“Kwa majonzi makubwa nasikitika kutangaza kifo cha Rais mstaafu wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo Februari 29 saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya saratani ya mapafu.
Mkuu huyo wa nchi amesema, kutokana na kifo hicho, bendera zitapepea nusu mlingoti kwa siku saba kuanzia kesho Ijumaa, Machi 1, 2024.
Mzee Mwinyi amefariki dunia akiwa na miaka 98 na miezi tisa na siku 21. Sawa na siku 36,091.
Historia ya Mwinyi
Mei 8, 1925, ndio tarehe ambayo Mwinyi alizaliwa. Kijiji cha Kivure, Wilaya ya Mkuranga, Pwani.
Mwinyi akiwa mtoto, alipelekwa Zanzibar kusoma madrasa (elimu ya dini ya Kiislam). Tangu hapo, Mwinyi alikulia na kusoma Zanzibar hadi kufikia daraja kubwa la uongozi.
Mwaka 1933, Mwinyi akiwa na umri wa miaka minane, aliandikishwa kuanza masomo, Shule ya Msingi Mangapwani, Unguja, Zanzibar. Alisoma hapo darasa la kwanza mpaka la nne, alilohitimu mwaka 1936. Alipomaliza darasa la nne, Mwinyi alijiunga na Shule ya kati (middle school), katika Shule ya Dole. Alisoma darasa la tano mpaka la nane mwaka 1942.
Mwaka 1943, Mwinyi alijiunga na Chuo cha Ualimu Zanzibar, aliposoma ngazi ya cheti. Alitunukiwa astashahada ya ualimu mwaka 1944. Mwinyi alijiendeleza zaidi kwenye fani ya ualimu kwa kusoma Astashahada Kuu ya Ualimu (General Certificate in Education ‘GCE’), kisha Stashahada ya ualimu, kupitia Chuo Kikuu cha Durban, Uingereza.
Mwaka 1961, Mwinyi alisoma na kuhitimu astashahada ya ufundishaji kwa lugha ya Kiingereza kupitia Taasisi ya Regent, London, Uingereza. Mwinyi pia alisoma kozi ya ukufunzi kwa mwaka mmoja, kuanzia mwaka 1961 hadi 1962, Chuo Kikuu cha Hall, Uingereza.
Mwinyi alisoma Lugha ya Kiarabu Chuo Kikuu cha Cairo, Misri mwaka 1972 mpaka 1974. Hii inamaanisha kuwa Mwinyi ni mwalimu mbobezi katika lugha tatu, Kiingereza, Kiarabu na Kiswahili.
No comments:
Post a Comment