Siku mbili baada ya kuondoka hospitalini, kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki, Papa Francis alianza tena desturi yake adhimu ya Jumapili, ya kusalimia umma katika uwanja wa St. Peters.
Alianzia kwa kuonekana dirishani akisema kwamba ukaribu wa kibinadamu na wa kiroho aliohisi alipokuwa hospitalini, akifanyiwa upasuaji wa tumbo ulimpa "faraja kubwa."
Maelfu ya mahujaji na watalii katika uwanja huo, walishangilia kwa kupiga makofi alipofika kwenye dirisha hilo. Papa Francis alisikika akipungukiwa na pumzi wakati fulani, lakini alionekana kufurahia kurejelea majukumu yake.
Mwishowe, umati ulisikika ukisema "Maisha marefu papa!" naye kwa haraka akasema, “Asante” kabla ya kuondoka dirishani. Papa Francis pia alielezea masikitiko yake kwa ajali ya boti ya wahamiaji iliyoanguka, ikitokea Ugiriki na kulaani shambulio dhidi ya wanafunzi nchini Uganda.
Madaktari wa papa wamemtaka afanye shughuli zake kwa utaratibu kufuatia upasuaji huo. Vatican imetangaza kwamba kiongozi huyo wa kidini atampokea rais wa Brazil Jumatano mchana, lakini ikaongeza kwamba ili kuhakikisha kuwa anaendelea kupata nafuu kwa uzuri, hataongoza hafla ya hadhira ya jumla ya Jumatano katika Uwanja wa St. Peters.
Mapema mwezi Agosti mwaka huu, Papa Francis atafanya hija nchini Ureno, ambako ataongoza hafla ya vijana. Mwishoni mwa mwezi huo, atasafiri kwa ndege hadi Mongolia kwa ziara ambapo, atakuwa papa wa kwanza kutembelea nchi hiyo ya bara Asia.
No comments:
Post a Comment