Advertisements

Wednesday, June 7, 2023

MFUKO WA UTAMADUNI NA SANAA NI WA WADAU WOTE WA SEKTA HIZO


Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana leo bungeni jijini Dodoma, amewasilisha Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Katika hotuba hiyo, Waziri Chana ameeleza kuwa mikopo inayotolewa kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa inatolewa kwa wadau wote wa sekta hizo ambao wamekidhi vigezo.

Akijibu hoja mbalimbali za Wabunge waliochangia bajeti hiyo, Mhe. Chana amesema upatikanaji wa Vazi la Taifa umefikia hatua ya kukusanya maoni na tayari wadau wa Tanzania Bara na Zanzibar wameshatoa maoni yao kwa Kamati na Kamati inaendelea kuyafanyia uchambuzi.

"Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limeendelea kuleta mageuzi ya kuboresha muziki wa kizazi kipya kwa kutengeneza Kivunge cha Mtozi yaani Producers’ Kit chenye zaidi ya vionjo 400 vyenye ladha ya asili ya kitanzania", amesema Mhe. Chana.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesisitiza wanaotumia kazi za Sanaa kuhakikisha wanalipa mirabaha kwa Wasanii ambapo ameendelea kusisitiza kuwa watakaokiuka watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.

Ameongeza kuwa, Wizara ina maelekezo ya kujenga viwanja viwili vya michezo katika Jiji la Arusha na Dodoma na miongoni mwa vyanzo vya mapato ni CSR za miradi mikubwa katika sekta za fedha, nishati na madini na tayari Wizara imeanza kufanya mawasiliano na Wizara husika na mawasiliano yanaendelea vizuri.

Nae Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba akichangia hoja hizo za Serikali amesema kuwa, Wizara yake itahakikisha Mipango ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo inatekekeza majukumu yake kwa kutoa fedha kwa wakati, huku akialika Sekta Binafsi kuona fursa zilizopo katika Michezo, Utamaduni na Sanaa na kuwekeza.

Bunge limepitisha Bajeti ya Wizara hiyo ya jumla ya shilingi bilioni 35.4 kwa mwaka wa fedha 2023/23 katika kutekeleza majukumu yake ya kutoa furaha kwa Watanzania.

No comments: