ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 16, 2023

ASILIMIA 41 WENYE VVU WAMEPATA MIMBA ZISIZOTARAJIWA

Taasisi ya Afya ya Ifakara imebaini kuwa asilimia 41 ya wanawake wanaoishi na virusi vya Ukimwi (VVU) Mkoa wa Dar es Salaam wamepata mimba zisizotarajiwa.

Hali hiyo imeelezwa kutokea kutokana na asilimia 60 ya wanawake wanaoishi na virusi hivyo, kutotumia njia za uzazi wa mpango.

Hayo yamebainishwa Juni 15, 2023 na Mtafiti kutoka Taasisi ya utafiti ya Ifakara Dk Francis Levira wakati akitoa wasilisho kuhusu utafiti huo uliofanyika katika miji ya Dodoma na Dar es Salaam mwaka 2021/22.

“Wakinamama ambao tuliwahoji, tuliwauliza kuwa mimba au uzazi wa mwisho kama ulikuwa umepangiliwa au haujapangiliwa na katika majibu tulipata Dodoma asilimia 29 na Dar es Salaam ilikuwa kubwa kwa asilimia 41, walipata mimba zisizotarajiwa”amesema Dk Levira.

Dk Levira amesema utafiti huo pia ulihusisha zaidi ya watu 15,000 ili kufahamu watu wangapi wanajua kama wana maambukizi na kutoa huduma ya upimaji.

Aidha Dk Levira amesema kati ya wanawake wenye virusi vya ukimwi ambao walifika kupata huduma kwenye vituo vya Afya ni asilimia 6 pekee ndio walikiri kupata huduma za uzazi wa mpango.

Akizungumzia kuhusu maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto amesema utafiti umeabaini kati ya wanawake wenye virusi walioohojiwa ni asilimia 2 waliwaambukiza watoto wao virusi vya Ukimwi Mkoani Dodoma huku Dar es Salaam ikiwa kwa 8 asilimia.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya ustawi na maendeleo ya jamii Fatma Taufiq amesema Serikali itumie tafiti hiyo kuboresha miundombinu ya vituo vya afya ili waathirika wanaofika vituo vya afya wapate na huduma za uzazi wa mpango.

Taufiq amesema huduma hiyo pia itasaidia kuwaeleza waathirika hao namna bora ya kuzuia watoto wao wasipatwe na virusi vya Ukimwi.

Chanzo: Mwananchi

No comments: