ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 9, 2024

SERIKALI YADHIBITI WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU


Na Happiness Shayo-Dodoma
Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inadhibiti wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) Februari 8,2024 Bungeni jijini Dodoma wakati wa kuchangia hoja ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

“Nipende kuwahakikishia waheshimiwa wabunge kuwa tunaendelea kuchukua hatua za dhati kabisa, hata Rais alipofanya ziara katika Mkoa wa Lindi alielekeza kamati zetu za ulinzi na usalama lakini alituelekeza pia na sisi tuweze kutafuta mwarobaini wa changamoto hiyo ya muingiliano kati ya wanyamapori na binadamu” Mhe. Kairuki amesisitiza.

Ametaja mbinu mbalimbali zinazotumika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kuwa ni pamoja na kuchimba mabwawa ya maji ndani ya hifadhi, kutumia teknolojia ya drones katika doria, udhibiti na ulinzi, kuweka fensi ya umeme na kutumia mfumo wa kielektroniki wa Geofencing kwa kadri Serikali inavyopata fedha.

Aidha, amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua ya kuongeza vituo vya askari ambapo ndani ya miaka miwili vimejengwa vituo vya askari 16 na mwaka huu vitajengwa vituo vingine 16 na ni zoezi endelevu litakalofanyika katika maeneo yanayopakana na hifadhi.

Kuhusu utangazaji wa vivutio vya utalii, Mhe. Kairuki amesema Serikali itaendelea kutangaza na kubuni mikakati mbalimbali kuhakikisha inaongeza idadi ya watalii sambamba na kuongeza uwekezaji hasa katika kufanya ujenzi wa vyumba vya malazi ili watalii waweze kupata malazi pindi wanapotembelea hifadhini.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa pendekezo la kuunda mfuko maalum wa utalii ambapo amefafanua kuwa imeundwa kamati ya kimkakati inayofanya uchambuzi wa suala hilo.

No comments: