduma za Sherehe, Kada inayotoa ajira kwa wastani wa watu 23,250.
Anna Lema ameendelea kueleza kuwa kupitia maonesho hayo wafanyabiashara wamejiongezea wigo wa biashara na kutambulika lakini zaidi kupata mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma zao na wateja wamepata nafasi ya kuchagua huduma bora kutoka kwa Wafanyabiashara hao.
No comments:
Post a Comment