Mbembwe, shangwe na kauli za kumsifu Rais Samia Suluhu Hassan ndizo zilitawala wakati Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2023/24 ya Sh44.38 trilioni.
Dodoma. ‘Mama yuko kazini, pochi la mama’. Ndiyo maneno aliyoyatumia mara kwa mara Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akisoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 ya Sh44.38 trilioni.
Si hivyo tu, Dk Nchemba pia alitumia maneno ‘mama apewe maua yake’ pale alipowataka wabunge kushangilia yale mazuri aliyotamka kwenye hotuba yake.
Alitumia maneno hayo na mengine ya kukisifia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kusema,“kila Mtanzania anayezaliwa ni CCM” huku akimsifu Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo kwa kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama hicho kwenye miradi ya utekelezaji ya Serikali.
Aidha, katika kitabu chake cha bajeti chenye kurasa 235 mbali na kutumia maneno hayo, lakini maneno ya Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo yalitawala kwani aliyatamka mara 46.
Ayatamka kwa muktadha tofauti hasa alipokuwa anazungumzia kazi nzuri alizozifanya tangu alipoingia madarakani Machi 19 mwaka 2021 kufuatia kifo cha mtanguzi wake, Rais John Magufuli kilichotokea Machi 17, 2021.
Maneno mengine yaliyotumika ni ‘pochi la mama’, mama ameanzisha, sote tumuunge mkono na jingine ni mama amedhamiria kufikisha umeme nchi nzima.
Waziri aliwasili bungeni saa 10.01 jioni akiwa kwenye msafara wa magari sita yakiongozwa na pikipiki ya askari wa usalama barabarani, akiwa ameongozana na baadhi ya maofisa wa wizara hiyo akiwamo Katibu Mkuu, Dk Natu Mwamba. Pia, Dk Mwigulu aliongozana na mkewe Neema.
Dk Nchemba baada ya kuwasili alishuka ndani ya gari akiwa amevalia suti yenye rangi nyeusi na kama kawaida yake akiwa amevaa tai yenye rangi za bendera ya Taifa aliuonyesha mkoba wenye Bajeti ya Serikali kwa waandishi wa habari kwa ajili ya kupata picha za kumbukumbu.
Jana Alhamisi Juni 15, 2023, ni siku ambayo Serikali za nchi za Afrika Mashariki kutangaza bajeti zao kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2023/24.
Kama ilivyo ada, wakati Dk Mwigulu anaingia ndani ya ukumbi wa Bunge aliongozwa na askari wa Bunge huku wabunge wakimshangilia kwa kupiga meza na alianza kuisoma saa 10.03 jioni na alimaliza kuisoma jioni ya saa 12.13.
Dk Mwigulu baada ya kufika kwennye eneo la kusoma Bajeti yake aliweka mezani mkoba na kuufungua na alitoa kishikwambi kilichokuwa na hotuba yake.
Amesoma bajeti kwenye kishikwambi kama zilizofanywa bajeti za wizara 23 yakiwamo maoni ya kamati mbalimbali za Bunge, hii ni kuonesha maendeleo ya teknolojia ambapo miaka ya nyuma hotuba za bajeti bungeni zilisomwa kwenye karatasi.
Hata hivyo, alipoanza kusoma mapendekezo ya Serikali kwenye kodi, Dk Mwigulu alifungua mkoba na kutoa miwani.
Pia, kwa maendeleo hayo ya teknolojia, wabunge nao walikuwa wakifuatilia hotuba ya bajeti kupitia kwenye vishikwambi vyao.
Hata hivyo, wageni waalikwa walifuatilia hotuba ya bajeti kwenye vitabu walivyogawiwa ndani ya Bunge.
Baadhi ya wasaidizi wa viongozi, madereva na maofisa wengine walifuatilia hotuba ya bajeti ndani ya kantini ya Bunge ambayo ina seti tatu za TV zinazowazesha wateja waliomo humo kuweza kuona kwa eneo lolote atakalokuwa amekaa.
Kabla ya Waziri wa Fedha kuwasili bungeni, wageni mbalimbali waalikwa walianza kuwasili kuanzia saa nane mchana, wakiwamo viongozi wa Serikali, taasisi za umma na vyama vya siasa.
Miongoni mwa viongozi wakuu wa Serikali alikuwapo Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka, Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Emmanuel Tutuba, makatibu wakuu na mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchini zao
No comments:
Post a Comment