ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 19, 2021

Serikali Kuokoa Bilioni 33 Kwa Mwaka Kwa Ujenzi Wa Kiwanda Cha Dawa


 Na.Catherine Sungura, Makambako
Serikali itaokoa Bilioni 33 kwa mwaka kwa ajili ya ununuzi wa Dawa na Vifaa tiba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa viwanda vya dawa na Vifaa tiba kinachojengwa Mkoani Njombe.

Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.Dorothy Gwajima mara baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo Idofi-Makambako mkoani hapa.

“Hapa nimeangalia takwimu zako Mkurugenzi tunapoenda kukamilisha kiwanda hiki Cha mipira ya mikono(gloves), Dawa za vidonge (tablet), vidonge vya rangi mbili (Capsules) na dawa za maji(Syrup) Serikali kwa mwaka inakwenda kuokoa Bilioni 33 ambazo zingehitajika kununua mahitaji hayo”.

Aliongeza kuwa Serikali ingehitaji Bilioni 33 zaidi ili kwenda kununua dawa na Vifaa hivyo sehemu nyingine ndani au nje ya nchi lakini hizo Bilioni zinazoenda kuokolewa tunakua tumeshazalisha kwa gharama za uzalishaji kwa mwaka Bilioni 15.

“Ina maana hii Bilioni 33 inayobaki ukigawanya kwa milioni 700 ambayo ndio gharama za Kujenga vituo vya afya na Vifaa vyake kwa ‘force account’ Ni sawa na kujenga vituo vya afya 43”.Alifafanua Dkt.Gwajima

Alisema Mradi huo unafanya kutimiza azma ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na Ilani yake inayosimamiwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na uwezekano wa kupunguza gharama za kununua bidhaa ambazo tunaweza kuzitengeneza badala ya kuzinunua nje zitanunuliwa hapa hapa.

“Lengo ni kupunguza gharama za Serikali kutafuta mahitaji ya kuwahudumia wananchi Kwenye eneo la Afya hususani Watoto wachanga,Wajawazito na Wazee.

“Tunapowekeza kiwanda hiki hapa tunatekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi chini ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ,Serikali ya awamu ya sita kujielekeza Kwenye kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali”.Alisisitiza

Aidha, amewapongeza MSD kwa kusimamia mradi huo kwa kutoka Kwenye maandishi na kwenda Kwenye uhalisia”Nawapongeza sana Bodi,Uongozi na Wafanyakazi wote wa MSD kwa kusimamia Jambo hili kwani sio Jambo jepesi, na lina Vita vya kutosha,sio watu wote wanapenda ilani itekelezwe au Serikali ichukue muelekeo wake inayoitaka lakini nyinyi mmesimania na endeleeni hivyo hivyo na ilani lazima itekelezwe”.

Dkt.Gwajima hakuacha kuwapongeza Viongozi na wananchi wa Mkoa wa Njombe hususani Makambako kwa kutoa eneo Hilo kwa kujua thamani ya kitu kinachowekezwa hapo kinaenda kuhudumia nchi nzima na majirani zake.

“kwahiyo lazima tutambue mchango mkubwa wa wana Makambako na wao watakua wa kwanza kufaidika,sitotarajia kusikia Njombe hawana ‘gloves’ au dawa na kiwanda kipo hapa kwani mcheza kwao hutunzwa”.

Hata hivyo amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa MSD kutekeleza ombi la Mbunge wa Jimbo la Makambako Mheshimiwa Deo Sanga la kuwaletea ‘Utra Sound’ ndani ya miezi miwili kwa ajili ya kituo Cha afya Makambako,aliongeza wanathamini pia maombi ya mahitaji ya Vifaa tiba Kwenye Mikoa mingine Serikali inajipanga kwa Mikoa mingine.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa MSD Meja Jenerali Gabriel Mhidze(Dkt) amesema ujenzi wa kiwanda Cha Mipira ya Mikono kimefikia asilimia 90 na kukamilika kwa ujenzi huo Wizara itakua imepiga hatua kubwa kwa upatikanaji wa dawa nchini.

Alisema kiwanda Cha Mipira ya Mikono kitakuwa na uwezo wa kuzalisha ‘gloves’ 20,000 kwa saa sawa na jozi 10,000 na hivyo kufanya uzalishaji wa jozi 86,400,000 kwa mwaka.

Kwa upande wa ujenzi wa viwanda vya vidonge,dawa za maji na vidonge vya rangi mbili ujenzi huo umekamlika kwa asilimia 90 na kinatarajia kuzalisha vidonge 425,000 kwa saa,rangi mbili kuzalisha vidonge 330,000 kwa saa na dawa za maji kuzalisha chupa 150 mpaka 180 kwa saa zenye ujazo wa mls.100.
-Mwisho-

No comments: