ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 14, 2023

WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TAASISI YA UONGOZI KUTOA TAFITI ZA KIMKAKATI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akizungumza na watumishi wa Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Katikati ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwan Kikwete na mwingine ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiangalia ofisi ya Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa taasisi hiyo. Aliombatana nao ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na katikati ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa taasisi yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo katika taasisi hiyo jijini Dar es Salaam iliyolenga kuhimiza uwajibikaji.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watumishi wa Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao. Wa pili kulia waliokaa ni Naibu Waziri wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete na wa pili kushoto waliokaa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo

Na. Lusungu Helela-Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameitaka Taasisi ya UONGOZI (UONGOZI Institute) kufanya tafiti za kimkakati zitakazoweza kuibua masuala mbalimbali ya kiuongozi kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii.

Waziri Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Taasisi ya UONGOZI jijini Dar es Salaam, ikiwa ni muendelezo wa kuzungumza na Watumishi kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema tafiti hizo zinatakiwa zilenge katika kuibua mijadala ambayo itachagiza dhana ya utawala bora kwa kujikita zaidi kuibua changamoto zinazosababishwa na viongozi wenyewe Barani Afrika.

“Tunataka mje na tafiti zitakazosomwa duniani kote ambazo zitaleta ukombozi kwa wananchi wa Bara la Afrika hususan katika masuala ya uongozi mfano kwenye suala la rushwa” amesema Mhe. Simbachawene

Amefafanua kuwa kwenye masuala ya uongozi bado kunahitajika tafiti nyingi ambazo zitatoa dira ya kuwaandaa viongozi vijana wenye mtazamo wa kimapinduzi.

Katika hatua nyingine Mhe. Simbachawene ameipongeza Taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya ya kuwaandaa viongozi wa ndani na nje ya nchi pamoja kukutana na kuzungumza na viongozi mbalimbali.

“Ninajivunia kwa kazi zenu kwani huko nje taswira yenu ni kubwa mno na ya kimataifa kutokana na jitihada zenu mnazofanya za kuhakikisha Afrika inakuwa na viongozi wenye kuwahudumia wananchi ” amesisitiza Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwan Kikwete ameihimiza Taasisi hiyo kuendelea kuandaa viongozi wa baadae watakaoweza kuendeleza mazuri yanayofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Bw. Kadari Singo akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi yake, amesema atatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa ikiwa pamoja na kutoa tafiti zitakazoleta matokeo chanya katika jamiii na taifa kwa ujumla.

No comments: