ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 19, 2023

KADINALI PENGO AJITOSA SAKATA LA BANDARI, AIBUA MASWALI MAWILI


Askofu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo

Je, tunataka kupata fedha nyingi zinazotokana na bandari? au Watanzania wawe na uwezo mkubwa wa kuendesha bandari yetu? Ni maswali mawili yaliyoibuliwa na Askofu mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Kadinali Polycarp Pengo kuhusu sakata la mkataba wa ushirikiano wa uendeshaji bandari kati ya Tanzania na Kampuni ya DP World ya Dubai.

Maswali ya Askofu huyo mstaafu, yanakuja kipindi ambacho tayari Bunge limeridhia mkataba huo licha ya kuwepo kwa baadhi ya majadiliano kinzani kwa wananchi.

Askofu Pengo aliibua maswali hayo jana, wakati akifanyiwa mahojiano na chaneli ya mtandao wa Youtube inayomilikiwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), huku akitaka viongozi wa Serikali kutafakari kwa kina kabla ya kufanya maamuzi.

Katika mahojiano hayo amesema licha ya kwamba yeye sio mchumi wala mwanasiasa lakini kazi ya uongozi wowote wa nchi ni kuendeleza kwanza binadamu.

“Katika suala la bandari bila shaka Serikali inaona inaweza kunufaika zaidi kutokana na kumleta mwekezaji wa kutoka nje, lakini mimi najiuliza hiyo itakuwa ni kusudi tupate fedha zaidi kuliko tunavyopata au kumfanya Mtanzania aendelee na kumfanya awe na uwezo zaidi katika mazingira ya nchi yake?,”amehoji.

Katika maelezo yake, Kadinali Polycarp amedai hilo ni swali gumu kwake huku akidai kwa kuzingatia maadili yake amewataka viongozi wa Serikali kutambua kwamba jukumu walilonalo mbele yao ni kumuendeleza Mtanzania.

“Mtanzania akishindwa huwezi kumtupa na kusema unaweza kupata fedha nyingi kwa kumleta mgeni na kumuacha Mtanzania katika uvivu wake akae huko,”amesema.

“Huwezi uka-Subject binadamu kwa faida ya fedha ukamfanya awe mtumishi wa fedha, huwezi kumfanya hivyo na haiendi. Ni hilo tu nadhani nisiseme zaidi,”amesema

Serikali yataja sababu
Hata hivyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akizungumza na viongozi wa dini jijini Dar es Salaam wiki iliyopita alisema sababu ya kusaini mkataba huo wa uendeshaji wa bandari ni kutokana na ufanisi mdogo wa bandari nchini.

Ametoa mfano mmoja kwamba wastani wa meli kusubiri nangani kwa Bandari ya Dar es Salaam ni siku tano ikilinganishwa na siku moja na saa sita kwa Bandari ya Mombasa. Pia, amesema Bandari ya Durban huko Afrika Kusini, meli inakaa kwenye nanga kwa siku moja na saa 13.

"Ufanisi mdogo wa Bandari ya Dar es Salaam unatokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa mifumo ya kisasa na kutokuwepo kwa maeneo ya kutosha ndani na nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhia shehena pamoja na eneo la maegesho ya meli," alisema.

Kutokana na changamoto hizo, Serikali ilitafuta mwekezaji kwa ajili kuongeza ufanisi wa bandari hiyo, ndipo akapatikana Kampuni ya DP World, wakaingia mkataba wa makubaliano ambao utawaongoza kwenye mikataba itakayofuata.

Kwa upande wake, mwenyekiti aliyeongoza majadiliano baina ya pande mbili kwenye mkataba huo, Hamza Johari amesema mkataba huo unakwenda kuifanya Bandari ya Dar es Salaam kuwa ya kisasa badala ya kuwa ile ya kupakua na kupakia mzigo.

"Modern port (bandari ya kisasa) maana yake unaufuata mzigo kwa mzalishaji hukohuko na kuuleta hadi bandarini, kisha unaupeleka hadi kwa mwagizaji, hii tunaita end to end port. Tunataka kwenda huko," alisema.

Johari ametumia nafasi hiyo kufafanua mkataba huo kifungu kwa kifungu na kuwaeleza viongozi wa dini namna mkataba huo utakavyokuwa na manufaa kwa Tanzania na kuifanya bandari ya Dar es Salaam kuwa ya kisasa.

"Hii itifaki siyo mkataba wa utekelezaji, ni makubaliano yanayoweka mawanda ya ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya DP World," alisisitiza Johari ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga (TCAA).


No comments: