Advertisements

Tuesday, May 24, 2022

WIZARA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI KUJENGA UCHUMI WA KIDIJITALI


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, akizungumza wakati wa kikao na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika Mei 23, 2022, jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye(Mb) akimkabidhi cheti na nyaraka za michoro Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mhandisi Peter Ulanga inayoonyesha jinsi na namna miundombinu ya Mkongo wa Taifa ulivyojengwa kutoka Mangaka-Mtambaswala (kilomita 72) na Arusha-Namanga (kilomita 105) ili kuliwezesha shirika kusimamia na kuendesha Mkongo huo 
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakifurahi na kupongezana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi mara baada kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika Mei 23, jijini Dodoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (wa katikati aliyeketi) akiwa katika picha ya Pamoja na Wakandarasi wa Mkongo wa Taifa uliokamilika mwaka 2021/2022 mara baada ya Waziri Nape kuzungumza na Wakandarasi hao kwenye kikao kazi na Wakandarasi kuhusu ujenzi wa Km 4,442 za Mkongo wa Taifa kilichofanyika Mei 23, jijini Dodoma.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amefanya kikao na Wakandarasi wajenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Mei 23 jijini Dodoma ambapo amesema kuwa Wizara anayoisimamia ipo tayari kujenga uchumi wa kidijitali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi.

Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia inaamini katika ushirikiano na Sekta Binafsi katika kuendesha shughuli zake kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi akitolea mfano wa nchi jirani ya Kenya ambayo takwimu zinaonesha sehemu kubwa ya Mkongo wa Mawasiliano umejengwa na Sekta Binafsi kuliko uliojengwa na Serikali ambapo imesaidia ufikishaji wa huduma za mawasiliano kuwafikia watu wengi zaidi

“Inawezekana hapa na pale Sekta Binafsi imekutana na mawimbi mbalimbali lakini tunawahakikishia kuwa mawimbi yametulia na tupo tayari kufanya kazi pamoja na tuwahakikishie kuwa tutawalinda ili mradi mtimize wajibu wenu na mfanye kazi kwa kuzingatia muda, viwango na ubora wa kimataifa”, amezungumza Waziri Nape

Waziri Nape amesema kuwa wakandarasi wazawa wanafanya vizuri na ni matamanio ya Serikali idadi yao izidi kuongezeka ambapo amesema kwa mwaka wa fedha unaomalizika Juni 30, 2022 jumla ya Mikataba 22 ya ujenzi wa kilomita 4,442 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano imeingiwa baina ya Wizara na Wakandarasi 8 ambao kati yao wakandarasi 6 ni wazawa na wakandarasi 2 wanatoka katika kampuni za nje zilizosajiliwa nchini

“Niliwaambia watendaji wa Wizara ninayoisimamia kuwa kila mmoja ni zawadi kwa mwenzke, kwetu sisi hata wakandarasi ni zawadi ya Mungu kwa Wizara yetu na ndo maana tupo hapa tunawapenda na tunawajali, tutahakikisha tunafanya kazi pamoja, uwepo wenu unachangia mafanikio yetu, nyie mnatuhitaji na sisi tunawahitaji

Ameongeza kuwa Wizara hiyo bado ina kazi kubwa ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kidijitali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano, hivyo fursa za kuendelea kufanya kazi na wakandarasi hao bado zipo lakini kipimo cha kuendelea kufanya kazi na Wizara hiyo ni kukamilisha kazi kwa kiwango, ubora na muda uliopangwa

No comments: