Friday, January 19, 2024

JWTZ WAPELEKA VIJANA KUJENGA NYUMBA 5000 MSOMERA

JESHI la Wananchi Tanzania limeleta vijana kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 5000 katika eneo la Msomera, hadi sasa tayari wamefyatua matofali ya kujenga nyumba 2,559.

Shukrani za juhudi zote zinazofanyika katika eneo hili la Msomera, zinaelekezwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ndiyo aliyeidhinisha pori hili la akiba kujengwa makazi mapya.

Katika eneo hili, zimepangwa zijengwe barabara zenye urefu wa KM 800 ambapo mpaka sasa KM 150 zimekamilika, mpaka sasa jumla ya visima 10 vimeshachimbwa na vingine vinaendelea kuchimbwa na umeme umeanza kusambazwa.
Shule ya Msingi imeshakamilika, Shule ya Sekondari ya kisasa yenye maabara za masomo ya sayansi, TEHAMA na Maktaba, Zahanati, Kituo cha Polisi vinaendelea kujengwa.

Mnada umeshajengwa, malisho ya mifugo yameshapimwa na vituo vya kuuzia mazIwa vinaendelea kujengwa.

Mawasiliano tayari yameshafikishwa na hatua inayofuata ni Mfuko wa Mawasiliano Tanzania kuendelea na usambazaji wa minara ya mawasiliano kwa kushirikiana na Kampuni binafsi za simu.

Majosho yanaendelea kujengwa na upimaji wa viwanja unaendelea .
Katika awamu ya pili, kufikia Januari 12, 2024, kaya zilizojiandikisha kuhama kwa hiari kutoka Ngorongoro ni 525, kati ya kaya hizo, 126 zenye watu 812 na mifugo 2,581 tayari zimeshahama.

Kaya zilizohama zimegawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza lenye kaya 74 lenye watu 520 na mifugo 1,599 limekuja Msomera na kundi la pili la kaya 52 lenye watu 292 na mifugo 982 wamechagua kwenda kwenye mikoa mbalimbali.

Kwa ujumla wake, mpaka sasa kaya 677 zimeshahama kwa hiari kutoka Ngorongoro zikiwa na watu 3,822 na mifugo 18,102.

Zoezi la uhamaji kwa hiari linaendelea, Januari 18, 2024, kutakuwa na kundi lingine la kaya 72 lenye watu 515 ambalo litaondoka Ngorongoro.

Ujenzi wa nyumba 1,000 uko katika hatua mbalimbali za ukamilikaji wake.

Uondokaji wa wananchi kutoka Ngorongoro kwenda Msomera kutasaidia eneo la Ngorongoro kuondoa tatizo la mmomonyoko wa ardhi na uchafuzi wa aina ya mimea pamoja na kuondoa tatizo la magonjwa ya wanyamapori kuingiliana na mifugo.

Nawashauri wote wenye mashaka na zoezi la kuhamisha watu kutoka Ngorongoro waje wauone ukweli na baada ya hapo wenye nia njema watasema ukweli. Serikali ina nia njema, hakuna muda ambao itakaa chini kwa ajili ya kufanya maamuzi yatakayoumiza wananchi wake.

No comments: